Majaliwa apiga 'stop' michango holela mashuleni

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Muktasari:
- Agizo hilo amelitoa leo Ijumaa, Novemba 24, 2023 wakati akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Ivugura Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe.
Songwe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya walimu kuwafukuza watoto muda wa masomo kwa madai ya kushindwa kutoa michango ambayo ameiita ya ovyo.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 24, 2023 wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ivugura mara baada ya kuwasha mradi wa usambazaji nishati ya umeme unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
“Sitaki kusikia wanafunzi wanafukuzwa kwa madai ya kushindwa kutoa michango ya ' ovyo' na walimu kutoa vitisho kuwa wasipochangia watafukuzwa, nasema hilo halipo,” amesema.
Ameongeza kusema: “Unakuta mwalimu anasema leteni mchango wa Sh200 mara Sh500 hiyo haipo Rais Samia Suluhu Hassan alishasema elimu bure sitopenda kusikia mtoto karejeshwa nyumbani kwa ajili ya kushindwa kutoa michango ya ovyo.”
Majaliwa amesema ipo michango ambayo kama vyoo vimebomoka lakini upo utaratibu unaotumika, hiyo michango ya ovyo hizo pesa waachieni wazazi wafanya matumizi ya nyumbani kwa familia,” amesema.
Amesema Rais amewekeza kwenye sekta ya elimu ya Msingi, Sekondari na Taasisi za elimu ya juu lengo ni kuona wanafanya vizuri katika kuzalisha viongozi wajao na sio vinginevyo.
“Walimu hayo ya michango ya ovyo hayapo, acheni watoto wapate elimu, sambamba na kukemea vijana wanaojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wa kike,” amesema.
Ameongeza kuwa “Vijana acheni wanafunzi wa kike wasome mnapaswa kutambua ukibainika kuishi kinyumba na mwanafunzi au kumpatia ujauzito ni kifungo cha miaka 30 gerezani sasa upige hesabu ya umri ulio nao na kuongeza kifungo hicho.”
Aidha katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wazee wa Mira (Machifu) kushirikiana na Serikali kukemea vitendo hivyo kwani wao ni sehemu ambayo inategemewa na Serikali.
“Machifu Serikali inawatambua mchango wenu tunaomba kuwa kipaumbele kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiserikali, tunatambua kiongozi wenu Mkuu ni Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mmekuwa mkizungumza mambo mbalimbali kwa maslai mapana kwa taifa ”amesema.
Kwa upande wake, Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Songwe, Juliana Shonza ameishukuru Serikali kwa kuwekeza katika sekta ya elimu na afya jambo ambalo limesaidia jamii kupata huduma bora kwa urahisi.
“Ndugu sote ni mashahidi Serikali ya awamu ya sita imeleta mambo mengi makubwa hivyo ni matarajio yetu mwaka 2025 kura za Rais Samia Suluhu Hassan zitakuwa za kishindo,” amesema.