Serikali kuzitafutia ufumbuzi kero Mlima Kitonga

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani, Salim Abri Asas akielezea changamoto zilizo katika eneo la Mlima Kitonga.
Muktasari:
- Serikali imeanza kutafuta ufumbuzi ili kumaliza kero za mlima wa Kitonga ikiwamo ajali na foleni.
Iringa. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema tayari Serikali imeanza kushughulikia kero za Mlima Kitonga unaounganisha mikoa saba na nchi mbalimbali za kusini.
Zaidi ya Sh6 bilioni zinatarajia kutumika katika kupata suluhisho la mda mfupi ili kupunguza kero za barabara kwenye mlima huo.
Miongoni mwa kero zinazo lalamikiwa katika mlima huo ni ajali na kufunga kwa barabara wakati ajali hizo zinapotokea.
Nyingine ni msongamano wa magari na kuoza kwa bidhaa hasa mali mbichi wakati inapotokea ajali na barabara hiyo kutopitika.
Akizungumza baada ya kutembelea Kitonga, Bashungwa amesema "Ndugu wamepotea, mali na muda umepotea kwa sababu ya changamoto ya barabara, tunatafuta suluhisho la muda mfupi na mrefu la kuondoa kero ya barabara hii."
Amesema tayari wameshapata mhandisi mshauri ili kupata suluhisho la muda mrefu kwenye barabara hiyo.
Bashungwa katika mambo aliyooagizwa kuyasimamia na Rais Samia Suluhu Hassan, moja wapo ni kutafuta suluhisho la haraka ili kumaliza kero za mlima Kitonga.
Mwenyekiti wa Usalama Barabarani ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapindui (CCM), Salim Abri Asas amesema licha ya ajali, Kitonga ni eneo linalopunguza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Awali Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa (Tanroads), Mhandisi Yudas Msangi, amesema tayari wameshafanya utafiti na kupata suluhisho la muda mfupi.
Amesema Sh6.4 zitatumika kwa ajili suluhisho hilo ambapo wanatarajia kupasua baadhi ya miamba kwenye maeneo hayo na kuweka taa kwenye kila kona ili madereva waweze kuona.
Msangi amesema Suluhu ya muda mrefu ni kujenga njia ya mchepuo yenye urefu za zaidi ya kilomita 30, nyuma ya mlima huo.
Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga amesema kati ya kero kubwa anayokabiliana nayo kwenye jimbo hilo ni pamoja na changamoto za Mlima Kitonga.