Bashungwa awaweka mtegoni Tanroads

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akitoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali mara baada ya kukagua miundombinu ya ujenzi wa barabara njia nne katika eneo la Nsalaga jijini Mbeya leo Oktoba 3, 2023. Picha na Hawa Mathias
Mbeya. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuagiza Wakala wa Barabara (Tanroads) makao makuu kuanza kuchunguza vitengo vya manunuzi nchi nzima baada ya kubaini miradi mingi kusuasua kufuatia tenda kupewa wakandarasi wasio na sifa.
Bashungwa ametoa agizo hilo leo, Jumanne Oktoba 3, 2023 baada ya kukagua miundombinu ya barabara ya njia nne yenye urefu wa kilometa 29 utakaogharimu zaidi ya Sh 137 bilioni kutoka Nsalaga mpaka Ifisi unaotekelezwa na Kampuni ya China Henan International Company Limited (CHICO) na kusimamiwa na Tanroad .
“Tumebaini kuwepo kwa miradi mingi kusuasua hususan barabara ya Ibanda -Kajunjumele yenye urefu wa kilometa 22 ambayo kandarasi wa Kampuni ya AVM-Dilligham Construction International Inco amesaini mkataba tangu Machi 30 mwaka huu mpaka sasa hajakamilisha vifaa kuleta vifaa kwa ajili ya kuanza mradi ”amesema
Amesema Serikali haitoweza kuvumilia watu wachache kukwamisha miradi na kusisitiza kufanyeke ufuatiliaji wa haraka na hatua zichukuliwe kwa wahusika ,huku akipongeza Kampuni ya Chiko ambayo imekamilisha vifaa na kuanza utekelezaji wa mradi huo ambao utakamilika ndani ya miezi 24.
“Kwanza nimshukuru Rais kwa kuleta mradi huu ambao utakuwa mwarobaini wa kuondokana na adha ya foleni katika barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam) ambayo imekuwa ni changamoto kubwa na kuchelewesha shughuli za kiuchumi,”amesema.
“Ujio wa miradi mingi katika Mkoa wa Mbeya ,Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya, Dk Tulia Ackson amekuwa mstari wa mbele kufuatia na kuishawishi Serikali ikiwepo mradi huu wa kimkakati wa barabara njia nne,”amesema.
Mkurugenzi wa miradi wa Tanroads ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Boniface Mkumbo amesema tayari asilimia 98 ya vifaa vya kutelekeza mradi vimefika na wana uhakika utakamilika kwa wakati na kuwa mwarobaini na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Amesema mradi huo wa barabara njia nne yenye urefu wa kilometa 29 kuanzia Nsalaga mpaka Ifisi Wilaya ya Mbeya utatekelezwa na kampuni ya Chico kwa muda wa miezi 24 wenye thamani ya zaidi ya Sh 137 bilioni .
“Mkandarasi yuko eneo la mradi tunatarajia kazi hii itafanyika kwa wakati na itakuwa mwarobaini wa kupunguza msongamano wa magari na kuchochea shughuli za kiuchumi huku ikielezwa zaidi ya magari 1,000 yatapita kwa siku.
Mkazi wa Mbalizi, Stella Mwaisaka amesema uwepo wa mradi wa barabara njia nne utafungua fursa za kiuchumi kwa wakulima kusafirisha mazao kwenda nchi mbalimbali hususan Zambia na Congo.