Bashungwa akerwa na kasi ndogo uwanja wa Msalato

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akisikiliza maelezo ya mradi wa uwanja wa Ndege wa msalato Jijini Dodoma.
Muktasari:
- Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua miradi ya ujenzi ya barabara ya mzunguko (ring road) na Uwanja wa Ndege Msalato kwa awamu ya kwanza ambao ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi jengo la kuongozea ndege na jengo la abiria.
Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtaka mhandisi anayesimamia mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato aliyeenda mafunzo kurudi mara moja kusimamia mradi huo ambao ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake.
Bashungwa amesema mradi huo wa sehemu ya pili katika awamu ya kwanza unaohusisha ujenzi wa barabara ya kutua, kupaa, jengo la kuongezea ndege na abiria upo nyuma ya muda.
Bashungwa ameeleza hayo leo Septemba 29, 2023 wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato na barabara ya mzunguko (Ring road) jijini Dodoma.
“Sijaridhishwa na ujenzi kwa sababu mkandarasi yupo nyuma ya muda na nimemwambia asivimbe kichwa kwa sababu tumempa kazi nyingi maana hapa, uwanja wa Mtwara, Mwanza, Tabora, Sumbawanga amejenga yeye.
Sasa asipozingatia maelekezo ambayo nimempatia kwenye mkataba vipo vipengele vinavyoweza kusimamisha mradi kwa mujibu wa sheria na akizembea kwenye mradi huu hapati kazi zijazo kwenye nchi hii,”amesema Bashungwa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohammed Besta amemhakikishia Waziri Bashungwa kuwa atamsimamia mkandarasi huyo kufanya kazi ili kufidia muda uliopotea.
Pia, Bashungwa amemtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi wa mradi huo ambaye alielezwa kuwa mafunzoni kwa muda wa wiki mbili, kurudi kuendelea kusimamia mradi huo baada ya ziara yake kukamilika.
Kwa upande wa mradi wa barabara ya mzunguko Bashungwa amesema mradi huo unaendelea vizuri na kuahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi kuhusu kuombwa rushwa ili wapate ajira kwenye mradi huo.