Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuoanisha mitaala ya ualimu stashada na shahada

Muktasari:

  • Wadau wamepongeza uamuzi wa Serikali wa kuaonisha mitaala ya ualimu katika ngazi ya stashahada na shahada kwa kile walichoeleza kuwa uamuzi huo umechelewa

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza kuoanisha mitaala ya ufundishaji walimu katika ngazi ya stashahada na shahada ili kupata walimu bora, wadau wamesema ni jambo lililochelewa na litaondoa mgogoro wa muda mrefu.

 Hiyo ni kutokana na kile kilichoelezwa na wadau kuwa, walimu wenye stashahada walikuwa na soko katika ajira kuliko wenye shahada kutokana na kile kilichoelezwa kuwa waliandaliwa vyema na kupewa mbinu za ufundishaji kuliko wenye shahada waliokuwa wakisoma nadharia zaidi.

Akizungumza leo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk Caroline Nombo alisema maelekezo ya sera ambayo itatangazwa hivi karibuni kunahitajika kuwapo kwa uoanisho wa namna ya kutoa mafunzo ya ualimu kwa kile kinachofanyika katika ngazi ya stashahada na shahada.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuzalisha walimu wenye vigezo na umahiri unaotakiwa kwa ngazi mbalimbali.

“Tunaimani tutaondoa kuambiwa mwalimu huyu ni bora kuliko huyu, lengo la serikali kupitia wizara ni kuhakikisha tunazalisha walimu bora, tunatamani walimu hawa wapewe elimu itakayofanya wasimame kama walimu bora kwa kuzingatia mafunzo stahiki waliyopewa iwe ni vyuo vya kati au vikuu,” amesema Dk Nombo.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika kikao cha wadau wa elimu ya ualimu ambacho kilienda sambamba na kufanya mapitio ya utekelezaji wa mradi wa kuendeleza elimu ya Ualimu (TESP) unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Canada unaogharimu Dola 53 milioni za Canada.

Dk Nombo alitumia nafasi hiyo kuwataka wadau wa mkutano kutoa maoni juu ya namna gani uoanishaji huo unaweza kufanyika kwa ajili ya kuzalisja walimu bora.

Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa walimu bora ndiyo kitovu cha maarifa kwa kile alichokieleza kuwa wasipoandaliwa vizuri ni kuandaa Taifa ambalo watu wake hawajaelimika.

Amesema lengo la kupitia mitaala ya elimu na sera ya elimu ilikuwa ni kubadili namna elimu ya Tanzania inavyotolewa ili kuzalisha wataalamu wanaoweza kufanya uzalishaji.

“Hivyo elimu inayokwenda kutolewa sasa kupitia mitaala yetu mipya ni ile ambayo itatuwezesha kuzalisha wahitimu walio na umahiri na ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira bila kujali ngazi yake ya elimu,” amesema Dk Nombo.

Akizungumzia uoanishaji mitaala, mdau wa elimu, Dk Avemaria Semakafu amesema uamuzi huo ulochelewa utakwenda kutatua mgogoro uliokuwapo hasa katika uajiri.

Hiyo ni kutokana na kile alichosema, wamiliki wa vyuo vya ualimu vya binafsi walikuwa walikuwa hawataki walimu waliosoma shahada kwa kile walichokieleza kuwa kuwaajiri wao ni sawa na kuleta mwanafunzi mwingine anayehitaji kujifunza.

“Tatizo si mishahara, wanafundishwa masomo lakini hawapewi mbinu za ufundishaji hivyo waliona bora kuajiri mwalimu mwenye astashahada au stashahada. Hivyo jambo hili ni zuri na linahitaji kutekelezwa,” amesema Dk Semakafu.

Maneno yake yanaungwa mkono na mdau wa elimu Nicodemus Shauri ambaye anaeleza kuwa kitendo hicho kitaondoa dhana ya kuwa walimu wa shahada hawana umahiri sawa na wale wa ngazi za chini yao.

“Hii hasa katika mbinu za ufundishaji, stashahada wanafundishwa mbinu na kuandaliwa tofauti na shahada ambao wanawekewa mkazo katika nadharia na ujuzi (Compitence),” amesema Shauri.

Amesema uamuzi huo ni utekelezaji wa maoni ya wadau ya muda mrefu ambao walikuwa wakitaka kufanyika kwa maboresho ya ufundishaji walimu.

Awali, Kansela mkuu, ushirikiano na Maendeleo kutoka Serikali ya Canada, Helen Fytche amesema Canada inafurahi kuwa mmoja wa washiriki katika kuboresha mfumo wa elimu ya walimu Tanzania ili kuwanufaisha walimu wa sasa na baadaye.

“Tunaamini kwa kushirikiana na wizara tutasaidia kuifanya elimu ya ualimu na elimu kwa ujumla kama mojawapo ya maeneo ya vipaumbele,” amesema Helen.

Kupitia utekelezaji wa mradi wa TESP, chuo kipya cha mfano cha ualimu Kabanga kimejengwa huku maabara za sayansi katika vyuo vya ualimu Korogwe, Butimba, Tukuyu, Patandi, Mpwapwa, Morogoro, Dakawa na Kasulu zikijengwa.