Serikali kuanzisha mfuko wa nishati safi kupikia

Rais Samia Suluhu Hassan akiwasikiliza wadau mbalimbali kwenye mabanda ya maonesho kuhusu matumizi ya Nishati safi ya kupikia kabla ya kufungua Kongamano la Kitaifa kuhusu Nishati ililofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam Novemba 1, 2022.
Muktasari:
- Serikali imejipanga kuanzisha Mfuko wa nishati safi ya kupikia, ambao itautengea fedha kuanzia bajeti ya mwaka 2023/2024.
Dar es Salaam. Serikali imejipanga kutenga fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa mfuko maalum kwa ajili nishati safi ya kupikia.
Fedha hizo zitaanza kutengwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha lengo likiwa kumtua mama mzigo wa kuni kichwani.
Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza uamuzi huo leo wakati wa kongamano la kitaifa la nishati safi ya kupikia linalofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema kama ambavyo aliweka lengo la kumtua mama ndoo kichwani ndivyo ambavyo nguvu itawekwa kwenye kumtua mama kuni kichwani kwa kumpa nishati safi ya kupikia.
Bila ya kutaja kiasi gani kitakachowekwa Rais Samia amesema hatua hiyo ya kuanzisha mfuko itasaidia kuwavutia wadau wa maendeleo kuona haja ya kutunisha mfuko huo.
Amesema, “Nikiwa Makamu wa Rais niliweka lengo la kumtua mama ndoo kichwani nina furaha kusema kwamba nimetimiza kwa asilimia 80, ukiacha hizi athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, ukame unaotuandama, upatikanaji wa maji umeshuka.
“Nitajisikia fahari ikifika 2032 Tanzania hii iwe na nishati ya kupikia kwa asilimia hizo hizo 80, 90 kama sio zote,” amesema Rais Samia.