Matumizi ya mkaa Dar yahatarisha misitu mikoani

Muktasari:
- Dar es Salaam ndiyo mtumiaji mkubwa wa mkaa wote unaozalishwa nchini na sehemu kubwa ya mikoa inayozalisha mkaa huo ndiyo yenye mito inayotakiwa kutiririsha maji kuelekea katika mkoa huo.
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, asilimia 50 ya mkaa wote unaozalishwa nchini unatumika katika jiji la Dar es Salaam na uzalishaji huo wa mkaa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Tanga na Lindi
Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba Mosi 2022 na mtalaam mwandamizi wa masuala ya fedha Shirika la Umoja wa Mataifa Mitaji ya Maendeleo, Emmanuel Muro wakati wa kongamano la nishati safi ya kupikia linalofanyika leo na kesho jijini Dar es Salaam .
Akichangia mada wakati wa mdahalo ulioongozwa na Waziri wa Nishati Januari Makamba, Muro amesema mikoa ambayo ndiyo wazalishaji wakubwa wa mkaa ndiyo chanzo cha maji yanayotiririka kwenye mito.
“Mikoa hiyo ndiyo chanzo cha maji na mito inayotiririka Dar es Salaam, ndiyo chanzo cha uhai wa jiji hili kwahiyo ni lazima tuwe wazi sio suala la kutafuta huruma au kukipendeza.
“Tusipochukua hatua sasa kukabiliana na hali hii tutafika mahali pabaya. Dar inaweza kuonekana ndogo kijiografia ila ina watu wengi na ndiyo hao watumiaji wa mkaa,” amesema Muro.
Kwa upande wake daktari Pauline Chale amesema magonjwa yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi yanagharimu fedha nyingi ambazo watanzania wengi inawawia vigumu kumudu.
“Kuna mgonjwa tulikuwa tunamhudumia kwa miaka sita, alikuwa anakuja kliniki kila mwezi anachukua dawa ya Sh100,000 mwezi ulipota alishindwa kabisa kupumua ikabidi tumlaze pale hospitali kitengo cha ICU ambayo gharama yake kwa siku Sh500,000 alikaa pale kwa siku 12.
“Huyu mama hali yake ilizidi kuwa mbaya mapafu yake yakashindwa kabisa kufanya kazi akafariki dunia, hii yote ni matokeo ya matumizi ya nishati isiyo safi katika kupikia,”amesema Dk Paulina.