Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matarajio ya wadau mjadala nishati safi

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza katika mahojiano maalumu na wahariri wa Mwananchi hivi karibuni.

Muktasari:

Wakati mjadala kuhusu nishati safi ya kupikia ukitarajiwa kufanyika kesho, wadau wameeleza matarajio yao, wakitaka kuona mbinu mbadala zitakazoandaliwa kurahisisha ufikiwaji wa nishati hiyo kwa wananchi wa hali ya chini.

Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu nishati safi ya kupikia ukitarajiwa kufanyika kesho, wadau wameeleza matarajio yao, wakitaka kuona mbinu mbadala zitakazoandaliwa kurahisisha ufikiwaji wa nishati hiyo kwa wananchi wa hali ya chini.

Pia, unafuu wa bei ya nishati hiyo na upatikanaji wa uhakika kutokana na ukuaji wa teknolojia ni eneo lingine ambalo wadau hao wamebainisha kuwa ni muhimu kutazamwa na kutafutiwa ufumbuzi.

Mjadala huo unakuja, wakati ambao tayari matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kupikia yametajwa kuendelea kugharimu maisha ya Watanzania na kuzalisha kundi kubwa la wagonjwa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Oktoba 31, 2022, Waziri wa Nishati, January Makamba amesema mwamko wa washiriki ni mkubwa na kwamba, baada ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi kutangazwa leo jijini Dodoma, kupitia kongamano hilo Tanzania inaweza kuibuka na mwelekeo mpya katika matumizi ya nishati.

Kwa mujibu wa Makamba ni kwamba, Rais Samia Suluhu Hassan ataongoza mjadala huo kesho na kutoa mwelekeo mpya kuhusu matumizi ya nishati safi kabla ya kuanza ziara yake nchini China.

Amesema kuwa wamelazimika kuandaa mjadala huo wa kitaifa ambao baadaye utakwenda hadi ngazi za chini ili kuzuia madhara kwa watanzania kwani, watu 33,000 ambao hupoteza maisha kila mwaka ni wengi na lazima Serikali ichukue hatua madhubuti kuwalinda.

Hata hivyo, asilimia 80 ya nishati iliyopo nchini, hutumika kwa ajili ya kupikia, huku wastani wa asilimia 5.7 pekee ndiyo Watanzania wenye uwezo wa kutumia nishati safi kwenye mapishi.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi leo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Climate Action Network Tanzania, Dk Sixbert Mwanga amesema kwenye mjadala huo anatarajia kusikia mbinu mbadala zilizoandaliwa ili kurahisisha ufikiwaji wa nishati safi.

“Kama tunataka tutumie gesi kwanza tujue wangapi wanayo au wanaweza kuipata kwa maana imesambaa kiasi gani,” alisema.

Amesema mjadala huo utabadili mtazamo wa jamii kuhusu urahisi wa bei ya nishati safi, tofauti na inavyodhaniwa sasa kuwa ni ghali.

Kurahisishwa kwa bei ya nishati safi ya kupikia ni jambo lingine alilosema anatarajia lijadiliwe, ili kila Mtanzania mwenye kila hali aweze kumudu gharama zake.

“Mkaa unachaguliwa kwa sababu unakula hela kidogo kidogo, natarajia mjadala wetu ujikite katika namna ya kuifanya nishati safi ipatikane hata kwa mtu mwenye kipato kidogo,” amesema.

Ameeleza anatarajia mjadala utatanzua mkanganyiko wa matumizi ya nishati unaosababishwa na utofauti wa vipaumbele baina ya wizara moja na nyingine.

Utashi wa kisiasa, amesema ni jambo muhimu katika kufanikisha hicho kinachojadiliwa, akifafanua katika bajeti ziwekwe fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuihusisha sekta binafsi ni jambo lingine litakalofanikisha kufikia matarajio ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Hata hivyo, amesema mjadala huo ni muhimu ingawa amedai umechelewa, akifafanua: “Ni mjadala ambao ulipaswa kufanywa miaka 50 iliyopita tumechelewa, lakini kheri kuchelewa kuliko kuacha.

Mtaalamu wa Miradi katika Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa eneo la nishati, mabadiliko ya tabianchi na majanga (UNDP), Abbas Kitogo amesema mjadala huo unapaswa kutoka na mkakati wa utekelezaji wa kitakachojadiliwa.

“Mara nyingi kumekuwa na mijadala na mikutano mbalimbali lakini changamoto ni namna ya kutekeleza kinachojadiliwa, nafikiri ni vema kuunda mikakati inayotelekezeka na kutekeleza,” amesema.

Kitogo amebainisha jambo muhimu kuzingatiwa ni kuangalia upatikanaji wa teknolojia zitakazofanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tujue teknolojia zipi zinapatikana wapi, zinanunulika vipi na ubora wake,” amesema.

Athari na fursa za kiuchumi

Matumizi ya nishati chafu hayaishii kuathiri afya, bali hata uchumi wa nchi kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Verdiana Tilumanywa.

Dk Verdiana amesema afya ndiyo mtaji mkubwa katika uchumi, kwa kuwa jamii inahitajika kuwa imara ili kuzalisha vema, hivyo kitakachojadiliwa kinalenga kuokoa maisha ya watu, lakini uchumi pia.

“Kama watu wengi wanakufa kutokana na athari za matumizi ya nishati chafu maana yake nguvu kazi ya kuzalisha inapungua, sekta nyingi zitakosa watu wa kufanya kazi ikiwemo kilimo, biashara uvuvi vyote vinaathirika,” amesema.

Madhara makubwa kiafya

Wataalamu wa afya wamesema nishati ya kupikia ya kuni na mkaa hutoa kemikali sumu nyingi zinazoathiri afya na kusababisha vifo, huku wanaopikia nishati hizo wakiwa ndani (eneo lililofunikwa) wakipata madhara makubwa zaidi.

Wataalamu hao wameeleza kuwa vifo vitokanavyo nishati zisizo safi nchini vinafikia watu 30,000 mpaka 45,000 kwa mwaka huku watu milioni 38.8 wanaishi wanaumwa magonjwa hayo ambayo yapo katika mfumo tofauti.

Mtaalamu wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji ambaye pia ni mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema moshi unaosababishwa na kuni na mkaa huzalisha kemikali ya monoksidi ya kaboni ‘carbon monoxide’ ambayo pia hupatikana kwenye mkaa ambayo mtu akiipata kwa wingi ni sumu inayoweza kusababisha kuondoka kwa oksijeni kwenye seli mwilini na ikashaondoka monoksidi ya kaboni huchukua nafasi ya oksijeni mwilini,

“Kwa mfano umefungiwa sehemu kuna jiko la mkaa unawaka unatoa moshi ingawa wengi hatuuoni ule moshi unazunguka na kuleta hilo tatizo kuna matukio ya watu wengi kufa,” amesisitiza.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Alex Masao amesema: “Mbaya kuliko yote kemikali hii inaharibu mapafu moja kwa moja na unaweza kuchukua muda mrefu kuugua, wale wanaotumia kuni kwa muda mfupi wanaweza wasipate madhara.”

Dk Masao amesema kitu kinacholeta athari zaidi kwa mtu anayepikia kuni moshi unaotoka una mchanganyiko wa kemikali tofauti nyingi hivyo wapo hatarini kuliko mkaa.

Kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2022/2023 iliyosomwa na Waziri Ummy Mwalimu ilieleza ongezeko la magonjwa ya mfumo wa upumuaji na kwamba ni miongoni mwa magonjwa yaliyoongoza kuathiri Watanzania wengi hasa waliofika kwa matibabu hospitalini.

Takwimu za ulimwengu

Kulingana na Wakala wa Nishati duniani (IEA), watu 2.5 bilioni wanatumia nishati za kuni, mkaa na mafuta ya taa kupikia.

Hatua hiyo husababisa vifo vya watu takriban 2.5 bilioni kila mwaka. Takwimu hizo zinabainisha, katika Bara la Asia ni watu 1.5 bilioni wanashindwa kuifikia nishati safi ya kupikia, huku nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni watu 940 milioni.