Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia kutoa muelekeo wa Serikali nishati safi ya kupikia

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza katika mahojiano maalumu na wahariri wa Mwananchi leo Oktoba 25, 2022.

Muktasari:

Katika kukabiliana na athari za matumizi ya nishati chafu ya kupikia, Serikali imeandaa mjadala wa kitaifa kujadili matumizi sahihi ya wa nishati safi ya kupikia utakaofanyika Novemba 1-2, 2022.

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na athari za matumizi ya nishati chafu ya kupikia na utunzaji wa mazingira, Serikali imepanga kufanya mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia ambao utahusisha wadau wa sekta mbalimbali.
Mbali na wadau wa ndani na viongozi wa Serikali, pia taasisi za kimataifa, mabalozi wanatarajiwa kushiriki kwenye mjadala huo.
Mjadala huo utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) na mgeni rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassa, ambaye anatarajiwa kutoa mwelekeo mpya kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Hatua hiyo inalenga kuwaokoa maelefu ya Watanzania ambao wamekuwa wakiathirika kutokana na kutumia nishati inayotokana na kuni, mkaa na mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama.
Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 30,000 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na kutumia nishati ya kuni na mkaa ambayo, kiafya sio salama lakini kutokana na changamoto mbalimbali imewalazimu kutumia.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na timu ya wahariri wa Mwananchi, leo Oktoba 25, 2022 Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Rais Samia atakuwepo kutoa muelekeo wa Serikali yake kuhusu nishati safi ya kupikia.
“Tunaamini siku hiyo atatoa (Rais Samia) maelekezo mahususi ya kurahisisha uratibu, sio suala jepesi ni gumu na sisi hatuamini kwamba majawabu yake yatapatikana kwa siku moja,” amesema.
Katika mahojiano hayo, Makamba ameeleza mjadala huo utahusisha majopo yatakayojadili maeneo mbalimbali ikiwemo haki za wanawake katika nishati ya kupikia na maboresho ya kisera kurahisisha utekelezaji wa kampeni hiyo.
Maeneo mengine yatakayojadiliwa, amesema ni vivutio ili kushawishi jamii kutumia nishati hiyo, ambayo pamoja na mambo mengine kanuni za kikodi pia zitajadiliwa ili kurahisisha upatikanaji wa nishati safi.
Amesema mjadala huo utahitimishwa kwa mapendekezo ya utekelezaji wa kampeni ya nishati safi ya kupikia, amebainisha unatarajiwa kutoa muda wa utekelezwaji wa kampeni hiyo.
Makamba amesema katika mjadala huo wahudhuriaji watashuhudia namna wanawake hasa wa vijijini wanavyoteseka na matumizi ya nishati chafu ya kupikia ikiwemo mkaa, kuni, mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama.
“Hatuhitaji kubadilisha sera ya nishati, tunachohitaji ni kuoanisha kati ya maelekezo yetu sisi (Wizara ya Nishati) na vipaumbele vya wizara nyingine, kwa mfano Wizara ya Mazingira wanazuia kukata miti, ukienda Maliasili na Utalii moja ya malengo yao ni kuongeza mapato na wanayatokana na mazao ya misitu ikiwemo mkaa, kuni.
“Kwa hiyo kikubwa ni kuoanisha ili malengo yetu yote kwa pamoja yawe yanashabihiana kwa maslahi mapana ya Watanzania. Hii suala la nishati safi ya kupikia halizungumzwi sana kwa sababu wengine hawajui hata vyakula vinapikwa vipi, lakini ni eneo nyeti sana. Sisi tuliokulia vijijini tunafahamu hili, na ndio sababu tumeona tatizo hivyo, tunataka kulijadili kwa kina na kupata mwelekeo wa pamoja,” amesema Makamba.