Serikali kuanzisha bodi ya ithibati kwa wanahabari

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kushoto) akizungumza bungeni huku wanahabari wakimpiga picha alipokuwa akiwasili makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
- Bodi hiyo itakuwa na jukumu la la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.
Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo Innocent Bashungwa amesema kwa sasa wizara yake inaendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati itayokuwa na jukumu la la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.
Bashungwa ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 31 2021 wakati akiwasilisha makadiro ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Amesema Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, inaelekeza kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Habari pamoja na mfuko wa mafunzo kwa wanahabari.
“Kwa sasa wizara inaendelea na taratibu za kuanzisha bodi hii,”amesema.
Aidha, amesema Baraza Huru la Habari litaundwa baada ya Bodi ya Ithibati kuanza kazi, kwa kuwa baraza hili litaundwa na wanahabari wenyewe watakaokuwa wamepewa ithibati.