Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekta binafsi kuokoa jahazi kero Mwendokasi

Abiria wakigombania kupanda katika basi la mwendokasi. Picha na mtandao

Dar es Salaam. Serikali imetoa miezi saba kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kuhakikisha inapatikana kampuni binafsi itakayotoa huduma ya usafiri jijini hapa.

Iwapo hilo halitatekelezwa hadi Oktoba mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amewataka mabosi wa Dart, Dk Athuman Kihamia na wa kampuni ya Uendeshaji Usafiri wa Haraka (Udart), Waziri Kindamba kuwasilisha kwake barua za kujiuzulu.

Kauli hiyo ya Mchengerwa inatokana changamoto zilizopo katika utoaji huduma za usafiri jijini Dar es Salaa, hivyo kuwepo muhimu kuishirikisha sekta binafsi kama ilivyokuwa imepangwa.

Mchengerwa alitoa maelekezo hayo wakati akiwasilisha randama ya Bajeti ya (Tamisemi na Fungu namba 2 la Tume ya Utumishi wa Walimu mbele ya Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa bungeni jijini Dodoma.

Alipotafutwa kuzungumzia agizo hilo, Dk Kihamia hakupatikana, lakini Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Dart, Dk Philemon Mzee aliyepatikana alisema “kinachofanyika ni utekelezaji”.

"Serikali ikisema ni agizo hilo, kinachofuata ni utekelezaji na hivyo tutatekeleza, lakini mengine mkurugenzi mkuu (Dk Kihamia), ndiye aliye katika nafasi nzuri ya kuyazungumzia," alisema DK Mzee.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Waziri Kindamba alisema ni mapema kusema chochote kwa kuwa bado anajifunza mengi kuhusu ofisi hiyo.

“Hapa mezani kwangu kumejaa nyaraka nasoma ili nielewe kuhusu Ofisi hii kwa hiyo naomba mnipe muda kisha tutapata nafasi ya kuzungumza,” alisema Kindamba.


Danadana mwekezaji mpya

Mchengerwa si kiongozi wa kwanza kuagiza apatikane mwekezaji mwingine na suala hilo limekuwa mithiri ya danadana.

Awali, kampuni iliyopewa fursa ya kutoa huduma katika mradi huo ni Simon Group, iliyokuwa na takriban mabasi 100.

Utoaji huduma wa kampuni hiyo, ulitajwa kuwa wa majaribio wakati mtoa huduma rasmi anaendela kutafutwa, ili angalau anunue mabasi 150.

Mchakato wa kumsaka mtoa huduma zilianza mwaka 2018 na Serikali ilitangaza kupatikana kwake, lakini haijulikani aliishia wapi.

Baadaye mwaka 2019 Serikali ilitangaza kumsaka mtoa huduma mpya atakayekuwa na uwezo wa kununua mabasi 170, yaliyotarajiwa kutosheleza huduma kwa wakati huo, lakini hadi mwaka 2021 hakuna mtoa huduma aliyepatikana.

Mwaka 2022 Serikali ilipotangaza kupatikana kwa mwekezaji mpya ambaye ni kampuni ya Emirates National Group.

Kampuni hiyo kutoka Falme za Kiarabu ilitajwa ingenunua mabasi 750, yatakayosafirisha abiria kati ya 600,000 hadi 700,000 kwa siku. Hata hivyo, nayo ‘iliyeyuka’.

Katika kipindi hicho mradi wa mabasi yaendayo haraka, umekuwa ukilalamikiwa kwa huduma mbovu na zinazokinzana na matarajio ya wananchi.

Miongoni mwa malalamiko ni mrundikano wa abiria vituoni bila kupata huduma huku baadhi ya mabasi yakipita vituoni bila kuwa na abiria.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa mzizi wa changamoto ni uchache wa mabasi na mengine zaidi ya nusu kuwa mabovu.

Wakati njia ya Kimara- Gerezani-Kivukoni - Morocco ikikabiliwa na uchache wa mabasi, ile ya Gerezani - Mbagala ilikuwa imekamilika lakini haina mabasi ya kutoa huduma.

Njia zingine zinazoendelea kutengenezwa katika awamu ya tatu ni ya Gerezani-Gongolamboto –Magomeni- Chang’ombe.

Pia, ujenzi wa barabara maalaum za zege zenye urefu wa kilometa 33.5, za Morocco – Kawe) kilomita 7.8, upanuzi wa BRT1 (Kimara – Kibaha) kilomita 20.7 na upanuzi wa BRT 2 (Mbagala rangi tatu – Vikindu) kilomita 5.0 nazo ziko mbioni.


Kauli ya Mchengerwa

Waziri Mchengerwa katika tamko lake alisema iwapo mradi huo utaboreshwa vizuri asilimia 80 ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam lenye watu zaidi ya milioni 5.3 watatumia usafiri wa mwendokasi.

"Wala hakuna mjadala, ikifika Oktoba wakishindwa kuhakikisha kwamba watu wa Dar es Salaam wanahudumiwa vizuri, walete barua za kujiuzulu.

"Kwa sababu hatuwezi kwenda kama kawaida, watu wanataka huduma hazitolewi, watu wanatoa huduma wanavyotaka wao, mtu anaweza akaamua tu kusimamisha basi,” alisema.

Iwapo itashirikishwa sekta binafsi, alisema haitawezekana huduma kudorora.

"Wakati mwingine unaona basi linakatiza haliwachukui hata wananchi kwa sababu tu alitengewa kwamba muda fulani awe sehemu fulani, wanashindwa hata kujiongeza,” alisema Mchengerwa mbele ya kamati hiyo.

Waziri huyo aliweka bayana kwamba “watu hawahudumiwi vizuri, watu wana wagonjwa, kulikuwa na wananchi hadi wanapigwa makofi ukilalamika ndani ya gari, kulikuwa na vitu vingine ukiangalia hata havileti afya kwa Serikali yetu.”

Waziri huyo alisema kulikuwa na uhitaji wa mabasi 170, wamekwisha kufanya uamuzi kwani awali walipelekewa bei ya basi moja karibu dola za Marekani 500,000, sawa na Sh1.27 bilioni.

“Haiwezekani ununue basi moja kwa dola laki tano, wananchi wangetuelewa vipi? Mimi nikasema hapana, hili jambo haliwezekani unanunua behewa la treini? Na ndio sababu tumechelewa kidogo,” alisema.

Mchengerwa alisema wameweka utaratibu wa kuhakikisha wanatumia sekta binafsi, “na Serikali tuiachie sekta binafsi kuendesha huu mradi. Wakati tunafikiria kuleta huduma hii Dodoma na majiji yote, lazima tuboreshe kwanza Dar es Salaam.”

Mbali na hayo, Mchengerwa alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha njia zote za mradi huo jijini Dar es Salaam zinakuwa na mabasi ya kutosha na huduma zinakwenda kama zilivyopangwa.

Hata hivyo, Mchengerwa alieleza matumaini yake juu ya uongozi mpya wa Dk Kihamia na Mkurugenzi wa Udart, Waziri Kindamba walioteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu mradi huo.

“Wapo waliopewa mamlaka ya kusimamia eneo hii hawasimamii vizuri, lakini tunampongeza Rais Samia kwa mabadiliko aliyoyafanya kwa majembe aliyotuletea kwa kweli ni wachapa kazi, naamini kwa rekodi walizonazo watatusaidia,” alisema.

Januari 11 mwaka huu, Dk Kihamia aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) aliteuliwa kuwa mtendaji mkuu wa Dart akichukua nafasi ya Dk Edwin Mhende ambaye ilielezwa atapangiwa kazi nyingine.

Miezi miwili baadaye, Machi 10 Rais Samia alimteua Kindamba kuwa mkurugenzi mtendaji wa Udart kuchukua nafasi ya Gilliard Ngewe ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Kindamba aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga kabla ya uteuzi huo na amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), anakuwa Mkurugenzi wa nne ndani ya Dart tangu ilipoanzishwa. Aliyeanza ni Charles Newe, alifuatiwa na John Nguya kisha Ngewe na sasa Kindamba.

Mmbali na upungufu wa mabasi, changamoto nyingine za mradi huo ni kupotea kwa mapato kulikokithiri kutokana na mfumo wa ukatishaji tiketi kuwa na walakini.

Hata hivyo, hivi karibuni Dk Kihamia alizungumzia suala hilo akisema tayari kadi 200,000 zimeshanunuliwa tangu Februari mwaka huu, kwa ajili ya mfumo huo.

Sambamba na kadi hizo, Kihamia alisema kazi iliyobaki ni utengenezaji wa mageti janja, kazi ambayo inafanywa na mkandarasi kutoka Italia.

"Matarajio yetu ni mwezi huu Machi au mwanzoni mwa Aprili kazi hiyo itakamilika na mfumo wa kadi utaanza kutumika," alisema.