Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sauda jela miaka 30 kwa kusafiria kilo moja ya bangi

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa Mahakamani hapo Julai 17, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye shtaka moja la kusafirisha bangi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Sauda Mohamed (48) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo moja ya dawa za kulevya aina ya bangi.

Sauda mkazi wa Majohe, alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 1.02, tukio analodaiwa kulitenda Septemba 21, 2023 katika Bandari ya Dar es Salaam.

Hukumu hiyo, ilitolewa leo, Alhamisi Mei 8, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Lyamuya amesema upande wa mashtaka walipeleka mashahidi sita, ambao wamethibitisha shtaka bila kuacha shaka.

Akichambua baadhi ya ushahidi, ambao ulitolewa mahakamani hapo, alisema shahidi ambaye alikuwa anafanya kazi eneo la kukagua mizigo ya kwenda Zanzibar kwa kutumia mashine alitilia mashaka begi la abiria (Sauda).

Shahidi huyo, baada ya kuwa na shaka alifungua begi na kukuta majani na ndipo mshitakiwa alipelekwa Kituo cha Polisi kilichopo Bandari.

Shahidi mwingine alikuwa ni mkemia Mkuu wa Serikali, alipofanya uchunguzi wa dawa hizo alithibitisha kuwa ni bangi.

Mshitakiwa katika utetezi wake, alikana kuwa begi ambalo alikutwa nalo likiwa na bangi lilikuwa siyo lakwake kwani lake lilipotea akiwa bandarini hapo.

“Nimeridhika na ushahidi ulitolewa mahakamani hapo kwa mashahidi wa upande wa mashitaka na namna kielelezo cha bangi kilivyotunza kimefuata mtiririko unaotakiwa, hivyo wamethibitisha shtaka pasina kuacha shaka," amesema Hakimu Lyamuya.

Amesema mshitakiwa, alikana kuwa begi halikuwa la kwake lakini vielelezo ambavyo ni simu, vitambulisho na tiketi ya kusafiri kwenda Zanzibar, ambavyo vilikutwa ndani ya begi hilo, alikiri ni mali zake.

Hakimu Lyamuya, baada ya uchambuzi huo, alisema anamtia hatiani kama alivyoshitakiwa.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Frank Rimoy, ameomba mahakama kutoa adhabu kali iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia hizo.

Naye, mshitakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana mama yake ni mgonjwa kwa miaka nane hawezi kutembea na yeye anasumbiliwa miguu.

"Mheshimiwa hakimu, naomba mahakama yako inipunguzie adhabu, mimi nina matatizo ya miguu lakini pia mama yangu ana mwaka wa nane anaumwa hawezi kutembea," ameomba Sauda.

Hata hivyo, Hakimu Lyamuya, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, alitupilia mbali ombi la upande wa mshtakiwa na kukubaliana na ombi la upande wa mashtaka.

Hakimu Lyamuya amesema kwa jinsi shtaka lilivyo, sheria inakataza kutoa dawa eneo moja kwenda sehemu.

"Lakini pia, kwa kuzingatia kiasi ulichokutwa nacho ulikuwa na lengo la kuuza na adhabu yake ni kifungo cha miaka 30," amesema Hakimu Lyamuya na kuongeza.

"Hivyo, Mahakama inakuhukumu Sauda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii na haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo hujaridhika na adhabu hii," amesema hakimu Lyamuya.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa Mahakamani hapo Julai 17, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye shtaka moja la kusafirisha bangi.