Wawili mbaroni kwa wizi wa bajaji Njombe

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe.
Muktasari:
- Wanatembea na kamba maalumu kwa ajili ya kuwafunga watu wanaowateka na kuwanyang'anya bajaji.
Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia Juma Kimata (24) na Wetrack Ephraim Ngangalawa (32), wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako kwa tuhuma za wizi wa bajaji, ambao wanatumia nguvu katika kutekeleza wizi huo.
Hayo yamesemwa leo, Aprili 25, 2025, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.
Amesema sambamba na tukio hilo, watuhumiwa hao wamekamatwa na vifaa mbalimbali, ikiwemo spana za kufungulia magari, kadi ya pikipiki, leseni ya udereva pamoja na kamba ambayo ilikuwa inatumika katika utekaji.
"Sambamba na tukio hilo, tumefanikiwa kuwakamata na vifaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na spana ya kufungulia magari, kadi ya pikipiki, leseni ya udereva, rectifier mbili, coilplug na kamba kwa ajili ya wanapokuwa wamemteka mtu, wanamnyang'anya na kumfunga kamba," amesema Banga.
Amesema uchunguzi wa shauri hilo unaendelea na mara utakapokamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakama kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
Amesema jeshi hilo pia linamshikilia Ally Mtate (25), mkazi wa Chaugingi na Dickson Mgaya (31), ambaye ni fundi simu kwa tuhuma za kukutwa na pikipiki, mali inayodaiwa waliipora. Upelelezi utakapokamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.
Aidha, jeshi hilo linamshikilia Fikiri Ngolle (43), mkazi wa Kijiji cha Ngamanga huko Makambako, kwa kukutwa na miche 19 ya majani yanayodhaniwa kuwa ni bangi, aliyoyapanda sambamba na mahindi.
Amesema uchunguzi wa awali wa kupeleka sampuli kwa Mkemia wa Serikali ili kupata uthibitisho umefanyika na uchunguzi utakapokamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.
Amesema jeshi hilo linamshikilia Jackson Kitalula (20), mkazi wa Lupembe, akiwa na simu sita, saa ya mkononi, redio ndogo, mali anazodaiwa kuzipora katika matukio ya uvunjaji.
Amesema jeshi hilo lilimkamata Michael Mahenga (39), mkazi wa Kijiji cha Itona, Wilaya ya Mufindi kwa tuhuma za mauaji yaliyotokea maeneo ya Mufindi, na tayari amekabidhiwa mkoani Iringa kwa ajili ya hatua nyingine za mashtaka.
Kwa upande wa Kikosi cha Usalama Barabarani, jeshi hilo limetoa elimu kwa madereva, wamiliki wa vyombo vya moto na wananchi katika maeneo ya shuleni ili kuepuka ajali zinazozuilika.
"Jumla ya madereva waliokamatwa ni 3,792, walioandikiwa faini ni 3,787, waliopewa onyo ni watatu na waliopelekwa mahakamani ni mmoja, na aliyefungiwa leseni ni mmoja," amesema Banga.
Mwenyekiti wa Maofisa Usafirishaji Wilaya ya Njombe, Veremund Msigwa amesema vyombo vyao vya usafiri vina namba za utambulisho na endapo mteja atafanyiwa jambo lolote, ikiwemo kuibiwa, anatakiwa kutaja namba ya chombo kilichofanya uhalifu huo.
"Hili jambo kama lipo, sisi tutaendelea kulifanyia kazi. Mmoja tulishamkamata, jeshi la polisi linajua na tulitumia nguvu zetu kumkamata," amesema Msigwa.
Mmoja wa madereva wa bodaboda mkoani Njombe, Longinus Hongoli amesema bodaboda wanaposhiriki katika uporaji, jambo hilo linawaathiri katika suala zima la uaminifu kwa wateja wao kwa kuonekana wote tabia zao ni moja.
"Kama sisi tunaofanya kazi ya bodaboda inapelekea na sisi kukosa uaminifu; wateja wetu wanakuwa wanatufikiria vibaya. Labda nikimtuma huyu bodaboda akachukue nyama, anaweza akatokomea na hela yake," amesema Hongoli.