Mjomba, mpwa wake kortini wakidaiwa kusafirisha bangi

Muktasari:
- Kulwa na mpwa wake wanadaiwa kusafirisha gramu 512 za bangi, tukio wanalodaiwa kulitenda eneo la ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Kulwa Mathias ( 31) na mpwa wake, Edina Paul, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shitaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 512.50.
Mathias ambaye ni mkazi wa Salawe mkoani Shinyanga na Edina mkazi wa Urambo, mkoani Tabora wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano, Machi 5, 2025 na kusomewa kesi ya jinai ya mwaka 2025.
Akiwasomea shitaka hilo, wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi kuwa washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 11, 2024 eneo la ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, walikutwa wakifanya biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 521.50 kinyume cha sheria.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikuwa wanasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa kutuma usafiri wa maji na ndipo walipokutwa na dawa hizo.
Washtakiwa baada ya kusomewa shitaka lao, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo upo latika hatua za mwisho kukamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hata hivyo Hakimu Mushi aliwauliza washtakiwa iwapo wadhamini wao wamefika mahakamani hapo. Washtakiwa hao walidai kuwa hawana wadhamini. Hakimu Mushi ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 20, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kwa kukosa wadhamini.