Saratani ya utumbo chanzo cha kifo cha Jaji Kisanga
Muktasari:
Jaji Kisanga aliwahi kwenda nchini India kwa matibabu.
Dar es Salaam. Saratani ya utumbo ni chanzo cha kifo cha Jaji mstaafu Robert Kisanga, imeelezwa.
Msemaji wa familia, Dk Onesmo Kisanga amesema Jaji Kisanga alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo kwa miaka minne.
Akizungumza na MCL Digital leo Jumatano Januari 24,2018 nyumbani kwa marehemu Oysterbay, Mtaa wa Bongoyo, Dk Kisanga amesema jaji huyo aliwahi kwenda nchini India kwa matibabu mara mbili.
Amesema Jaji Kisanga alipatiwa dawa ambazo alikuwa akiendelea kuzitumia hadi alipofariki dunia jana jioni Jumanne Januari 23,2018.
"Kwa muda mrefu alikuwa anaumwa lakini wiki mbili zilizopita hali yake ilikuwa mbaya zaidi ndipo daktari wake alipoelekeza akalazwe hospitalini kwa uangalizi zaidi," amesema Dk Kisanga.
Amesema juzi Jumatatu Januari 22,2018 hali yake ilibadilika akawekwa chumba cha wagonjwa mahututi na jana saa 12:30 jioni alifariki dunia.
Kuhusu utaratibu wa mazishi, Dk Kisanga amesema, "Bado hatujapanga ndiyo kwanza naenda Mahakama Kuu. Jioni tutakuwa na kikao ndipo itafahamika mazishi yatakuwa lini ila ni kati ya Jumamosi na Jumatatu."