Samia mgeni rasmi mkutano mamalishe, babalishe
Muktasari:
- Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Aprili 11, 2026 katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), unatarajiwa kuwakutanisha wauza chakula kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili mustakabali wa biashara hiyo na nafasi yake katika uchumi wa taifa.
Dar es Salaam. Sekta ya wauza chakula maarufu kama mamalishe na babalishe inayolisha maelfu ya Watanzania kila siku, sasa inaelekeza macho yake katika mkutano mkubwa wa kitaifa utakaofanyika jijini Dar es Salaam, huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Aprili 11, 2026 katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), unatarajiwa kuwakutanisha wauza chakula kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili mustakabali wa biashara hiyo na nafasi yake katika uchumi wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumamsi, Aprili 4, 2026, Mwenyekiti wa Wauza Chakula (Mamalishe), Avijawa Omari amesema kupitia umoja wao wa Umoja wa Mamalishe na Babalishe Tanzania (Umalita), wanaiomba serikali kulitambua rasmi kundi hilo ili liweze kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Amesema utambuzi huo utafungua milango kwa wanachama kupata mikopo pamoja na programu za kuwawezesha kukuza biashara zao, hatua ambayo pia itachochea ajira kwa Watanzania wengine.
Kwa mujibu wa Avijawa, mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu kwa mamalishe na babalishe kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa viongozi wa serikali, huku wakijadili mbinu za kuongeza kipato na kupanua biashara zao.
“Tunawaalika wauza chakula wote kujitokeza kwa wingi Aprili 11 katika ukumbi wa Julius Nyerere ili kwa pamoja tujenge mustakabali wa biashara zetu,” amesema Avijawa.
Ameongeza mkutano huo utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Pika Kishua, Vaa Kishua,” inayolenga kuboresha viwango vya huduma na kuinua taswira ya kitaaluma ya wauza chakula nchini.
“Sisi ni wajasiriamali binafsi tunaolisha taifa asubuhi, mchana, jioni na usiku. Tunaomba jamii itambue mchango wetu na kuheshimu kazi yetu,” amesema.
Aidha, alibainisha kundi hilo limekuwa likikumbana na changamoto mbalimbali zikiwemo hatari za kiafya na mazingira magumu ya kazi.
Hata hivyo, amesema wanachama wengi sasa wanaanza kutumia nishati safi pamoja na mbinu bora za upishi ili kulinda afya zao na kuboresha huduma wanazotoa kwa wateja.
Kwa upande wake, mwakilishi wa babalishe, Ngosha amesisitiza umuhimu wa wanachama kuimarisha umoja na ushirikiano ili waweze kufikia malengo yao ya kiuchumi na kijamii.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa wa kihistoria kwa sekta ya wauza chakula, ukileta pamoja wadau wa sekta isiyo rasmi na viongozi wa serikali kujadili namna ya kuimarisha ajira na kukuza ujasiriamali nchini.