Samia: Hatujazuia kuuza mazao nje ya nchi

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Serikali haijafunga mipaka ya uuzaji wa mazao nje ya nchi, isipokuwa inataka iweke mfumo rasmi wa ununuzi, uuzaji na usafirishaji wa mazao ambao utaonyesha kiwango na thamani ya mazao hayo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Serikali haijafunga mipaka ya uuzaji wa mazao nje ya nchi, isipokuwa inataka iweke mfumo rasmi wa ununuzi, uuzaji na usafirishaji wa mazao ambao utaonyesha kiwango na thamani ya mazao hayo.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 8, 2023 katika kilele cha sikukuu ya wakulima Nanenane iliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale Mbeya, akianisha lengo la utaratibu huo kuwa kuwezesha Serikali kufahamu kiasi cha mazao kinachouzwa nje ya nchi, na fedha inayopatikana na hivyo kudhibiti wafanyabiashara wasiokuwa waamilinifu.
Ili kufanikisha hilo, Rais ameitaka Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Idara ya Uhamiaji, kuweka mfumo wa pamoja ili kusimamia bishara ya mazao nje ya nchi na hivyo kuwanufaisha wakulima kutokana kazi zao.
"Uzoefu uliopo sasa ni kwamba magari yanatoka tu nchi jirani yanaingia moja kwa moja kwenye mikoa yetu, kwenye wilaya zetu hayaulizwi, yanakwenda mpaka kwa wakulima kununua mazao na pale wanakwenda kulipa fedha zetu za ndani," amesema na kuongeza;
"Kuna mawakala wanagawiwa pesa mipakani huko, wanaingia kukusanya mazao yetu kwa fedha za ndani, hayo ni mazao tunayoweza kuyauza kwa fedha za nje."
Amesema ikiwa mfumo mzuri utawekwa wa ununuaji na kudhibiti magari kwenda moja kwa moja kwa wakulima, itaiwezesha nchi kujua inauzaje na inalipwaje.
Amesema jambo hilo lilimfanya yeye kumpa Waziri wa Kilimo fedha nyingi ili Wakala wa hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA), anunue mazao mengi kwa wakulima na kuweka stoo, jambo lililofanya wanunuzi wa toka nje, wanunue kwa bei ya soko.
"Hii ndiyo kauli niliyoitoa kule Mwanza kuwa sasa hivi wakulima wenyewe hakuna ruhusa ya kuuza mazao nje, kwa mtindo huo kwamba magari yanakwenda kule wanauza na magari yanaondoka bila kuwa na utaratibu wa kiserikali,” ameogeza kusema.
Kuhusu mazao ya bustani aambayo uzalishaji wake unaongezeka na kwamba yamekuwa na soko zuri nje ya nchi, Rais amesema, Serikali itaendelea na ujenzi wa vituo jumuishi viwili, huku kimoja kikijengwa Mufindi, mkoani Iringa na kingine kinajengwa Hai mkoni Kilimanjaro.
Vituo hivi vitahusika na ukusanyaji, uchambuaji, upangaji wa madaraja na ufungashaji mazao hayo na kwamba vitakuwa chini ya chini ya sekta binafsi kwa utaratibu wa Serikali.
Amesema hili ni moja ya eneo linalohitaji uwekezaji kutoka sekta binafsi hususani katika usafirishaji na uhifadhi baada ya mavuno.