Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia azima ndoto za wataka urais 2025

Samia azima ndoto za wataka urais 2025

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amezima ndoto za wanasiasa waliokuwa wakijiandaa kuwania urais mwaka 2025, badala yake amewataka waache mara moja mawazo hayo ili wachape kazi kwa maendeleo ya Taifa.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezima ndoto za wanasiasa waliokuwa wakijiandaa kuwania urais mwaka 2025, badala yake amewataka waache mara moja mawazo hayo ili wachape kazi kwa maendeleo ya Taifa.

Rais Samia aliyasema hayo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, baada ya kumwapisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga pamoja na mawaziri na manaibu waziri katika wizara zao mpya, baada ya kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Imekuwa ni ada ikifika kipindi cha pili cha Rais aliye madarakani, wanasiasa huanza harakati zinazolenga kuwania urais. Lakini jana Rais Samia aliwaonya mawaziri wake juu ya jambo hilo.

“Nafahamu 2025 iko karibu na kawaida yetu inapoingia kipindi cha pili cha Rais aliyepo, watu kidogo mnakuwa na hili na lile kuelekea mbele, nataka kuwaambia acheni!

“Twendeni tukafanye kazi, hili na lile tutajua mbele. Rekodi yako inakufuata katika maisha yako, kuna wengine wamekosa hizi nafasi kwa rekodi zao tu. Kwa hiyo rekodi yako inakufuata kwenye maisha yako,” alisema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi alisema hatafumba macho katika kusimamia suala hilo na kwamba kila mwenye nia ya kugombea urais, basi aache mara moja kabla hajakutana na jicho lake wakati akiangalia rekodi.

“Na mimi nitakuwa na jicho kubwa sana kuangalia rekodi zenu na safari ya mbele yetu. Lakini nataka kuwaambia kila mwenye nia ya 2025, aache mara moja,” alisisitiza Rais Samia.

Kifo cha Rais wa Tano, hayati John Magufuli, kimemfanya Samia ambaye alikuwa makamu wake, kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Rais Samia atamalizia miaka minne ambayo mtangulizi wake alikuwa amebakisha katika utawala wake.

Hata hivyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamruhusu kugombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2025 kwa kipindi kimoja cha mwisho.

Inaelezwa kuwa kifo hicho cha hayati Magufuli kimeharibu mipango ya wanasiasa ndani ya CCM ambao walikuwa wakijiandaa kugombea baada ya kiongozi huyo kumaliza awamu yake mwaka 2025. Huenda watalazimika kusubiri kwa miaka tisa hadi mwaka 2030 baada ya Rais Samia kumaliza muda wake.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Andrew Bomani alisema kifo cha hayati Magufuli kimeharibu mipango ya wanasiasa wengi ambao walikuwa na matumaini ya kurithi nafasi yake katika uchaguzi wa mwaka 2025. “Miaka tisa ni mingi sana kwa mtu mwenye umri wa miaka zaidi ya 60 sasa, ikifika mwaka 2030 atakuwa hana mvuto tena. Wengi katika umri huo hawataweza kuupata urais, ni ngumu sana,” alisema Bomani.