Samia atoa maagizo kwa uongozi halmashauri Mwanza

Muktasari:
- Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani ameuagiza uongozi wa halmashauri za Mkoa wa Mwanza kuongeza ukusanyaji wa mapato yakayowezesha uboreshaji wa miundombinu ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa masoko ya kisasa kufikia lengo la kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara ukanda wa Maziwa Makuu.
Mwanza. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani ameuagiza uongozi wa halmashauri za Mkoa wa Mwanza kuongeza ukusanyaji wa mapato yakayowezesha uboreshaji wa miundombinu ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa masoko ya kisasa kufikia lengo la kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara ukanda wa Maziwa Makuu.
Akizungumza na wananchi eneo la Buzuruga jijini Mwanza leo Jumatano Septemba 8, 2021 Rais Samia amesema mkoa huo una vyanzo vingi vya mapato ya ndani ambavyo vikikusanywa vema Serikali itafikia lengo la kuboresha miundombinu ya masoko, barabara na huduma zingine za kijamii.
“Mwanza ina mapato mengi, kama hayakusanywi ni uzembe nimewachagulia mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wazuri nimeelezwa mipango na mikakati yao na niko nyuma yao kuhakikisha yanafanikiwa,” amesema Rais Samia
Katika mkakati huo, Serikali imeahidi kutekeleza ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli ya kujenga kilometa 12.5 ya barabara za jiji hilo.
Rais pia amesema Serikali inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa maji kwa kujenga chanzo kipya eneo la Butimba kumaliza tatizo la maji jijini Mwanza na wilaya jirani za Magu na Misungwi.
Awali, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel alimweleza mkuu huyo wa nchi kuwa mkoa huo umepanga kujenga masoko mapya ya kisasa kama njia ya kumaliza tatizo la wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga wanaotandaza bidhaa zao kila eneo la wazi mitaani.