Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia ashangaa maadili ya vijana

Samia ashangaa maadili ya vijana

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ameshangazwa na mmomonyoko wa maadili kwa vijana wakati kuna Chama cha Skauti Tanzania, Umoja wa Vijana wa CCM na wale wa vyama vya upinzani wanaotakiwa kuwahimiza vijana wenzao kuzingatia maadili.

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ameshangazwa na mmomonyoko wa maadili kwa vijana wakati kuna Chama cha Skauti Tanzania, Umoja wa Vijana wa CCM na wale wa vyama vya upinzani wanaotakiwa kuwahimiza vijana wenzao kuzingatia maadili.

Rais, ambaye ni mlezi wa Chama cha Skauti nchini, aliyasema hayo juzi, wakati wa hafla ya Siku ya Mlezi wa Skauti Tanzania ambayo haijafanyika tangu mwaka 1995.

Si Rais Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete wala Dk John Magufuli ambao kwa nafasi zao walikuwa walezi wa skauti, hawakuwahi kuadhimisha Siku ya Mlezi wa Skauti Tanzania.

“Mfumo wa Skauti ni kama wa Serikali, imeenea nchi nzima. Kuna Skauti, Girl Guide (Chama cha Skauti wa Kike), Umoja wa Vijana wa CCM na umoja wa vijana kwenye vyama vingine vya siasa,” alisema Rais Samia katika hafla hiyo, iliyoenda sambamba na kuwatunuku nishani baadhi ya skauti na viongozi waliochangia shughuli za skauti.

Suala la mmomonyoko wa maadili limekuwa likishuhudiwa kutokana na tabia ya kuiga utamaduni wa magharibi.

Hata hivyo, Rais aliahidi kushirikiana na skauti kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwamo kuwafanya kuwa pamoja kati ya Skauti na Girl Guide.

Pia, alisema mwaka huu kuna maazimisho ya miaka 60 ya uhuru na miaka 59 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo skauti wanapaswa kujivunia na kuyatangaza.

“Kiapo cha skauti kinasema uskauti ni kuliunganisha Taifa. Rai yangu mchukue hatua ya kujilinda na korona (Uviko-19) na kuhamasisha kuchanja,” alisema huku akiongeza kuwa Taifa litakuwa na sensa ya watu na makazi na wakati huu majengo yatahesabiwa, ikiwamo kuweka anuani za makazi.

Skauti Mkuu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Skauti, Mwantumu Mahiza alimweleza Rais Samia kuwa skauti imesajili wanachama 800,000 hadi mwaka jana. Alisema vijana wengi hawana ajira, licha ya kuwa na elimu nzuri na alimuomba Rais afikirie hilo.

Pia, alimueleza namna skauti inavyounganisha vijana kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, vita dhidi ya Ukimwi, rushwa na kwamba wanatoa elimu kuhusu amani ya nchi, uzalendo na elimu ya ugani.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said ambaye ni Makamu wa rais wa Skauti nchini, alisema ndoto yake ni kuona mabadiliko.

Simai aliyataja mabadiliko anayotaka kuyaona kwenye Skauti ni kujenga watoto wenye ubunifu, wawe na uwezo wa kutafuta suluhisho, wenye ujuzi zaidi ya mmoja na raia wa dunia.

Pia, rais wa chama cha Skauti Tanzania ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema wametimiza agizo la Rais Samia la kuongeza wanachama hadi vyuo vikuu.

Skauti ilianzishwa na Robert Baden-Powell, ambaye ni luteni mstaafu wa Jeshi la Uingereza. Uskauti uliingizwa Tanganyika mwaka 1917 na Frank Weston, askofu wa Kanisa la Anglikana.