Samia apokea barua ya Chongolo kujiuzulu

Muktasari:
- Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda amesema Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan amepokea na kuridhia ombi la kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa chama hicho Daniel Chongolo.
Dar es Salaam. Hatimaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehitimisha uvumi wa kujiuzulu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu, Daniel Chongolo baada ya kutoa taarifa kuwa Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na mwanasiasa huyo.
Taarifa kuhusu Chongolo kuandika barua ya kuomba kujiuzulu zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu juzi na jana baadhi ya magazeti yaliandika yakionyesha kuwa barua iliandikwa Novemba 27, mwaka huu.
Katika barua hiyo, Chongolo amemwandikia Mwenyekiti wake, Rais Samia nia ya kujiuzulu kwa kile alichokifafanua anachafuliwa katika mitandao ya kijamii.
Uvumi huo, ulipata mashiko zaidi pale ambapo hakuonekana katika vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (NEC) vilivyofanyika leo, Jumatano, Novemba 28, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Taarifa za Rais Samia, kuridhia kujiuzulu kwa Chongolo, zimetolewa leo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda ambaye amesema kiongozi huyo aliijulisha NEC juu ya kukubali kujiuzulu kwa mtendaji mkuu wa chama hicho.
Akisoma taarifa hiyo Makonda amesema, "Mwenyekiti wa CCM na Rais Samia ameijulisha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ya Taifa kupokea barua ya kujiuzulu kwake (Chongolo) na ameridhia ombi hilo."
Mbali na taarifa kuhusu Chongolo, Makonda amesema kikao hicho kimejadili kuhusu hali ya siasa nchini na kufanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wagombea wa nafasi uongozi ndani ya CCM ngazi ya Mikoa na Wilaya.
Katika uteuzi huo kwa mujibu wa Makonda, Dk Daniel Pallangyo, Loy Sabaya na Edna Kivuyo wameteuliwa kuwania uenyekiti wa CCM katika Mkoa wa Arusha.
Aidha, katika Mkoa Mbeya ambao wanachama 48 walijitokeza, walioteuliwa kuwania nafasi hiyo ni Felix Lyaniva, Patrick Mwalunenge na Fatuma Kasenga.
Makonda amesema Mkoa wa Mwanza walijitokeza wagombea 109 na walioteuliwa ni Michael Masanja, Sabana Salinja, Dk Angelina Samike, Elizabeth Nyingi na David Mulongo.
Katika kinyang'anyiro cha uenyekiti wa Wilaya ya Mpanda, waliojitokeza ni wanachama 36 huku walioteuliwa ni Hamis Soud, Joseph Lwamba, Josephine Baraga na Emmanuel Manamba
Wilayani Kusini Unguja, waliojitokeza ni 15 na walioteuliwa ni Maryam Suleiman Haji, Ali Timamu Haji na Mohammed Haji Hassan.
Kikao cha NEC pia kimewapongeza Rais Samia na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025.