Samia afyeka mawaziri watatu, ateua wapya watatu

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassanamefanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri kwa kutengua uteuzi wa mawaziri watatu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi na kuteua mawaziri wapya watatu.

Ambao uteuzi wao umetenguliwa ni aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani; Ujenzi na Uchukuzi, Leonard Chamuriho na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile.
Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu leo usiku Septemba 12, 2021, kiongozi huyo amehamisha idara ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na kuipeleka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Walioteuliwa kuwa mawaziri ni Dk Stergomena Tax kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akichukua nafasi ya Elias Kwandikwa (marehemu).

Mbunge wa Bumbuli, January Makamba ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati huku Dk Ashatu Kijaji akiteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Mwingine ni Profesa Makame Mbarawa aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Dk Eliezer Feleshi ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Dk Kilangi aliyeteuliwa kuwa balozi.

Mawaziri wateule pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wataapisha kesho Septemba 13, 2021 Ikulu Chamwino Dodoma.
Haya ni mabadiliko ya kwanza kufanywa na Rais Samia tangu aapishwe kushika nafasi hiyo Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha hayati John Magufuli na ya kwanza tangu alipotangaza baraza la mawaziri Machi 31, 2021.