Prime
Sakata la kitita kipya bima ya afya

Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Benard Konga akizungumzia tamko chama cha watoa huduma na wamiliki wa vituo vya afya binafsi lililopinga gharama za kitita kipya cha matibabu kinachoanza utekelezaji wake Machi mosi, 2024.
Muktasari:
- Wenye vituo vya afya wamesema katika kitita kipya bei imeshuka kwa kati ya asilimia 20 hadi 30, wakati thamani ya Dola ya Marekani, dawa na ya uwekezaji zikiwa zimepanda.
Dar es Salaam. Wakati Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ukitangaza kuanza matumizi ya kitita kipya cha mafao kwa mwaka 2023, Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini (APHFTA), vimesema vituo vyao vitashindwa kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF kwa kutumia kitita hicho.
NHIF imesema kitita hicho kitaanza kutekelezwa Machi Mosi, mwaka huu.
Si mara ya kwanza kutokea mvutano kati ya pande hizi mbili, kwani Januari 4, 2024 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alikutana kwa mazungumzo na APHFTA baada ya kuibuka hali kama hiyo.
Baada ya mazungumzo, Serikali ilisitisha bei mpya za kitita cha matibabu zilizowekwa na NHIF na Waziri Ummy alitangaza kuunda kamati huru itakayofanya mapitio ya maboresho yaliyofanyika.
Maboresho ya kitita hicho yamefanyika ikiwa ni miaka minane tangu kufanyika kwa mchakato kama huo mwaka 2016, hivyo inaelezwa kuwepo haja kwa NHIF kufanya mapitio hayo kuendana na uhalisia wa soko na huduma zinazotolewa.
NHIF ikizungumza na wanahabari leo, Februari 28, 2024 kuhusu kuanza matumizi ya kitita hicho, APHFTA kupitia taarifa kwa umma iliyosainiwa na Mwenyekiti wake wa Taifa, Dk Egina Makwabe imesema mazungumzo yao na kamati maalumu ya Serikali iliyoundwa na Waziri Ummy yameshindwa kupata muafaka.
“Kama kitita kipya cha NHIF cha bei za huduma ya afya kilichopendekezwa na kamati teule ya waziri kitatangazwa kuanza kutumika, itakuwa kinyume cha mapendekezo ya Bunge ya kumalizwa tatizo hili kwa maridhiano.
“Hivyo, basi tunautangazia umma kuwa vituo binafsi vya afya vitashindwa kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF kwa kutumia kitita kisichokubalika kwetu. Ili kuepuka usumbufu, wanachama wa NHIF wanaombwa kuwasiliana na mfuko ili kujua namna ya kupata huduma hizo,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Dk Makwabe.
Undani wa madai
Akizungumza na Mwananchi Digital, mmoja wa maofisa waandamizi wa APHFTA ambaye hakutaka kutajwa jina amesema wamefikia uamuzi huo kwa kuwa utekelezaji wa kitita kipya ni hasara kwao.
Amesema katika kitita hicho bei imeshuka kwa kati ya asilimia 20 hadi 30, wakati thamani ya Dola ya Marekani, dawa na ya uwekezaji zikiwa zimepanda.
“Kwa bei mpya hasara tutakayopata itakuwa asilimia 20, pia makato ni asilimia tano mpaka 10 kwa hiyo hasara tunayopata kwa ujumla ni asilimia 30. Ikumbukwe vituo binafsi havipati ruzuku, hivyo tunategemea fedha hizo-hizo kulipa mishahara na kujiendesha,” amesema.
Ofisa huyo amesema hakuna vituo vya afya vinavyoweza kufanya kazi katika viwango vilivyopo sasa kwa gharama hizo, hivyo akashauri kama NHIF haina fedha za kutosha ilipie sehemu ya gharama na kuruhusu wananchi wachangie huduma.
Mwanachama mwingine wa APHFTA aliyekuwa mjumbe wa kamati iliyoundwa na Waziri Ummy (jina limehifadhiwa) amesema maboresho yanayotajwa yanawaumiza kutokana na kushushwa kwa gharama za matibabu.
"Ukimshushia mtu kipato chake kwa asilimia 25 hadi 30 hilo ni pigo kubwa, sasa unataka ajiendeshe kwa namna gani, tufanye kazi kwa hali ngumu? Kila kitu kimepanda sasa unapojaribu kushusha bei maana yake wanataka turudi nyuma kuanza kuchemsha sindano," amesema.
Amesema namna ya uendeshaji wa NHIF matumizi ni makubwa kiasi cha kuwasababishia hasara, hivyo wanafikiri mabadiliko wanayofanya ni kujaribu kukabiliana na hasara wanayopata.
Amesema maamuzi waliyochukua yatawaathiri, lakini hawawezi kukubaliana na mabadiliko yanayofanyika.
"Tumewaambia waondoe vitita vinavyowapa hasara, hospitali binafsi na Serikali tunalipwa kima sawa, lakini wenzetu wa Serikali wanapata ruzuku, hatuwezi kufanana, hivyo wapunguze bei kama hawataki basi wanachama wachangie hilo nalo wamekataa, kwa hiyo tunashindwa kuelewa wanataka sisi tufe wao wabaki?" amehoji.
Kilichoelezwa na NHIF
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga amesema kupitia maboresho wameongeza fedha za kumuona daktari bingwa kutoka Sh15,000 hadi Sh25,000, gharama za dawa zimeongezeka kufikia Sh10,000 kutoka bei ya awali ya Sh3,000.
“Kuna dawa tulikuwa tunalipa kati ya Sh500,000 hadi Sh600,000 kumbe zimeshuka hadi Sh400,000 kwenye bei ya soko, hatuwezi kuendelea hivyo. Ili mfuko uwe endelevu ni lazima tuangalie nini kilichopo kwenye soko tuweze kukifanyia kazi,” amesema.
Konga aliyesema hakuwa na taarifa kuhusu kilichoelezwa na APHFTA, hata hivyo amesema:
“Milango yetu ipo wazi wakituletea maoni kabla ya Machi mosi tunaweza kuyafanyia kazi yakawa sehemu ya kitita kipya, lakini hata baada ya tarehe hiyo tutapokea maoni na maelekezo tuliyonayo ni kuendelea kuyapokea kwa kuwa tunaweza kuyatumia kwenye maboresho yajayo.
“Tusingependa mwanachama yeyote akose huduma na hilo tunawahakikishia, hakuna namna mwanachama atakosa huduma, hivyo waje watueleze shida yao ni nini, yale maeneo wanayotaka tuyafanyie kazi. Hilo tamko sijaliona, ila tutalifuatilia tuone ni eneo gani wanasema halijafanyiwa kazi,” amesema Konga.
Hata hivyo, amesema; “Ila vituo ni suala la kimkataba, tuliingia mkataba na kituo kimoja-kimoja, hivyo ikifikia hatua ya kusitisha huduma kuna maelekezo ya nini cha kufuata, ili mfuko tuweze kujua. Nitoe wito kwa mameneja wa mikoa kutoka kufuatilia hali ya utoaji huduma kwenye vituo, lengo ni kuhakikisha mwanachama hapati changamoto yoyote.”
Kuhusu NHIF kufungua milango ya mazungumzo, ofisa huyo wa APHFTA amesema wameshazungumza kwa takribani miezi mitatu, hivyo kama hakutakuwa na mabadiliko wataendelea na msimamo wao wa kutotoa huduma kwa wagonjwa wa NHIF kuanzia Machi mosi.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipotafutwa na Mwananchi Digital amesema Serikali itazifanyia kazi tofauti zilizopo baina ya pande hizo mbili, ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya, hivyo kama kuna tatizo basi zitafanyika kila jitihada kujadiliana na watoa huduma, ili kuhakikisha huduma hazikosekani,” amesema Matinyi.
Kauli ya mdau
Akizungumzia mvutano huo, mshauri wa masuala ya afya, Festo Ngadaya amesema utaleta taharuki kwa wananchi.
"Taharuki hii inakuja kwa sababu tupo katika kipindi ambacho tunahangaika kujenga jina na uaminifu kwa NHIF, tunawafanya wananchi kuiamini taasisi hii hasa tunapoelekea kwenye Bima ya Afya kwa Wote, sasa tunapowaona hawa mafahari wawili wakigombana athari inakwenda kwa mwananchi," amesema.
Ngadaya amesema mwananchi atakapokwenda kufuata huduma akakosa kwa sababu ya kadi yake kukataliwa anapoteza uaminifu na NHIF, hivyo kupoteza utayari wa kujiunga na bima ya afya.
Amesema NHIF kwa sasa haipaswi kuangalia kupata faida yoyote kutokana na bima hiyo kutokuwa na wachangiaji wengi, hivyo njia ya kutatua tatizo hilo si kubadili vifurushi na baadhi ya huduma.
"Watu wakae chini waangalie namna ya kuipeleka sokoni NHIF, ukibadili vifurushi unapoteza watu, suluhu iletwe bima ya afya kwa wote iliyo nafuu na kila mtu atachangia. Athari watakayopata Aphfta kwao ni kukosa mapato yanayotoka kwa NHIF," amesema.
Kauli ya madaktari
Madaktari kwa upande wao wamesema hawana tatizo na maboresho yaliyofanyika na wako tayari kuendelea kutoa huduma kitita kitakapoanza kutumika.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndilanha amesema madaktari hawana tatizo kwa kuwa mapendekezo yao yamefanyiwa kazi kwa asilimia kubwa.
“Kwenye maboresho ya kwanza kulikuwa na maeneo ambayo hatukuridhishwa nayo, tulitoa maoni yetu mbele ya kamati na kwa kiasi kikubwa waliyachukua na tumeona yamefanyiwa kazi hasa yale yanayohusu masilahi ya madaktari,” amesema na kuongeza:
“Kutokana na uhalisia huo, hatuna malalamiko tuko tayari kuendelea kutoa huduma, ingawa yapo maeneo mengine ambayo tumekubaliana watayafanyia maboresho kuelekea mbele, hatuna shida na hilo kwa kuwa yale yote ya msingi yanayomhusu daktari na utendaji kazi wake yamefanyiwa kazi.”
Kuhusu kitita kipya
Akizungumza kitita hicho cha mafao, Konga amesema yalifanyika maboresho yaliyolenga kuangalia maeneo kadhaa ikiwemo upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo awali.
Kitita pia kinalenga kufanya maboresho ya huduma na gharama zake kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na hali halisi ya bei katika soko, kuwianisha kitita cha mafao na miongozo ya tiba iliyoboreshwa, ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa mfuko.
Sababu nyingine amesema ni kujumuisha maoni na mapendekezo ya wadau, kutekeleza ushauri wa taarifa ya mapendekezo ya tathmini ya uhai na uendelevu wa mfuko na kuimarisha udhibiti katika mianya ya udanganyifu.
Ameyataja maeneo yaliyofanyiwa mapitio na maboresho katika kitita hicho kuwa ni ada ya usajili na kupata ushauri wa daktari, huduma za dawa, vipimo, upasuaji na gharama za kliniki za kawaida na kibingwa.
“Hapa kwenye huduma za usajili na kupata ushauri wa daktari tumewezesha madaktari kufanya kazi katika ngazi zote kutokana na kuwepo kwa usawa wa ada ya kumwona daktari kwa ngazi zote kwa madaktari wa kada zinazoendana.
“Hii itasaidia wanachama kupata huduma za kibingwa katika ngazi mbalimbali za vituo kwa kuzingatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya,” amesema.
“Tumeongeza wigo wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi za upasuaji na vipimo katika hospitaji za rufaa ngazi ya Kanda na Taifa. Maboresho haya yataongeza upatikanaji wa huduma za matibabu ya saratani, upasuaji wa mifupa, upasuaji wa moyo katika hospitali si za Taifa tu, bali hata hospitali za Kanda, hivyo kusogeza huduma karibu zaidi na maeneo ya wananchi,” amesema Konga.
Kuhusu dawa, amesema maboresho hayo yataongeza upatikanaji wa huduma za dawa katika vituo vya ngazi ya msingi, mfano dawa za matibabu ya shinikizo la damu na kisukari na kuongeza dawa mpya 247 ambazo hazikuwepo awali ili ziwepo kwenye Mwongozo wa Orodha ya Dawa Muhimu za Taifa (Nemlit).
“Jumla ya dawa 736 zimefanyiwa mapitio kwa kuzingatia bei za soko na gharama za uendeshaji na wastani wa faida. Hii itaondoa changamoto ya wanachama kukosa baadhi ya huduma za dawa kutokana na changamoto ya bei,” amesema.
Maboresho hayo yamegusa pia huduma za upasuaji na vipimo, ambazo gharama za vipimo 311 na huduma za upasuaji zimefanyiwa mapitio kwa kuzingatia bei za soko katika ununuzi wa vifaa na vitendanishi, gharama za uendeshaji na wastani wa faida.