NHIF, watoa huduma binafsi bado ngoma ngumu

Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Benard Konga akizungumzia tamko chama cha watoa huduma na wamiliki wa vituo vya afya binafsi lililopinga gharama za kitita kipya cha matibabu kinachoanza utekelezaji wake Machi mosi, 2024.
Muktasari:
- Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema Serikali itazifanyia kazi tofauti zilizopo baina ya pande hizo mbili.
Dar es Salaam. Siku moja kabla ya kuanza matumizi ya kitita kipya cha mafao kwa mwaka 2023 cha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini (APHFTA), vimesema vituo binafsi vitashindwa kutoa huduma kwa wanachama wa mfuko huo kwa kutumia kitita hicho.
Kitita hicho kimepangwa kuanza kutekelezwa Machi Mosi, 2024.
Maboresho ya kitita hicho yamefanyika ikiwa ni miaka minane tangu kufanyika kwa mchakato kama huo mwaka 2016, hivyo kuwepo haja kwa NHIF kufanya mapitio hayo, ili kuendana na uhalisia wa soko na huduma zinazotolewa.
NHIF ikizungumza na wanahabari leo, Februari 28, 2024 kuhusu kuanza matumizi ya kitita hicho, huku APHFTA kupitia taarifa kwa umma iliyosainiwa na mwenyekiti wake wa Taifa, Dk Egina Makwabe ikieleza mazungumzo yao na kamati maalumu ya Serikali iliyoundwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu yameshindwa kupata muafaka kuhusu kitita hicho kipya cha NHIF.
“Kama kitita kipya cha NHIF cha bei za huduma ya afya kilichopendekezwa na kamati teule ya waziri kitatangazwa kuanza kutumika, itakuwa kinyume cha mapendekezo ya Bunge ya kumalizwa tatizo hili kwa maridhiano.

“Hivyo basi tunautangazia umma kuwa vituo binafsi vya afya vitashindwa kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF kwa kutumia kitita kisichokubalika kwetu. Ili kuepuka usumbufu, wanachama wa NHIF wanaombwa kuwasiliana na mfuko, ili kujua namna ya kupata huduma hizo,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Dk Makwabe.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga amesema hana taarifa kuhusu taarifa ya APHFTA.
“Milango yetu ipo wazi wakituletea maoni kabla ya Machi mosi tunaweza kuyafanyia kazi yakawa sehemu ya kitita kipya, lakini hata baada ya tarehe hiyo tutapokea maoni na maelekezo tuliyonayo ni kuendelea kuyapokea kwa kuwa tunaweza kuyatumia kwenye maboresho yajayo.
“Tusingependa mwanachama yeyote akose huduma na hilo tunawahakikishia hakuna namna mwanachama atakosa huduma, hivyo waje watueleze shida yao ni nini, yale maeneo wanayotaka tuyafanyie kazi. Hilo tamko sijaliona ila tutalifuatilia tuone ni eneo gani wanasema halijafanyiwa kazi,” amesema Konga.
Amesema kupitia maboresho hayo wameongeza fedha za kumuona daktari bingwa kutoka Sh15,000 hadi Sh25,000, gharama za dawa zimeongezeka kufikia Sh10,000 kutoka bei ya awali ya Sh3,000.
“Kuna dawa tulikuwa tunalipa kati ya Sh500,000 hadi Sh600,000 kumbe zimeshuka hadi Sh400,000 kwenye bei ya soko, hatuwezi kuendelea hivyo. Ili mfuko uwe endelevu ni lazima tuangalie nini kilichopo kwenye soko tuweze kukifanyia kazi. Kwa kuwa wametoa tamko tutakaa tuzungumze nao.
“Ila vituo ni suala la kimkataba, tuliingia mkataba na kituo kimoja-kimoja, hivyo ikifikia hatua ya kusitisha huduma kuna maelekezo ya nini cha kufuata, ili mfuko tuweze kujua.
“Nitoe wito kwa mameneja wa mikoa kutoka kufuatilia hali ya utoaji huduma kwenye vituo, lengo ni kuhakikisha mwanachama hapati changamoto yoyote,” amesema.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipotafutwa na Mwananchi Digital amesema Serikali itazifanyia kazi tofauti zilizopo baina ya pande hizo mbili, ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya, hivyo kama kuna tatizo basi zitafanyika kila jitihada kujadiliana na watoa huduma ili kuhakikisha huduma hazikosekani,” amesema Matinyi.
Januari 4, 2024 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alikutana kwa mazungumzo na APHFTA. Baada ya hapo, Serikali ilisitisha bei mpya za kitita cha matibabu zilizowekwa na NHIF.
Waziri alitangaza kuunda kamati huru itakayofanya mapitio ya maboresho yaliyofanyika.
Kuhusu kitita kipya
Akizungumza kitita hicho cha mafao, Konga amesema yalifanyika maboresho yaliyolenga kuangalia maeneo kadhaa, ikiwemo upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo awali.
Kitita pia kinalenga kufanya maboresho ya huduma na gharama zake kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na hali halisi ya bei katika soko, kuwianisha kitita cha mafao na miongozo ya tiba iliyoboreshwa, ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa mfuko.
Sababu nyingine, amesema ni kujumuisha maoni na mapendekezo ya wadau, kutekeleza ushauri wa taarifa ya mapendekezo ya tathmini ya uhai na uendelevu wa mfuko na kuimarisha udhibiti katika mianya ya udanganyifu.
Ameyataja maeneo yaliyofanyiwa mapitio na maboresho katika kitita hicho kuwa ni ada ya usajili na kupata ushauri wa daktari, huduma za dawa, vipimo, upasuaji na gharama za kliniki za kawaida na kibingwa.

“Hapa kwenye huduma za usajili na kupata ushauri wa daktari tumewezesha madaktari kufanya kazi katika ngazi zote kutokana na kuwepo kwa usawa wa ada ya kumwona daktari kwa ngazi zote kwa madaktari wa kada zinazoendana. Hii itasaidia wanachama kupata huduma za kibingwa katika ngazi mbalimbali za vituo kwa kuzingatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya,” amesema.
“Tumeongeza wigo wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi za upasuaji na vipimo katika hospitaji za rufaa ngazi ya Kanda na Taifa. Maboresho haya yataongeza upatikanaji wa huduma za matibabu ya saratani, upasuaji wa mifupa, upasuaji wa moyo katika hospitali si za Taifa tu, bali hata hospitali za kanda, hivyo kusogeza huduma karibu zaidi na maeneo ya wananchi,” amesema Konga.
Kuhusu dawa, amesema maboresho hayo yataongeza upatikanaji wa huduma za dawa katika vituo vya ngazi ya msingi, mfano dawa za matibabu ya shinikizo la damu na kisukari na kuongeza dawa mpya 247 ambazo hazikuwepo awali ili ziwepo kwenye Mwongozo wa Orodha ya Dawa Muhimu za Taifa (Nemlit).
“Jumla ya dawa 736 zimefanyiwa mapitio kwa kuzingatia bei za soko na gharama za uendeshaji na wastani wa faida. Hii itandoa changamoto ya wanachama kukosa baadhi ya huduma za dawa kutokana na changamoto ya bei,” amesema.
Maboresho hayo yamegusa pia huduma za upasuaji na vipimo, ambazo gharama za vipimo 311 na huduma za upasuaji zimefanyiwa mapitio kwa kuzingatia bei za soko katika ununuzi wa vifaa na vitendanishi, gharama za uendeshaji na wastani wa faida.