Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu madaktari, hospitali binafsi kupinga maboresho NHIF

Dar es Salaam. Maboresho yaliyofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwenye ada ya usajili na ushauri wa daktari, yameibua sintofahamu baada ya hospitali binafsi na madaktari bobezi kuyapinga.

NHIF juzi ilitangaza mapitio ya kitita cha mafao kwa mwaka 2023, ikisema imewashirikisha wadau, lengo likiwa ni kufanya baadhi ya huduma ziendane na bei halisi ya soko.

Siku moja baada ya kuanika mpango wake huo, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimetoka hadharani na kusema hakikushirikishwa katika mchakato huo.

Hata Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphta) kilichokiri kushirikishwa kwenye mchakato huo, kimesema hawakuafikiana na viwango vilivyotajwa.

NHIF kupitia taarifa yake iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, imeonyesha kuwa miongoni mwa wadau walioshirikishwa ni MAT na Aphta.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray alisema kwa kipindi cha mwaka mzima, wamekuwa wakifanya vikao vya kushirikisha wadau, wakiwemo MAT, kuhusu mabadiliko hayo.

“Ushirikishwaji ulikuwa mkubwa kwa kipindi cha mwaka mzima, tangu tulipoanza hakuna mdau ambaye hakushirikishwa, Aphta tulikaa nao hadi juzi,” alisisitiza.

Taarifa iliyotolewa juzi na Rais wa MAT, Dk Deusdedit Ndilanha iliwataka wanachama na wadau wa afya kuwa na subira na kwamba chama kitatoa tamko rasmi na msimamo wake baada ya kikao cha kamati ya utendaji.

“Chama kimeshtushwa na taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha kushiriki kwenye mapendekezo ya kitita cha mafao cha mwaka 2023 cha NHIF. Chama kinakanusha kushiriki na kushirikishwa kwenye mchakato huu,” alisema Dk Ndilanha.

Moja ya masuala makubwa yanayowagusa madaktari hao, ni kuhusu viwango vya ada za kumuona daktari vilivyopangwa na NHIF.

Katika mabadiliko ya ada ya usajili na ushauri wa daktari, viwango vya mgonjwa kumuona daktari Hospitali ya Taifa vimeshushwa hadi Sh25,000 kutoka Sh35,000 kwa daktari bingwa mbobezi, Sh20,000 kutoka Sh 25,000 kwa daktari bingwa.

Mabadiliko mengine ni kwenye hospitali ya rufaa ya kanda ambapo kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh35,000 na kumuona daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh25,000.

Hospitali ya mkoa, gharama zimepanda ambapo kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh15,000 na kwa daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh15,000.

Pia kwa kliniki bobezi (za matibabu ya kibingwa), kumuona daktari bingwa mbobezi na daktari bingwa gharama zitakuwa Sh10,000 kutoka Sh15,000 za awali na kwenye kliniki za kawaida kumuona daktari bingwa na bingwa mbobezi zimesalia Sh10,000.

Marekebisho hayo kwa mujibu wa NHIF yamelenga kuongeza wigo wa utoaji huduma za kibingwa kuanzia ngazi ya rufaa ya kanda hadi Taifa.

Hata hivyo, Dk Ndilanha alisema hawajakubaliana na maboresho hayo na kwamba, watatoa taarifa rasmi.

Alisema maboresho hayo yamekuja ghafla na licha ya baadhi ya wataalamu kushirikishwa, MAT haikushirikishwa.

"Haya maboresho hatuyaungi mkono. Kiwango cha fedha cha kumuona daktari kimeshuka kwa hospitali za rufaa na kanda, ndiyo hayo mabadiliko madogo lakini hayana tija sana kwa sababu sisi tulifikiri kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa unafanyika, wataalamu wetu pia wangepewa motisha.

"Wanasoma udaktari bingwa na ubobezi kwa miaka mingi, lakini kitu cha kwanza ni kuwakandamiza. Badala ya kushusha kiwango cha kumuona daktari, wangeongeza.

“Ada hii huwa haishuki, wamewavunja moyo sana (madaktari) na tunaona italeta taharuki kidogo. Huwezi kusema ada ya mwaka 2016 ilikuwa kubwa kidogo na 2023 ukapunguza," alisema Dk Ndilanha.

Alisema suala hilo haliendani na kujitokeza kwa wataalamu na hali halisi ya maisha ya sasa, kwani ada hiyo ilitakiwa kuongezeka.

"Mabadiliko haya yanakwenda kupunguza morali, sidhani kama yanasapoti juhudi za Serikali kuwekeza huku kwetu, ikiwemo Super Specialisation Program (mpango wa ubobevu) ya Mama Samia Suluhu Hassan ambapo wataalamu wakihitimu wanakwenda kufanya kazi hospitali za rufaa na kanda," alisema Rais huyo wa MAT.

Hata hivyo, wakati daktari huyo akisema hayo, juzi akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema kila baada ya miaka mitatu, mfuko huo hufanya maboresho ya huduma zake.

“Maboresho haya yako wazi na huwa tunawashirikisha wadau wetu wote, na safari hii tumefanya hivyo pia. Na hapa tunapomaliza kikao hiki na ninyi wahariri, tunaendelea na watoa huduma katika ukumbi huu huu,” alisema Konga.


Hospitali binafsi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphta), Dk Egina Makwabe alisema NHIF iliwashirikisha kwenye mabadiliko hayo, lakini hawakuafikiana juu ya mabadiliko hayo.

Alisema kinachowashangaza ni kuona NHIF imefanya uamuzi ambao hawakuutarajia.

“Mabadiliko sio mazuri, sekta binafsi tutaumia kwa kiwango kikubwa, tutatoa tamko kesho (leo) au kesho kutwa. Gharama ya kumuona daktari imeshuka kuanzia ngazi ya mkoa hadi kituo cha afya, kuna vipimo vimeshuka na dawa nyingi bei zake zimeshushwa,” alisema.

Pamoja na malalamiko hayo, upande wa wamiliki wa vituo vya afya kwao ni kicheko baada ya bei za dawa kupandishwa kwa wastani wa asilimia 10 hadi 20.

Hali hiyo imetokea baada ya suala la mabadiliko ya gharama kujadiliwa kwa miaka mingi bila kufikia muafaka na NHIF na hivyo kuendelea kutumia gharama za mwaka 2016, licha ya mabadiliko mengi yaliyotokea, kwa mujibu wa Dk Makwabe.

Kwa mfano, anasema dawa ya Paracetamol (maarufu panado) mwenye hospitali alinunua kwa Sh35 kwa kidonge hadi Sh250 kutegemeana na mtengenezaji, lakini NHIF ilimlipa mtoa huduma Sh20 kwa kidonge.


Unafuu huduma

Kupitia maboresho ya kitita cha mafao yaliyofanywa na NHIF, wananchi watanufaika kutokana na kuongezwa kwa huduma ambazo hazikuwepo na kupungua kwa baadhi ya huduma.

Chini ya mabadiliko hayo, wanachama ambao kuanzia Januari mosi 2024, watapata huduma ya vifaa pandikizi, kupandikizwa viungo, upasuaji wa moyo, huduma za upasuaji kwa njia ya video/mtandao na vifaa bandia kupitia bima watapata unafuu.

Fursa nyingine ya matibabu kwa wanachama ni kuongezwa kwa dawa 124 kwenye orodha ya dawa muhimu ya Taifa.

Pia, kupitia mabadiliko hayo, kutakuwepo mbadala wa dawa 309 katika kitita cha mafao ili kuwianisha na zilizopo kwenye orodha ya dawa muhimu.

Kundi lingine litakalonufaika na mabadiliko hayo, kwa mujibu wa NHIF, ni watoa huduma za afya ambao wataongezewa motisha kuanzia ngazi ya afya ya msingi ambapo kumuona daktari ilikuwa Sh1,000, sasa inakwenda kuwa Sh2,000.

Hata hivyo, licha ya maboresho hayo, bado Dk Makwabe alisema maboresho hayo hayakidhi haja, bali yanakwenda kuiumiza sekta binafsi na uwezekezaji kwenye sekta ya afya utakuwa mgumu.


Ugumu sekta binafsi

Kwa mujibu wa Dk Makwabe, ugumu watakaokutana nao wenye hospitali binafsi ni ulipaji wa mishahara ambao utaanza kuwa kikwazo kwao na uboreshaji wa huduma tofauti na hospitali.

“Wanasema wameboresha bei lakini huku ni kushusha, kila kitu sasa kimepanda bei, mafuta, dola imepanda na shilingi imeshuka thamani,” alisema.

“Itakuwa ngumu kuendesha kituo cha afya na vigumu kituo cha afya kukua kwa bei hizo za NHIF. Tumekaa vikao vingi lakini hatujakubaliana,” alihitimisha.