Safari za baharini zarejea kimbunga Hidaya kikipoteza nguvu

Boti ikiwa safarini kuelekea Zanzibar, ikitokea katika bandari ya Dar es Salaam leo Mei 05,2024.  Picha Michael Matemanga

Muktasari:

  • TMA katika taarifa iliyotolewa saa 5.59 usiku wa kuamkia leo Mei 5, 2024 imesema kimbunga Hidaya kimepoteza nguvu kabisa baada ya kuingia nchi kavu katika Kisiwa cha Mafia.

Unguja/Dar.  Baada ya kujiridhisha kuwa hali ya hewa imetulia na upepo kupungua, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeruhusu usafiri wa majini kuendelea kama kawaida.

Usafiri wa meli na boti  kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam, Unguja kwenda Pemba na Pemba kwenda Tanga ulizuiwa tangu jana Mei 4, 2024 saa moja asubuhi kutokana na upepo mkali ulioanza kuvuma saa 3.00 usiku wa Mei 3, 2024  uliosababishwa na kimbunga Hidaya.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kimbunga hicho kilipoteza nguvu kadri kilivyokuwa kikisogea nchi kavu.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 5, 2004 Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Sheikha Ahmed Moh'd amesema baada ya kujiridhisha na utulivu wa hali ya hewa wameruhusu safari ziendelee.

"Tulikuwa bado tunaangalia hali ikoje lakini kwa sasa tumeona imetulia na tumeruhusu safari ziendelee kama kawaida, kwa hiyo kuna boti inaenda Dar es Salaam na meli inaondoka kwenda Pemba," amesema.

Hata hivyo, Sheikha amesema wataendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali ya hewa ili yakitokea mabadiliko wachukue hatua za haraka kuzuia.

Enock Isaya, ni miongoni mwa abiria ambaye amesema licha ya kusafiri bado ana hofu kutokana na mabadiliko yanayoweza kutokea.

"Nitaondoka na boti ya saa 3.00 asubuhi, hakuna jinsi lazima kusafiri japo huwezi kujiachia kwani bado tahadhari inawekwa," amesema.

Taarifa ya mwisho iliyotolewa na TMA saa 5.59 usiku wa kuamkia leo Mei 5, imesema kimbunga Hidaya kimepoteza nguvu kabisa baada ya kuingia nchi kavu katika Kisiwa cha Mafia.

TMA kupitia mwendelezo wa taarifa zake kuhusu kimbunga Hidaya imesema:

"Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa wa kilichokuwa kimbunga Hidaya zilizokuwa zikitolewa na TMA tangu Mei 1, 2024, mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa katika kipindi cha saa sita zilizopita, kimbunga Hidaya kimepoteza kabisa nguvu baada ya kuingia nchi kavu katika Kisiwa cha Mafia."

Taarifa ya TMA imesema mabaki ya mawingu yaliyokuwa yameambatana na kimbunga hicho yamesambaa katika maeneo mbalimbali ukanda wa kusini hususani katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro, hivyo hakuna tena tishio la kimbunga Hidaya.


Hali ilivyo Dar

Leo Jumapili Mei 5, 2024 katika maeneo ya Posta, shughuli za usafiri wa boti kuelekea Unguja ziliendelea kama kawaida kuanzia saa moja asubuhi.

Msimamizi wa Uendeshaji Boti za Kilimanjaro, Ally Juma amesema wamerejesha usafiri baada ya mamlaka husika kuwaruhusu kutokana na hali ya hewa kutengamaa tofauti na jana Jumamosi Mei 4, 2024.

"Mamlaka imejiridhisha na hali ya hewa ndiyo maana tumeruhusiwa, ila kwa Zanzibar zitachelewa kutoka tofauti na huku kulingana na hali ya hewa ya kule. Kifupi hali ya hewa ya bahari ipo shwari,” amesema.

"Abiria wapo wengi kama kawaida, ingawa jana baada ya kusitisha wapo tuliowarejeshea fedha zao na wale waliobaki na tiketi wamekuja nazo leo, tunaendelea na shughuli zetu lakini tunafuatilia kwa ukaribu Mamlaka ya Hali ya Hewa," amesema Juma.

Mmoja wa makuli katika eneo hilo, Hamad Mshana amesema kusitishwa kwa safari kuliwaweka katika mazingira magumu, lakini wanamshukuru Mungu kutokana na kimbunga Hidaya kupoteza nguvu yake.

"Unajua shughuli zetu zinategemea abiria kuwepo katika eneo hili, wasipokuwapo inakuwa mtihani, tunamshukuru Mungu leo mambo mazuri," amesema Hamad.

Mmoja wa abiria aliyekuwa akisafiri kuelekea Unguja ameshukuru hali ya hewa kutengemaa na Serikali kurejesha usafiri.

Dereva wa pikipiki, maarufu bodaboda katika maeneo ya Posta, Aloyce John amesema huwa hafanyi kazi Jumapili, lakini leo amelazimika kuingia kazini ili kufidia siku ya jana Jumamosi kutokana na shughuli za usafiri wa Dar es Salaam kwenda Unguja kusitishwa.

Samaki hawashikiki Feri

Katika hatua nyingine, upatikanaji wa samaki bado ni mgumu kutokana na hali ya hewa na wavuvi kutokuingia baharini kuvua.

"Hivi sasa dagaa mchele ndoo kubwa ya lita 20 wanauzwa kati ya Sh130,000 hadi Sh150,000 kutoka Sh50,000 na Sh45,000 yaani hawashiki kabisa," amesema Said Rashid, mchuuzi wa samaki.

Amesema hali hiyo inawaathiri waoshaji na watengenezaji wa samaki, wauza barafu, mifuko na mamalishe wanaotegemea shughuli hizo kujipatia vipato.

"Tunaomba Mungu hali itengemae ili turudi katika maisha yetu ya kawaida, maana hapo tulipo tupo tu, hatuna shughuli za kufanya," amesema Rashid.

Mfanyabiashara Juma Rashid amesema, "samaki ni bei kubwa kwa sasa wenye uwezo ndio wanaomudu kuwanunua, ukija Jumapili hapa Feri huwezi kukuta watu wachache kama hivi hasa kwenye minada lakini leo hali ni kama inavyoonekana," amesema.

TMA ilianza kutoa tahadhari ya kimbunga hicho tangu Mei 1, 2024 kilikuwa na mwendokasi wa kilomita 130 kwa saa kabla hakijapungua nguvu.

Hii ni mara ya pili ndani ya miaka minne vimbunga kupungua nguvu vikiwa vinaingia nchini.

Aprili 25, 2021 kimbunga Jobo kilipoingia Pwani ya Bahari ya Hindi kilipungua nguvu na kutoweka.