Sababu ya kusuasua mradi wa Liganga na Mchuchuma yatajwa

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
Serikali ya Tanzania imesema mradi wa Liganga na Mchuchuma umekwama kuzna kutokana na mazunguzo yanayoendelea kati yake na mwekezaji huo anayetaka kupewa vivutio vya ziada
Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema majadiliano kati yake na mwekezaji anayetaka kupewa vivutio vya ziada ndio sababu ya kusuasua kuanza wa mradi wa chuma na makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 20, 2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya wakati akijibu swali la mbunge wa Viti maalum (Chadema), Lucia Mlowe aliyetaka kujua mradi huo utaanza lini.
Manyanya amesema changamoto ni majadiliano kati ya mwekezaji na Serikali ya Tanzania kuhusu vivutio vya uwekezaji kuchukua muda mrefu kutokana na mwekezaji kutaka kupewa vivutio vya ziada ambavyo havipo kisheria.
“Serikali inaangalia njia bora ya kuhakikisha mradi huo unatekelezwa ili kuleta manufaa mapana kwa wananchi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla,” amesema Manyanya.
Amebainisha Serikali inafahamu umuhimu wa mradi huo katika ujenzi wa uchumi, kwamba hatua za awali za ujenzi wa mradi zimeshaanza kutekelezwa.
“Hatua hiyo ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu, kupata cheti cha mazingira kwa miradi iliyotekelezwa, kujenga barabara kuu la lami ili kurahisisha usafirishaji wa mitambo na huduma nyingine katika eneo la mradi, kufanya uthamini wa mali na maeneo ya wananchi watakaopitisha mradi,” amesema Manyanya.
Katika swali la nyongeza, Mlowe alitaka Serikali kubadili mwekezaji katika mradi huo na Manyanya kubainisha kuwa kutokana na umuhimu wa mradi huo ni lazima umakini uwe mkubwa ikiwezekana atatafutwa mwekezaji mwingine jambo alilodai kuwa si la siku moja au mbili.
Mei 16, 2019 aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda alitangaza mpango wa kuanza uchimbaji wa makaa ya mawe ya Liganga licha ya kuwepo kwa mlolongo wa mambo ambayo yameorodheshwa.
Alitaja mambo mengi ambayo yanatakiwa kukamilishwa kabla ya kuanza kwa uchimbaji huo ambayo ni pamoja na kupitia mkataba na mwekezaji na kugawanya kwa mkataba usiwe Liganga na Mchuchuma ili kila mradi ujitegemee.
Mambo mengine ni ulipaji wa fidia, umeme, ujenzi wa miundombinu na kupitia upya baadhi ya vipengele.