Prime
Sababu mafuriko ya Rufiji hii hapa

Muktasari:
- Bwawa hilo lenye uwezo wa kubeba maji mita ujazo bilioni 34 limejaa na kiasi fulani kikaachiwa kiingie Mto Rufiji, hatua ambayo imesababisha mafuriko kwa vijiji vilivyopo pembezoni kwa mto huo.
Dar es Salaam. Kata 12 kati ya 13 za Rufiji zimeathirika na mafuriko kutokana na maji yanayoelezwa kufunguliwa kwenye Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) ambalo limejaa wilayani humo.
Bwawa hilo lenye uwezo wa kubeba maji mita ujazo bilioni 34 limejaa na kiasi fulani kikaachiwa kiingie Mto Rufiji, hatua ambayo imesababisha mafuriko kwa vijiji vilivyopo pembezoni kwa mto huo.
Tathmini ya awali, kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele imebaini kuharibiwa kwa nyumba na wananchi kukosa makazi hivyo kuondolewa kwenye maeneo yao. Pia zaidi ya hekta 28,374.74 za mazao ya kilimo na biashara ikiwamo mahindi, mpunga, ufuta na migomba zimeathiriwa.
Mamlaka zimesema uwezekano wa wanafunzi kurejea shuleni mara shule zitakapofunguliwa uko shakani kutokana na maeneo yake kuzingirwa na maji.
Mkazi wa Kijiji cha Chumbi, Halima Mbwana, ambaye ni miongoni mwa waathirika wa mafuriko hayo alidai hali inazidi kuwa mbaya kuanzia kupata chakula, malazi na makazi.
“Tumesalia watupu, mazao shambani yamesombwa na maji na hata vyakula vya ziada tulivyokuwanavyo vimesombwa pia, nyumba nazo zimesombwa na sasa hatuna pa kuishi wala chakula, tunaomba tusaidiwe maana hali zetu ni mbaya,” alisema Mbwana.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu maji yaliyofunguliwa JNHPP, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamohanga amesema bwawa hilo limejaa na kwa asilimia kubwa ndilo lililosaidia kupunguza mafuriko ya Rufiji na Kibiti.
“Kwa kawaida eneo lile lina mafuriko, endapo maji yangekuta hakuna bwawa yakapita, shida ingekuwa kubwa zaidi. Bwawa hili lilipojengwa lilisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mafuriko maeneo hayo kwa kuwa tulikuwa tunayadaka na kuyaingiza kwenye bwawa kipindi chote.
“Maji yaliyokuja mwaka huu ni mengi, Februari 15 yalikuja maji mita za ujazo 8,000, yalikuta bwawa halijajaa, tukayadaka,” amesema Nyamohanga.
Amesema baada ya kujaa wameruhusu mita za ujazo 2,000 au 3,000 zitoke ziingie mtoni, ambazo endapo wangeziachia ziingie kwenye bwawa, zingekuwa na madhara kwa kuwa tayari limejaa.
“Kabla (ya kuyaruhusu) tulitoa taarifa kwa maandishi kwenye halmashauri, kwa mkuu wa wilaya na mkoa kuwaambia kuwepo uwezekano wa mafuriko kipindi hiki, hivyo wale waliosogea sana karibu na mto wahame.
“Lile eneo si sehemu sahihi ya kujenga, wala kulima, kwani kwenye mkondo wa Mto Rufiji mafuriko ni kawaida yake. Hata kwenda kujengwa bwawa ni kwa kuwa palionekana pana mafuriko ya asili,” amesema.
Amesema wakati wa ujenzi, maji yote yalikuwa yakidakwa na kuingia huko (bwawani).
“Changamoto nyingine ni mvua za El-Nino, kimsingi mwaka huu kumekuwa na mvua kubwa, hata hivyo kama shirika tunaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kutoa msaada na kuwahamisha wale wanaotakiwa kuhama,” alisema Nyamohanga.
Kata 12 zasombwa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rufiji, Abdul Chobo amesema mafuriko hayo yamesabisha athari katika kata 12 kati ya 13 za Jimbo hilo: “Na yameharibu miundombinu ya barabara, makazi ya wananchi, mazao na kusimamisha shughuli za maendeleo.”
Amezitaja kata hizo ni Mohoro, Chumbi, Mbwara, Ikwiriri, Umwe, Mgomba, Mkongo, Ngorongo, Kipugira, Mwaseni na Utete.
Chobo, ambaye pia ni Diwani Mohoro alisema kuna shule zilizoko kwenye maeneo ambayo wanafunzi wanapata matatizo kufika shuleni kwa sababu ya njia za kupita kujaa maji ambazo ni shule ya msingi Mohoro, King'ongo, Ndundutawa na Kanga.
Amesema, pia kuna shule shikizi za Nyamidege na Nyandote, huku akibainisha kwamba mafuriko hayo yamesababisha kituo cha afya Mohoro kujaa maji na kumekuwa na changamoto ya utoaji wa huduma.
“Hali ni mbaya, tumepata athari kubwa sana kutoka Bwawa la Nyerere, (mafuriko) yameharibu miundombinu kama barabara na madaraja. Mazao yamefunikwa, mifugo imepotea, mingine imekufa, wananchi wetu wameachwa bila makazi,” amesema Chobo.
Mwenyekiti huyo alisema Desemba 1 mwaka jana kuna mkataba ulisainiwa wa ujenzi wa daraja la Bibi Titi katika Kata ya Mohoro lenye thamani ya Sh11.2 bilioni, lakini kwa hali ilivyo haiwezekani.
“Tunaiomba Serikali kuangalia hali hii, kama mashamba ya mahindi, matikiti, ufuta na mazao mengine yameharibika, wananchi wanakosa huduma za kijamii kama afya, lakini mafuriko haya hayawezi kumalizika, kwani yanasababishwa na hili bwawa,” amesema.
Alisema Waziri wa Tamisemi, (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Mohamed Mchengerwa aliagiza Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) kufika kuangalia kama mchoro wa awali unaweza kuendelea vilevile au ubadilishwe.
Mchengerwa awafariji
Juzi, Waziri Mchengerwa ambaye ni Mbunge wa Rufiji aliwatembelea wathirika wa mafuriko hayo na kutoa Sh40 milioni ili kusaidia ununuzi wa mbegu.
Alisema fedha hizo alizidunduliza kutoka kwenye mshahara wake kwa ajili ya kuandaa futari ya pamoja katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kama anavyofanya kila mwaka.
"Kwa hali hii ya mafuriko niseme tu kwamba futari si kitu, nalazimika kuitoa kwa ajili ya ununuzi wa mbegu na nitakwenda kuwaomba marafiki zangu wanichangie angalau tufikishe Sh100 milioni kwa ajili ya kuwasaidia wana Rufiji walioathirika na mafuriko.
“Tulitegemea tunajenga Bwawa la Nyerere tutakuwa tumeondokana na mafuriko, kumbe tuna kila sababu ya kujipanga vizuri, kwa sababu mafuriko yataendelea kuwepo. Mimi kama mbunge wenu nitaendelea kuwa nanyi, kwani nisingefika hapa nilipo bila ninyi,” alisema Waziri Mchengerwa.
Kwa upande wake, Meja Gowele alisema tathmini ya awali imebaini kuharibiwa kwa nyumba 58 na jumla ya wakazi 951 waliokuwa wakiishi kwenye maeneo ya vitongoji vya Kanga na Kiegele, Kilindi na Nyandote katika Kata ya Chumbi wameondolewa katika maeneo yao na kuhamishiwa sehemu salama.
Alisema Rufiji ni bonde na mara kwa mara yanatokea mafuriko na yanapokwisha watu wanarudi, akitolea mfano ya mwaka 2020.
Hata hivyo, alisema wameendelea kutoa tahadhari watu waondoke.
ACT-Wazalendo yatia mguu
Waziri Mkuu kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaki Mchinjita ametoa taarifa kwa umma jana akisema Serikali inapaswa kufanya tathmini ya athari na kuwalipa fidia waathirika hao.