Saba kutoa ushahidi, vielelezo vinne kesi ya bangi

Muktasari:
- Mshtakiwa anadaiwa kusafirisha bangi hiyo Februari 25, 2021 eneo la Kurasani Kijiji cha Wavuvi, kilichopo Temeke.
Dar es Salaam. Vielelezo vinne pamoja na mashahidi saba wanatarajia kutoa ushahidi wao katika kesi ya kusafirisha bangi inayomkabili mshtakiwa, Frank Mwita.
Mashahidi hao wa anatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi.
Hatua hiyo, inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali (PH).
Hayo yameeleza leo Novemba 14, 2023 na Wakili wa Serikali, Winiwa Samson mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo yake.
Wakili Samson alimkumbusha mashtaka yake kwa kuwasomea upya.
Alidai katika shtaka la kwanza ambalo ni la kusafirisha dawa za kulevya, Mwita ambaye ni dereva anadaiwa Februari 25, 2021 eneo la Kurasani Kijiji cha Wavuvi, wilayani ya Temeke, alikutwa akisafirisha kilo 419 za bangi.
Shtaka la pili, siku na eneo hilo, alisafirisha bangi kilo 19.61 na shtaka la tatu alisafirisha kilo 6.63 na shtaka la nne, anadaiwa kusafirisha bangi kilo 6.09.
Maelezo yake
Akimsomea hoja za awali, Wakili Samson alidai kuwa siku hiyo ya tukio mshtakiwa alikutwa akiwa na viroba 24 vya bangi vikiwa nyumbani kwake.
Alidai kati ya viroba hiyo, kiroba kimoja lilikuwa na mbegu za bangi wakati mifuko mingine ikiwa imejaa misokoto ya bangi.
Aliendelea kudaiwa kuwa mshtakiwa alipokamatwa alipelekwa kituo cha Polisi cha Chang'ombe.
Alidia wakati akihojia katika kituo hicho, mshtakiwa alikiri kuvuta bangi na kuuza bangi na kweli alikutwa akiwa na viroba hivyo.
Mwita alidai bangi hiyo alikuwa anainunua kidogo kidogo kwa mtu aliyemtaja kama Manywele na wengine kutoka mkoani Mara na alikuwa anaisafirisha kwa kutumia lori.
Alidai kuwa kiroba kimoja alikuwa anainunua Sh300, 000 huku msokoto mmoja alikuwa anauza Sh3, 000 na kwamba kazi hiyo ya kuuza bangi anaifanya kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, Hakimu Kyaruzi alimuuliza mshtakiwa kama anachochote cha kusema.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alisema analo la kusema lakini atalisema atakapofika Mahakama Kuu.
"Mheshimiwa hakimu ninalo la kusema ila kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina Mamlaka ya kusikiliza shauri hili, nitayasema nitakapofika Mahakama Kuu," alisema Mshtakiwa Mwita.
Baada ya maelezo hayo, mshtakiwa amerudishwa rumande akisubiri kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza kusikiliza kesi hiyo Mahakama Kuu.