Ruto kuapishwa Septemba 13

Rais mteule wa Kenya, William Ruto
Muktasari:
Mahakama ya Juu nchini Kenya imetupilia mbali maombi ya kikatiba yalifunguliwa wiki iliyopita na mgombea aliyeshindwa, Raila Odinga kupinga ushindi wa Rais Mteule, William Ruto.
Dar es Salaam. Rais mteule wa Kenya, William Ruto ataapishwa Jumanne Septemba 13, 2022.
Hiyo ni baada ya Mahakama ya Juu nchini Kenya kutupilia mbali maombi ya kikatiba yalifunguliwa na Raila Odinga kupinga ushindi wa Ruto.
Akitoa uamuzi huo leo Jumatatu Septemba 5, 2022, Jaji Mkuu Martha Koome amesema Raila na waleta maombi wenzake wameshindwa kuthibitisha kuwa kulikuwa na udanganyifu na uchakachuaji wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi, siku na baada ya kupiga kura.
Odinga (77), mwanasiasa mkongwe ambaye aligombea huku akiungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta amepinga matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9, akiyaita ‘upotoshaji.’
Alishindwa na Ruto kwa kura 230,000 tu chini ya asilimia mbili tu alizohitaji
Uamuzi huo unamfanya Ruto kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya kufuatia uchaguzi uliokuwa na upinzani mkali.
“Uchaguzi ulikuwa halali na ulifanyika kwa namna huru na wa haki. Hakuna ushahidi wa kuonesha Fomu namba 34 ilingiliwa kwa namna yoyote wakati wa kuzipakia kwenye tovuti ya tume ya uchaguzi,” alisema Jaji Koome katika hukumu aliyoisoma kwa karibu saa mbili.
Katika matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati Agosti 15, 2022, Dk William Ruto alishinda kwa kura 7,176,142 (asilimia 50.49 ya kura) na Raila Odinga akafuatiwa kwa kura 6, 942, 930 (asilimia 48.85). wangombea wengine wawili hawakufikisha asilimia moja ambapo David Waihiga alipata asilimia 0.23 % huku George Wajackoyah akipata asilimia 0. 44.