Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rufaa yamwepusha na kitanzi aliyehukumiwa kunyongwa

Muktasari:

  • Emanuel Ndunguru alishtakiwa na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kumuua dereva bodaboda kisha kutelekeza mwili wake ambao ulikutwa umefungwa shingoni na waya, miguu ikiwa imefungwa na kamba ya mkonge huku mikono ikiwa imefungwa na kitambaa.

Arusha. Mahakama ya Rufaa Tanzania imemwachia huru Emmanuel Ndunguru aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya aliyekuwa dereva bodaboda, Nemes Shomari.

Ilielezwa kuwa  mwili wa Shomari baada ya kuuawa, ulikutwa ukiwa umeanza kuoza huku shingo yake ikiwa imefungwa waya na miguu imefungwa kamba ya mkonge na mikono ikiwa imefungwa na kitambaa kwa nyuma.

Inaelezwa kituo chake cha kazi kilikuwa eneo la Mgeninani, wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam na siku ya tukio Mei 4,2016 Emmanuel alimpigia simu Mariam Mfaume (shahidi wa pili ambaye pia alikuwa mpenzi wake).

Inadaiwa kuwa Emmanuel alimwomba Mariam amtafutie pikipiki ya kukodi kutoka Keko, Dar es Salaam, hadi Kibaha Pwani kwa malipo ya Sh50,000.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimuhukumu Emmanuel kwa kosa la mauaji Machi 17, 2023 adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Hata hivyo, Machi 28, 2025, Mahakama ya Rufaa ilitoa hukumu iliyomwachia huru Emmanuel.

Jopo la majaji watatu akiwamo Barke Sehel, Amour Khamis na Ubena Agatho, lilifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi, kusikiliza hoja za pande zote na kubaini kuwa ushahidi uliomtia hatiani ulikuwa dhaifu.

Ilivyokuwa

Ushahidi wa mashtaka ulieleza Mei 5, 2016, shahidi wa pili alipokea ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa Emmanuel ukieleza kuwa walirejea salama kutoka safari yao.

Mariam alisema  kuwa baadaye watu wawili, dereva bodaboda na mwajiri wa Nemes walifika nyumbani kwake na kumweleza kuwa yeye ndiye mtu wa mwisho kuonekana na Nemes, ambaye hadi wakati huo hakuwa amepatikana.

Shahidi huyo alieleza kuwa aliyemkodi alikuwa Emmanuel, ambaye alimtumia ujumbe kuwa walirejea salama.

Hata hivyo, kutokana na mashaka kuhusu maelezo hayo, Mariam alichukuliwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Kijichi na baadaye Kituo cha Polisi Maturubai kwa maelezo zaidi.

Shahidi wa tatu, Sajenti Salehe, Ofisa Mpelelezi kutoka Kituo cha Polisi Kibaha, alieleza kuwa alikabidhiwa jalada la uchunguzi na alifika eneo la tukio, ambako mwili wa mwanaume ulikutwa umefungwa shingoni na miguuni kwa kamba ya mkonge, huku mikono ikiwa imefungwa kwa kipande cha kitambaa kwa nyuma.

Alisema kuwa mwili huo ulipelekwa Hospitali ya Tumbi kwa uchunguzi. Lakini Machi 7, 2016, ndugu wa marehemu, Avelin Charles na Shangwe Mhene, walifika Kituo cha Polisi Kibaha na baadaye Hospitali ya Tumbi, ambako walishuhudia uchunguzi wa mwili wa marehemu.

Emmanuel alikamatwa Agosti 16, 2016, na kufikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.

Utetezi

Katika utetezi wake, Emmanuel alikana kuwa na uhusiano wa kimapenzi na shahidi wa pili na pia alikana kumtuma amtafutie bodaboda.

Alisema kuwa alikamatwa Temeke kwa Aziz Ally na baadaye kupelekwa rumande Kituo cha Polisi Mbagala huku akisisitiza kuwa shitaka la mauaji lilitungwa katika Kituo cha Polisi Kibaha.

Wakitoa kauli yao, wazee wa baraza walitoa maoni kuwa Emmanuel hakuwa na hatia, kwa kuwa shahidi wa pili alishindwa hata kutaja namba ya simu ya Emmanuel iliyotumika katika mawasiliano yao.

Hata hivyo, jaji aliyesikiliza kesi hiyo alitofautiana na maoni ya wazee hao wa baraza, akamkuta na hatia ya mauaji na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.


Rufaa

Katika rufaa hiyo, Emmanuel aliwasilisha sababu 11 za kupinga hukumu ambazo ni pamoja na ya kwamba jaji alikosea kisheria kumtia hatiani kwa msingi wa ushahidi wa kimazingira uliotolewa.

Lakini pia amesema ushahidi wa shahidi wa pili ulikuwa dhaifu na haukutosha kuaminika.

Pia amesema kamba na nguo zilizodaiwa kukutwa kwenye mwili wa marehemu hazikuwasilishwa mahakamani kama ushahidi na  utetezi wake haukuzingatiwa ipasavyo.

Amesema upande wa mashitaka haukuthibitisha kosa hilo kwa kiwango kinachohitajika kisheria.

Katika rufaa hiyo, Emmanuel alitetewa na Wakili Musa Mhagama, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Baraka Mgaya.

Wakili Mgaya aliunga mkono rufaa hiyo, akieleza kuwa kosa hilo halikuthibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Alikiri kuwa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaomuunganisha Emmanuel na kifo hicho, isipokuwa maelezo ya shahidi wa pili pekee ambayo hayakuthibitishwa, hata madai ya mawasiliano kati yao hayakuthibitishwa.

Uamuzi wa majaji

Jaji Barke Sehel alisema baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili, suala la msingi lililozingatiwa katika uamuzi wao lilikuwa iwapo hukumu ya kesi hiyo ya mauaji inaungwa mkono na ushahidi wa kimazingira wa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu akiwa hai.

Akirejelea hukumu ya rufaa ya jinai namba 207 ya mwaka 2009 ya Sadiki Mkindi dhidi ya DPP, Mahakama ya Rufaa iliweka kanuni za jumla kuhusu ushahidi wa kimazingira.

"Kwa hiyo, kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana na marehemu akiwa hai si lazima yenyewe ipeleke kwenye hitimisho kwamba mtuhumiwa alitenda kosa. Badala yake, inanyoosha kidole kwa hatia ya mtuhumiwa, lakini bado upande wa mashitaka unabeba mzigo wa kuthibitisha ukweli wa hatia na mazingira yanayomuhusisha mshtakiwa na uhalifu," alisema Jaji Sehel.

Alifafanua kuwa katika rufaa hiyo, Emmanuel alipatikana na hatia kwa msingi wa ushahidi wa shahidi wa pili, ambaye alijaribu kumuhusisha na mauaji hayo kwa kudai kuwa alimwagiza kumtafutia pikipiki ya kukodi kutoka Keko hadi Kibaha.

Hata hivyo, baada ya kutathmini upya ushahidi uliopo kwenye rekodi, jopo la majaji halikuona ushahidi wowote unaomuhusisha moja kwa moja Emmanuel na kifo cha marehemu, isipokuwa maelezo ya shahidi wa pili pekee.

"Hakukuwa na shahidi aliyemwona mrufani akipanda pikipiki ya marehemu, na tunaamini kwamba mlolongo wa mazingira ulioelezwa na shahidi wa pili haukuwa kamili vya kutosha kuendeleza hukumu dhidi ya mrufani," alisema Jaji Sehel.

Akiendelea, alieleza kuwa ni jambo la kusikitisha kwamba mahakama ya awali ilimuhusisha mrufani na kifo cha marehemu kwa misingi ya maelezo yasiyokuwa na uthibitisho wa kutosha, wakati ambapo upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha mazingira yote yanayomuunganisha na kifo hicho.

"Tunakubaliana na hoja za mawakili wa pande zote kuwa ushahidi uliomtia hatiani mrufani ulikuwa dhaifu kwani ulitegemea maneno pekee ambayo hayakuthibitishwa. Kwa msingi huo, tunafuta hukumu iliyotolewa dhidi ya mrufani na tunatoa agizo kwamba aachiliwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine," alihitimisha Jaji Sehel.