Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rostam: Hakuna mgeni atakayeijenga nchi yako, tuwarejeshe wataalamu walio nje

Muktasari:

  • Mfanyabiashara, Rostam Azizi ametaka uwezeshwaji zaidi kwa sekta binafsi ya ndani ili kukuza uwezo, kwa kuwa ndiyo nyenzo itakayojenga uchumi nchini.

Dar es Salaam. Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kuvutia wawekezaji kutoka nje, mfanyabiashara Rostam Aziz, amesema ni muhimu kutungwa sera na sheria zinazowabeba na kuwapendelea wafanyabiashara wa ndani, kwa kuwa, ndio watakaoijenga nchi.

Amelisisitiza hilo, akisema duniani hakuna nchi iliyojengwa na wageni, hivyo kunapaswa kuwa na mabadiliko ya sekta ya kifedha kuwafanya wafanyabiashara wa Tanzania wapate mitaji ya kutosha kuwekeza.

Ameambatanisha hoja hiyo akirejea katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisema Tanzania ni hodari wa kupanga, lakini inasuasua katika utekelezaji, hivyo ni muhimu ibadilike na kuwa mtekelezaji mzuri.

Mfanyabiashara huyo amesema hayo leo, Alhamisi Julai 17, 2025 alipowasilisha salamu za sekta binafsi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, itakayoanza kutekelezwa Julai 1, 2026.

Uzinduzi wa Dira 2050 unafanywa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Rostam ametaka Serikali iweke mkakati maalumu wa kulinda na kuijenga sekta binafsi ya ndani na ifanye hivyo ikitambua ni muhimu kuendelea kuwavutia wawekezaji wa nje.

“Tunapongeza kazi kubwa iliyofanyika katika kuwavutia wawekezaji waje kuwekeza kwenye nchi yetu lakini Watanzania ndiyo watakaoijenga nchi yao, hivyo ni lazima wawekezaji wa ndani wapewe fursa na kulindwa,” amesema.

Rostam amesema viwanda vya ndani vinapaswa kulindwa, kwa kuwa,  hakuna nchi iliyofanikiwa kuujenga uchumi wake bila kuwa na viwanda.

“Hakuna nchi duniani inayojengwa na wageni, ni Watanzania ndiyo watafanikisha dira hii, sera na sheria zitungwe kuwabeba kibiashara, manunuzi na zabuni za Serikali ziwapendelee Watanzania kwa makusudi bila woga,” ameeleza.

Ametaka kuwepo mabadiliko ya sekta ya kifedha ili wafanyabiashara wa Kitanzania wapate mitaji ya kutosha kuwekeza.

“Mifumo yetu ya kibenki tuliyonayo kwa sasa hairuhusu mfanyabiashara wa Kitanzania kukua, tukirekebisha haya; SGR, bwawa la Nyerere na barabara zote hizo mnazoziona zingeweza kujengwa na kampuni za Kitanzania,” amesema.

Ametolea mfano imetumika Sh30 trilioni katika ujenzi, kwa miaka 15 ingekuwaje fedha hizo zingebaki nchini, maana yake uchumi ungekuwa na sura kubwa.

“Tukiweza kurekebisha hayo, fedha ambazo zitapatikana katika hizi zabuni zitabaki hapa nchini na kuendeleza nchi yetu,” amesema.

Sambamba na hayo, amesema wakati nchi inajipanga na ngwe mpya ya mageuzi ya kiuchumi yanayoongozwa na maarifa na ubunifu, ni muhimu kuwa na hekima katika kuhakikisha kunakuwa na amani na utulivu.

“Amani inaendana na taasisi imara, sera thabiti na uongozi unaoweza kuelekeza vipaji katika mstari mmoja wa maendeleo ya Taifa, ni katika mazingira haya ndipo mipango ya muda mrefu inaweza kutekelezwa kwa ufanisi,” amesema.


Uwekezaji kwa vijana

Amesema ili Tanzania ipige hatua haraka ni muhimu kuwekeza katika rasilimali watu hasa vijana, huku akisisitiza kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo wa vipaji utakaokuwa na bajeti ya takribani Dola 100 milioni za Marekani.

“Hatua ya kwanza ni kuanzisha mfuko wa maendeleo ya vipaji wenye bajeti ya takribani Dola milioni 100 kila mwaka,” amesema.

Kupitia mpango huo, amesema vijana takribanI 1,000 wenye uwezo wa nyanja mbalimbali ikiwamo uhandisi, akili unde na sayansi ya takwimu, watatambuliwa na kulelewa ili kuleta maendeleo.

Rostam amesema Tanzania ni hodari wa kupanga, lakini katika utekelezaji inasuasua, hivyo sekta binafsi ingependa kuona mabadiliko.

“Sisi kama sekta binafsi tungependa kuona tunabadilika na safari hii tutekeleze kweli,” amesema.

Amesema vijana hao wanapaswa kupewa mafunzo katika vyuo vikuu vinavyoongoza duniani, watakapomaliza watarejea nchini na kuhudumu katika tume ya mipango na taasisi nyingine za Serikali.

Mpango huo, amesema si wa masomo tu bali ni uwekezaji wa kimkakati katika uelekeo wa Taifa.

Wakati vijana hao wakiwa huko, amesema Tanzania inapaswa kuimarisha vyuo vyake, kuhakikisha vina uwezo wa kuzalisha watalaamu wa viwango vya kimataifa.

“Hili linawezekana kwa kuboresha mitalaa iliyopo, kuimarisha utafiti na kuhakikisha sekta ya elimu imeandaliwa kwa mahitaji ya uchumi wa kisasa,” amesema.

Kwa upande wa viongozi, amesema ni muhimu kuwaendeleza hasa waliopo kwenye taasisi mbalimbali kwa kuwapa fursa ya kushiriki katika programu za uongozi za kimataifa ili kuwajengea uwezo wa kuongoza katika mazingira mapya.

“Kama hatua ya dharura tunapendekeza balozi zetu ziwe na jukumu maalumu la kuwatambua na kuwarudisha nyumbani Watanzania wanaosomea au wanaofanya kazi nje ya nchi katika nyanja hizi muhimu,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Susan Namondo amesema Tanzania imefanikiwa kukuza uchumi wake na kufikia hatua ya uchumi wa kati na kupunguza vifo vya uzazi, huku idadi ya watoto wanaojiunga na shule za msingi na sekondari imeongezeka.

Amesema Tanzania imefanikiwa kuwa na usalama wa chakula na hatua nyingine muhimu zimepigwa katika wakati ambao dira mpya inaandaliwa.

Katika hotuba yake hiyo, amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mipango iliyowekwa na kwamba watajitahidi kusaidia kupitia ushirikiano na hata kifedha.


Endelea kufuatilia Mwananchi