REA yapambana kusambaza umeme Kilimanjaro

Muktasari:
- Vijiji 11 na vitongoji 359 havijafikiwa na huduma ya umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Moshi. Serikali kupitia Wakala wa Nishati vijiji (REA) imetumia zaidi ya Sh90 bilioni, kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye vijiji 502 na vitongoji 1,901 mkoani Kilimanjaro.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka wakala wa nishati vijijini, James Olotu wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi katika ziara ya uongozi na wabia wa maendeleo mkoani Kilimanjaro.
Olotu amesema mpaka sasa vijiji 11 na vitongoji 359 havijapatiwa huduma ya umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba jitihada za kusambaza umeme maeneo hayo zinaendelea na hadi kufikia mwaka 2025.
"Katika Mkoa wa Kilimanjaro Kata zote 148 sawa na asilimia 100 zimefikiwa na miundombinu ya umeme, vijiji 502 kati ya 513 sawa na asilimia 98 na vitongoji 1,901 kati ya 2,260 sawa na asilimia 84 vimefikiwa na miundombinu ya umeme," amesema.
Aidha, amesema Vijiji 11 ambavyo havina umeme vitapatiwa huduma hiyo kupitia mradi wa REA III mzunguko wa pili, ambapo amesema REA ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi katika mkoa huo Juni mwaka huu.
"Vitongoji 359 ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme, vitapatiwa umeme kupitia mradi wa Densification III ambapo kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na hadi ifikapo mwaka 2025, vitongoji vyote vitakuwa vimefikiwa."
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Francis Songela amesema wameridhika na namna ya utekelezaji wa mradi huo kwani umechangia kwa kiasi kikubwa kuchochea maendeleo ya wananchi maeneo ya vijijini.
Naye Daniel Tiveau, kutoka ubalozi wa Sweden amesema wamekuwa wakisaidia miradi ya nishati kwa miaka mingi na katika ziara waliyoifanya, wamebaini kuwepo kwa matumizi ya umeme kwa maendeleo kwa kiasi kikubwa.
"Lengo letu tulitegemea umeme umkomboe mwananchi kiuchumi na tumefarijika kuona hilo limefanikiwa. Pia tumeona mahitaji ya nishati ya umeme bado ni makubwa, hivyo tuombe wananchi wawe wavumilivu wakati mipango mingine inaendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo," amesema.
Baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro wamesema kufika kwa umeme vijijini kumepanua wigo wa maendeleo na kupunguza matukio ya uhalifu yaliyokuwa yakichangiwa na uwepo wa giza nene.
Mwanaidi Omary, Mkazi wa Shabaha Wilaya ya Moshi, amesema umeme umekuwa chachu kubwa ya maendeleo katika maeneo yao, ambapo wameweza kutumia umeme kuanzisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kujikwamua kiuchumi.
"Tulikuwa tunanyanyasika na vibatari ambavyo viliwafanya wanafunzi pia wateseke kwenye kusoma, lakini leo umeme umefika, vijana wameanzisha miradi yao midogo midogo ya kuwawezesha kujikwamua kiuchumi,” amesema.