Mvua yakata mawasiliano barabara ya Ifakara–Mlimba

Muktasari:
- Barabara hiyo ya Ifakara–Mlimba iko chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), na tayari wataalamu wanaelekea eneo hilo kwa ajili ya matengenezo.
Mlimba. Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo huko Mlimba imesababisha kukatika kwa barabara ya Ifakara–Mlimba kwenye maeneo mawili, hivyo kukata mawasiliano wilayani humo.
Barabara hiyo imekatika kwenye eneo la Kijiji cha Ngwasi na Kalengakelu, Halmashauri ya Mlimba, na kwamba mvua kubwa inayoendelea kunyesha wilayani humo imesababisha maeneo mengi kuharibika.

Akizungumza na Mwananchi, Diwani wa Kalengakelu, Matha Mkula, amesema barabara hiyo imekatika usiku wa kuamkia leo baada ya kunyesha mvua kubwa iliyoanza saa saba usiku hadi alfajiri.
"Hili eneo la Kalengakelu, barabara imekatika upande mmoja na hivyo kubaki sehemu nyembamba ambayo watu wamekuwa wakiendelea kupita kwa tahadhari kubwa. Lakini hili eneo la Ngwasi maji yamesomba karavati na kusababisha barabara kugeuka mto, na mpaka sasa maji ni mengi na yanakasi kubwa," amesema Mkula.

Diwani huyo amesema kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, wananchi wamekuwa wakivushwa kwa kubebwa mgongoni na vijana na mgambo. Hata hivyo, hali ya hewa bado ni mbaya na maji yamekuwa yakipungua na kuongezeka mara kwa mara.
"Hili eneo la Ngwasi sio mara ya kwanza kuharibiwa na mvua, hii ni mara ya tatu katika kipindi cha mwaka mmoja. Walishakuja viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri na palitengenezwa, lakini bado hapajapata suluhisho la kudumu," amesema Mkula.

Naye Bundo Level, Katibu wa mbunge wa Mlimba, amesema tayari mbunge ameshapata taarifa za changamoto hiyo na jitihada za kurekebisha eneo hilo zinaendelea.
"Taarifa nilizonazo, tayari wataalamu wetu wa Tanroads wameshapata taarifa na muda wowote kuanzia sasa watafika na kuona namna ya kurekebisha maeneo hayo mawili, ambayo yapo kwenye kata moja ya Kalengakelu. Tunatambua barabara hii ni muhimu kiuchumi, lakini pia kijamii," amesema Level.