Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mafuriko yakata mawasiliano Ulanga - Malinyi

Muktasari:

  • Baada ya barabara hiyo kukatika wananchi sasa wanavuka kwa kubebwa mgongoni kwa malipo ya Sh2,000 na kwa kutumia bodaboda ambayo ni Sh5,000.

Ulanga. Mvua za masika zinazoendelea kunyesha zimesababisha kukatika kwa barabara ya Ulanga -Malinyi baada ya mto Namuhanga kufurika na karavati lake kubwa kusombwa na maji eneo la Ilagua, hivyo kufanya barabara hiyo kushindwa kupitika kuanzia Mei 4 usiku hadi leo hii Mei 5, 2025.

Barabara hiyo hadi sasa haipitiki na kufanya wananchi kuteseka na kutumia gharama kubwa ikiwamo kuvushwa kwa kubebwa mgongoni kwa Sh2,000 au kwa kutumia bodaboda ambayo ni Sh5,000 ambapo kazi hiyo imekuwa ikifanywa na vijana ambao wamegeza changamoto hiyo kama fursa ya kujipatia fedha.

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wananchi wamesema eneo hilo limekatika baada ya mto kujaa na kupoteza uelekeo wake, hivyo kusomba karavati linalounganisha barabara hiyo.

Wananchi wakiwemo wasafiri wakiangalia namna barabara ya Ulanga - Malinyi ilivyokatika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha juzi Mei 3 Wilayani humo na kusababisha makaravati yaliyokuwepo eneo hilo kusombwa na maji. Picha Hamida Shariff

Mmoja wa wananchi hao Feruzi Mohamed ameiomba Serikali kumaliza tatizo hilo kwa kuwatengenezea barabara ya kudumu ya kiwango cha lami na kuweka madaraja makubwa, badala ya kuweka mkaravati ambayo yamekuwa yalisombwa mara kwa mara.

Naye Stanislaus Lichombe amesema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa wilaya ya Ulanga, Malinyi na Kilombero kwa kuwa wilaya hizo zimekuwa ni wazalishaji wakubwa wa mpunga ambao husafirishwa mikoa mbalimbali na hata nje ya nchi.

Amesema kipindi cha mvua barabara hiyo imekuwa ikikatika mara kwa mara na kusababisha adha kwa wananchi, hivyo Serikali inapaswa kutatua changamoto hiyo Kwa kutafuta suluhisho la kudumu.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Simba amethibitisha kukatika kwa barabara hiyo akiahidi kuwa jitihada za kurejesha mawasiliano zinaendelea.

"Ni kweli barabara imekatika katika kata ya Ilagua kijiji cha Namuhanga ambapo barabara hii inaunganisha wilaya ya Ulanga na Malinyi, mpaka sasa hakuna gari inayoweza kupita eneo hilo kwa sababu sehemu ya barabara imesombwa na maji," amesema Simba.

"Maji bado ni mengi na mvua bado zinaendelea kunyesha, kama yatapungua wakati wowote kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo itaanza, niwaombe wananchi wawe na subira na uvumilivu wakati Serikali ikihangaika kufanya matengenezo katika eneo hilo.," amesema Simba.

Wiki mbili zilizopita Waziri wa Ujenzi, Abdalah Ulega akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,  Adamu Malima alifika wilayani Malinyi kufuatia barabara ya Ifakara - Malinyi kukatika eneo la Misegese baada ya karavati kusombwa na maji.

Katika ziara yake hiyo Ulega alisema Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2025-2026 imetengea Sh18 bilioni kwa ajili ya madaraja mawili ya Misegese kuelekea Malinyi mjini na daraja la kivuko cha mto Mnyera kuelekea Halmashauri ya Mlimba wilayani Kilombero.

Aidha Waziri Ulega alisema Serikali imepanga kutengeneza barabara kilomita 110 kuanzia Lupiro wilayani Ulanga hadi Malinyi mjini kwa kiwango cha lami na kilomita 50 za kiwango cha lami wilayani Ulanga.

Alisema Serikali imeshamwingizia mkandarasi fedha tayari na kinachosubiriwa kwa sasa ni kupisha mvua za masika zinazoendelea kunyesha.