RC Batilda akerwa utoro wa watumishi kazini, atoa agizo

Muktasari:
- Walioapishwa ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Ayubu Sebabile na Salum Nyamwese wa Wilaya ya Handeni walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Juni 23, mwaka huu.
Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amepiga marufuku uombaji wa ruhusa usio na lazima kwa watumishi wa Serikali wakiwamo wakuu wa wilaya, na badala yake wafanye kazi kama walivyoahidi kwenye viapo vyao katika kutatua kero za wananchi.
Akizungumza wakati wa kuwaapisha wakuu wa wilaya ya Muheza Ayubu Sebabile na Salum Nyamwese wa Wilaya ya Handeni leo Jumatatu Juni 30, 2025 Balozi Batilda amesema sio sawa kuomba ruhusu bila sababu maalumu.
Amesema kuna baadhi ya watumishi wanaomba ruhusa kuwa wanaumwa, ila baadaye anakutwa kwenye viwanja vya mpira au matukio mengine tofauti na alichokisema jambo ambalo sio sahihi na kinyume na maadili.
Balozi Batilda amewataka wakuu hao wa wilaya kuhakikisha wanakwenda kutatua migogoro mbalimbali iliyopo kwenye maeneo yao, ikiwemo ya ardhi kwani ni moja ya sababu ya uvunjifu wa amani.
Kuhusu kukusanya mapato amesema ni jambo muhimu kwani wakuu wa wilaya ndio wenyeviti wa baadhi ya kamati za mambo ya makusanyo.
Pia ameagiza kufufuliwa shughuli za kilimo hasa minazi, kokoa na migomba na kila kaya inatakiwa kupanda migomba 10, shughuli ambayo itaweza kunyanyua uchumi wa wananchi hasa Wilaya ya Muheza.
Amesema wahakikishe wanakuwa na siku maalumu rafiki ya kusikiliza kero za wananchi na kutatuliwa kwa wakati.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Rashid Mchata aliyehamishwa kutoka Mkoa wa Pwani amewaomba watumishi kumpa ushirikiano katika ofisi yake, kwani wote wanajenga nyumba moja.
Sebabile amesema kipaumbele cha kwanza ambacho anakwenda kufanyia kazi ni changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika la machungwa katika wilaya hiyo, na maagizo mengine yaliyotolewa na Serikali.
Aidha, Salum Nyamwese amesema wilaya hiyo ni ya kimkakati hivyo atakwenda kuangalia watanyanyua vipi shughuli za kiuchumi, ikiwemo suala la viwanda na uchimbaji wa madini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alifanya uhamisho na mabadiliko ya uteuzi wa viongozi mbalimbali Juni 23, 2025.