Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Stubb apigia chapuo ubunifu

Rais wa Finland Alexander Stubb wa kwanza kulia akizungumza na wabunifu wadogo leo Mei 15, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa JNICC jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Rais wa Finland, Alexander Stubb, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kurejea upya dhana ya ubunifu, akisisitiza kuwa ubunifu haupaswi kuangaliwa kama suala la kiteknolojia pekee bali kama chombo chenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kijamii.

Akizungumza leo Alhamisi Mei 15, 2025 jijini Dar es Salaam, katika Wiki ya Ubunifu, Rais Stubb amesema ubunifu unapaswa kuchukuliwa kwa upana zaidi, kwani maendeleo ya teknolojia kama vile akili bandia (AI) yanaonesha jinsi mabadiliko yanavyotokea kwa kasi.

Stubb amesema kuwa pamoja na changamoto hizo, ubunifu hutoa fursa mpya, kazi fulani huweza kutoweka, lakini nyingine huibuka.

Katika hafla hiyo, Serikali ya Finland ikishirikiana na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), ilisaini makubaliano ya msaada wa Sh6.3 bilioni kwa ajili ya kuendeleza ubunifu katika sekta ya misitu kupitia mradi wa Green Catalyst.

Mradi huo unalenga kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu, uhifadhi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini.

Rais Stubb amependekeza njia tatu za kuimarisha ekosistemi ya ubunifu: kuweka kanuni na malengo wazi, kuwekeza kwenye mawazo mapya hata kama hayana faida ya haraka, na kuunga mkono mchakato wa ubunifu kwa upana.

Amezitaka serikali kutengeneza mazingira wezeshi badala ya kujaribu kuchagua nani anastahili kufanikiwa katika soko.

“Huwezi kutegemea sheria au fedha pekee,” alisema na kuongeza kuwa “unahitaji mawazo mapya na mazingira wezeshi kwa ujasiriamali kustawi.”

Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP, John Rutere, amesema Green Catalyst ni fursa ya kipekee ya kukuza ubunifu na ujasiriamali wa sekta ya misitu. “Si kila siku tunamwona Rais wa taifa akihusika moja kwa moja kwenye juhudi kama hizi,” alisema.

Mkurugenzi wa Ubora Forest Solution, Daudi Kilonzo, amesema anafarijika kuona programu kama FUNGUO zikileta mchango mkubwa kwa wabunifu chipukizi nchini kwa kubadilisha mawazo kuwa biashara zenye tija.

Awali, Rais Stubb alikutana na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan ambapo walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo misitu, biashara, uwekezaji, madini, utalii, elimu, uwezeshaji wanawake, TEHAMA, na uhamilishaji teknolojia.

Rais Samia alisema wameikaribisha Finland kuungana na mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, lengo likiwa ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2030.

“Sote tulikubaliana kuwa kuna fursa ya kukuza ushirikiano katika maeneo hayo na tukaeleza utayari wetu kutumia fursa hizi kwa manufaa ya mataifa yetu,” amesema Rais Samia wakati wa mkutano wao na vyombo vya habari.

Rais Samia amebainisha kwamba kwenye mazungumzo yao walikubaliana kuongeza maeneo mengine ya ushirikiano hasa yale  muhimu kama vile uchumi wa buluu, nishati na elimu kwa manufaa ya watu wao.

Kwa upande wake, Rais Stubb alisema Tanzania ina nafasi maalum katika mioyo ya raia wa Finland na ziara yake inalenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Amesema wanaamini katika usawa, ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na Tanzania imekuwa na sehemu kubwa kwenye mioyo ya raia wa Finland.