Rais Samia na mkakati wa kuifanya Tanga kuwa ufunguo wa uchumi

Muktasari:
- Mkakati wa kuifungua Tanga, kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, unaanzia wilayani Pangani, ambako unatekelezwa mradi wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo (Makurunge)-Mkange-Pangani-Tanga yenye urefu wa kilomita 256.
Pangani. Rais Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Serikali ni kuunganisha Mkoa wa Tanga na shoroba kadhaa ili kufungua biashara, utalii na hatimaye uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Mkakati wa kuifungua Tanga, kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, unaanzia wilayani Pangani, ambako unatekelezwa mradi wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo (Makurunge)-Mkange-Pangani-Tanga yenye urefu wa kilomita 256.
Mradi huo pia unajumuisha ujenzi wa daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 litakalotekelezwa kwa miezi 36, linalotajwa kuwa mwokozi wa adha zinazowakabili wananchi wa Pangani pale kivuko kinapoharibika.

Kwa ujumla, mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), iliyotoa mkopo wa Sh390.1 bilioni, na Serikali imetoa Sh58.47 bilioni.
Kwa mujibu wa Rais Samia, barabara hiyo, ambayo ni sehemu ya zile za Afrika Mashariki (EAC), inaunganisha Kenya na Tanzania kupitia Ukanda wa Pwani.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Februari 26, 2025, na Rais Samia alipowahutubia wananchi wa Pangani katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Tanga.
Baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo wa daraja na barabara, Rais Samia amesema dhamira yake hasa ni kubadili uchumi wa Pangani.
Mabadiliko ya uchumi wa wilaya hiyo, ameeleza, yatatokana na mradi huo kuiunganisha Tanga na shoroba kadhaa za kiuchumi.
Katika ufafanuzi wake kuhusu mradi huo wa barabara, amesema utaiunganisha Tanga hadi mpaka wa Kenya, kisha Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Ili kutengeneza fursa za kiuchumi kupitia shoroba hizo, Rais Samia amesema Serikali itajenga kongani za viwanda na bandari kubwa katika eneo la Bagamoyo.

"Tunaiunganisha Tanga tena kupitia Pangani. Pangani hii itaunganisha majimbo mengi na moja kwa moja hadi kwenye mpaka wetu na Mombasa na tunaungana na Bandari ya Mombasa," amesema.
Barabara inayojengwa, amesema, inaifungua Tanga kiutalii na kibiashara kwa kuwa maeneo kadhaa ya utalii yasiyofikika, sasa yatakuwa rahisi kufikika kwa barabara hiyo mpya.
Kwa kuwa maeneo hayo ya utalii, hasa Hifadhi ya Saadani, amesema itarahisisha kuwachukua watalii kutoka katika chanzo hicho na kuwapeleka kwenye vivutio vingine.
"Barabara hii itaunganisha Tanga na Pwani ya Afrika Mashariki na hivyo ukitoka Horohoro unapita Tanga, Bagamoyo hadi Dar es Salaam," ameeleza.
Amesisitiza kuwa barabara hiyo inaunganisha Tanzania na maeneo ya Kusini, Mashariki na Magharibi.
"Kwa hiyo kujengwa kwa barabara hii ni kuifungua Tanga ndugu zangu, kuifungua Tanga kiuchumi, kiutalii, kibiashara na mambo mengine yatakuja huko mbele," amesema.

Kwa kuwa Pangani kuna wakulima wa mkonge, mihogo na nazi, amesema barabara hiyo itawezesha usafirishaji wa mazao hayo hadi kuyafikia masoko.
Awali, akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema daraja hilo ni miongoni mwa kazi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Kwa mujibu wa Ulega, urefu wa daraja hilo unalingana na viwanja vitano vya mpira wa miguu na robo.
"Pamoja na daraja hili, zitakuja kilomita 25 za barabara kama maungio ya daraja hili," amesema.
Amesema daraja hilo pia litaambatana na uwekaji wa taa 240 na nyingine 200 zitakazowekwa katika barabara za Wilaya ya Pangani.
Ulega amesema kilomita 2,031 za barabara zinaendelea kujengwa, zikiwemo zinazotoka Bagamoyo-Mkange-Tungamaa-Pangani na Tanga, barabara ambayo ilipigiwa kelele na wabunge mbalimbali.
Ameahidi kuhakikisha wizara hiyo inasimamia kazi usiku na mchana bila kuchoka.
Amesema jambo la kufurahisha ni kwamba wakandarasi wa barabara hiyo hawaidai chochote Serikali, badala yake wao ndio wanadaiwa.
"Wizara ya Ujenzi ikiwa inamdai mkandarasi, inamwambia asicheke wala asi-relax, afanye kazi usiku na mchana hadi kieleweke. Watanzania waendelee kupata matunda ya uhuru wa nchi yao," amesema.
...agawa boti za uvuvi
Sambamba na hayo, Rais Samia pia amegawa boti 35 za mkopo kwa wavuvi wilayani Pangani, ikiwa ni awamu ya pili.
Amesema boti moja inabeba tani tatu hadi tano za samaki na zinakwenda hadi karibu na bahari kuu.

"Boti zile za zamani hazikuwa zinafika huko, lakini hizi zinafika. Kwa hiyo bila shaka wavuvi wetu wanavuna mazao mengi ya bahari," amesema.
Amewataka wavuvi waliokopeshwa boti hizo, kuzitunza na wasiache kuendelea kulipa mikopo waliyochukua.

"Nimeambiwa mmeanza kulipa vizuri, na wengine, sababu ya kulipa, ndio wameweza kuingia kwenye mkopo wa pili. Niwaombe muendelee kulipa ili twende vizuri," amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji, amesema Sh11.5 bilioni zilitumika kununua boti 160 kwa awamu ya kwanza na kusambazwa katika maeneo yote yenye wavuvi ya ukanda wa Pwani, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, na Ziwa Rukwa.
"Kwa ukanda wa Pwani, tulipeleka boti 88; mkoa wa Tanga ulipata boti 14, Dar es Salaam tano, Lindi 32, Mtwara 18, na Pwani 19. Mheshimiwa Rais (Samia), naomba kusema mradi huu unaendelea vizuri, na hapa Pangani wavuvi wameendelea kunufaika," amesema Dk Kijaji.
Dk Kijaji amesema mradi wa boti za kisasa zinazotolewa na Serikali umesaidia kuwawezesha wavuvi kufanya shughuli zao kwa uhakika na kujiingizia kipato katika maeneo mbalimbali.

Aidha, amesema kuwa baada ya mradi huo kuwa na maendeleo mazuri, waliwasilisha mapendekezo kwa Rais Samia kwamba kwa mwaka 2024/25, Serikali iwaongezee fedha ili kuendelea na uwezeshaji wa boti.
"Mheshimiwa Rais, tunashukuru Serikali ilitupatia tena Sh11.5 bilioni, ambazo zimetumika kununua boti 120. Kwa maelekezo yako, ulituambia tukawatafute wavuvi; kupitia mwaka huu, tutawagusa wavuvi 1,870," amesema.
"Tunakwenda kugusa maisha yao, mifuko yao, pamoja na wanawake na vijana wanaohusika na miradi ya uvuvi. Katika boti 120, 70 zitakwenda ukanda wa Pwani, 29 Ziwa Victoria, wakati 21 zitakwenda Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa," amesema Dk Kijaji.
...kiwanda cha sukari kujengwa Pangani
Katika hotuba yake, Rais Samia pia aligusia mpango wa kujenga kiwanda cha sukari wilayani humo.
Amesema ujenzi wa kiwanda hicho utaambatana na uanzishaji wa shamba kubwa la miwa katika Bonde la Mto Pangani.
Dhamira ya kiwanda hicho, amesema, ni kuiwezesha nchi kujitosheleza kwa bidhaa ya sukari, hasa ya viwandani.
"Kiwanda hiki kitajengwa karibu na Bandari ya Tanga, lakini shamba kubwa la miwa litakuwa huku Pangani," amesema.
Amesema hilo litafungua fursa zaidi za ajira kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Pia, amemwagiza Ulega kufuatilia ili kuona uwezekano wa kuongeza safari za boti zinazotoka Tanga kwenda Unguja na Pemba.
Mbunge wa Pangani, ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema moja ya changamoto inayowakabili kwa muda mrefu ni barabara mbovu iliyopo kwenye jimbo hilo kuelekea Tanga mjini.
Hata hivyo, Rais Samia amemtaka Waziri Ulega kushinikiza ujenzi wa kilomita nane za barabara hiyo, kwa kuwa tayari fedha zimeshapatikana.
Imeandikwa na Juma Issihaka, Bakari Kiango na Rajabu Athumani