Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumaini mapya wakazi Tanga, mradi wa Daraja la Mto Pangani

Muonekano wa Daraja la Mto Pangani, litakalokuwa kiungo cha mikoa ya Tanga na Pwani (Bagamoyo) kupitia Barabara ya Afrika Mashariki.

Muktasari:

  • Mradi wa Daraja la Mto Pangani unatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na sasa umefikia zaidi ya asilimia 50.

Pangani. Suala la wakazi wa Pangani mkoani Tanga, kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine wa Mto Pangani kwa kutumia kivuko kinachotoa huduma kwa muda, halitakuwepo tena.

Badala yake, wananchi hao watakuwa na uwezo wa kuuvuka mto huo kwa saa 24, wakitumia vyombo mbalimbali vya usafiri.

Hatua hiyo itatokana na kukamilika kwa mradi wa Daraja la Mto Pangani unaotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ambao kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 50.

Muonekano wa Daraja la Mto Pangani, litakalokuwa kiungo cha mikoa ya Tanga na Pwani (Bagamoyo) kupitia Barabara ya Afrika Mashariki.

Kwa sasa, wakazi wa eneo hilo, wanavuka mto huo kwa kutumia kivuko maalumu, ambacho hata hivyo kinatoa huduma mwisho saa 4:00 usiku.

Leo Jumatano, Februari 26, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 525, jambo lililowaibua wananchi wa Pangani, wakisema litakapokamilika litawarahisishia kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Wamesema licha ya kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji, lakini daraja hilo litawasaidia kuvuka kwa urahisi kutoka upande mmoja kwenda mwingine badala ya sasa kutumia kivuko kinachotoa huduma kwa muda maalumu.

Ujenzi wa daraja hilo umefikia zaidi ya asilimia 50 ambapo ukikamilika utaunganisha mikoa ya Tanga na Pwani kupitia barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ipo katika ushoroba wa Pwani ya EAC unaoanzia Malindi- Mombasa Lunga Lunga Kenya, Horohoro na Tanga- Pangani- Bagamoyo wenye urefu wa kilomita 454.

Wananchi hao wameeleza hayo leo Jumatano Februari 26,2025 wakati wakimsubiri Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ataweka jina la msingi katika daraja hilo na barabara ya Bagamoyo (Makurunge) Saadani na Tanga – Pangani.

Ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Tanga.

Zainab Ramadhan ni mkazi wa Pangani amesema kilio cheo ni daraja kutoka upande wa Pangani kwenda ng’ambo ya pili, akisema kivuko wanachokitegemea ikifika saa nne au saa tano usiku hakitoi huduma.

"Changamoto ya kivuko hiki ikifika saa nne hakitoi huduma, lakini daraja likiwepo muda wowote tutakuwa na uhakika wa kupita na kufanya shughuli zetu kwa uhakika zaidi," amesema.

Mkazi mwingine, Mwanamkasi Sheria amesema kukamilika kwa daraja hilo, kutarahisisha kupata huduma kwa haraka hasa inapotokea dharura nyakati za usiku, ikiwemo kwenda hospitali kupata matibabu.

Naye, dereva wa bodaboda wilayani Pangani, Mahine Ally amesema, "kuwepo wa daraja hili utarahisisha shughuli zetu, mfano ukienda safari hautakuwa tena na mawazo sijui nitavuka saa ngapi na kivuko au kivuko kimezima...itakuwa ni mwendo wa kujiandaa na safari tu."

Dereva wa pikipiki maarufu bodaboda, Burhani Hassan amesema kuwepo kwa daraja hilo na ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Tanga hadi Pangani kutawawezesha kutumia nusu saa kufika Tanga mjini.

"Ukiwa ng’ambo ya pili ulifika kwenye kivuko unajikuta unapoteza muda wa zaidi ya saa moja kwa kusubiri kivuko ambacho kipo kimoja. Kilio chetu kikubwa ni daraja tunaishukuru Serikali kwa utekelezaji wa mradi huu," amesema.

Kwa upande wake, Chuda Hisani amesema uwepo wa daraja hilo utasaidia kukuza uchumi wa Pangani kupitia watalii watakaopita kuelekea mbuga ya Saadani iliyopakana na Bahari ya Hindi iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

"Watalii wengi walikuwa wanapenda kutembelea mbuga ya Saadani changamoto ilikuwa barabara na daraja sasa zinakwenda kupata ufumbuzi utakaowezesha shughuli za biashara wilayani Pangani kuchangamka," amesema Hisani.

Mwezi uliopita Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alikagua mradi huo, akamtaka mkandarasi kuharakisha ujenzi akisema ni kiungo muhimu katika barabara ya EAC itakayokuza uchumi wa wananchi wa Tanzania.