Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia: Kwa nini nateua majaji wanawake

Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Mzee Ramadhani Nyamka wakila kiapo cha Maadili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amebainisha kilichomsukuma kuteua majaji wanawake, kuwa ni weledi wao katika kazi na kwamba wanazingatia maadili yao ya kazi kuliko majaji wanaume.


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amebainisha kilichomsukuma kuteua majaji wanawake, kuwa ni weledi wao katika kazi na kwamba wanazingatia maadili yao ya kazi kuliko majaji wanaume.

Rais Samia aliyasema hayo juzi Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha majaji 21kati ya 22 wa Mahakama Kuu ambao aliwateua Agosti 6 mwaka huu pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), Mzee Nyamka.

Alisema lawama za wananchi dhidi ya Mahakama zimepungua nchini, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya majaji wanawake katika Mahakama ya Tanzania.

Aliongeza pia lawama hizo zimepungua kwa sababu ya usimamizi mzuri wa Mahakama, usimamizi mzuri wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (JSC), maboresho yaliyofanywa na tume, weledi wa majaji wanaoteuliwa na idadi kubwa ya majaji hasa wanawake wanaoteuliwa.


Akoshwa na wanawake

Kuhusu majaji wanawake, Rais Samia alisema majaji wanawake, wanatoa hukumu zao kwa kuangalia mazingira ya Kitanzania.

“Majaji wanawake wanakaa vizuri kwenye kuhukumu, wana extra (ziada) sifa kwenye kutoa hukumu kuliko majaji wanaume. Kwa hiyo lengo langu ni kuelekea 50 kwa 50 ili Mahakama ya Tanzania tukae vizuri zaidi.

“Kwa hiyo, majaji wanawake siwateui tu kwamba ni wanawake tu, hapana! Napima na sifa na uwezo wako na yale yote ambayo Tume itapendekeza kwangu,” alisema Rais Samia na kuwataka waende kufanya kazi.

Mkuu huyo wa nchi alisema ataendelea kuteua majaji kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu kwa sababu jaji akiteuliwa, stahiki za malipo na matumizi ya Serikali yanaongezeka.



Upendeleo maalumu

Rais Samia alibainisha huwa anafanya upendeleo maalumu kwa mhimili wa Mahakama na hajawahi kukataa ombi lolote la mhimili huo linalopelekwa kwake ikiwa ni pamoja na ombi la safari au mafunzo.

“Lengo langu ni kwamba mnakwenda kubadilishana mawazo na wengine, hata kama mnakwenda kwenye mkutano, mnajadiliana mnafanya vipi. Mnapokwenda kule mnajifunza kwa wenzenu, kama ni makosa mnajifunza kuepuka makosaa ambayo wenzenu wameyafanya.

“Kwa maana hiyo, sijawahi ku-turndown (kukataa) maombi ya majaji na nitaendelea kufanya hivyo, lengo langu mkajifunze. Mhimili wa Mahakama usimame na muachane na yale yaliyokuwa historia huko nyuma,” alisisitiza Rais Samia.

Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma alisema ongezeko la majaji 22 walioteuliwa na Rais Samia litawapunguzia mzigo wa mashauri majaji katika Mahakama Kuu na hatimaye kuharakisha uendeshaji wa kesi.

Pia, alisema uteuzi huo umeongeza uwiano wa kijinsia wa majaji ambapo idadi ya wanawake sasa imeongezeka hadi kufikia asilimia 37 ya majaji wote katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwa sasa.

“Ongezeko hili la majaji 22, litapunguza mzigo wa mashauri ambao mnaubeba kwa mwaka. Kila mwaka kabla ya uteuzi wa majaji hawa 22, jaji alikuwa na mashauri 340, baada ya kuwapata hawa 22, huo wastani utashuka hadi 265, kwa hiyo si haba.

“Kabla ya uteuzi wa majaji 22, majaji wanawake Mahakama Kuu walikuwa ni 27 kati ya 78. Hiyo ilikuwa ni asilimia 35. Baada ya huu uteuzi, sasa asilimia imepanda hadi 37, siyo haba, tunaendelea kuongezeka,” alisema Profesa Juma.

Mpaka sasa Mahakama ya Rufani ina majaji 25 ukijumuisha na Jaji Mkuu wa Tanzania. Kati ya majaji hao 25; Majaji 10 ni wanawake.


Agizo kwa Kamishna Magereza

Aidha, Rais Samia alimtaka Nyamka kwenda kufanya marekebisho ya tabia za wafungwa kwenye magereza yote nchini. Alimtaka kwenda kuiongoza taasisi hiyo kwa weledi mkubwa na kuzingatia haki za wafungwa.

“Wale (wafungwa) ni wanadamu kama wanadamu wengine, wanatakiwa kupata hewa safi, wanatakiwa kupata mavazi ya sare zao, wanatakiwa kupata chakula kizuri. Sasa siyo kwa kuwa ni wahalifu, adhabu ziwe nyingi nyingi, ile kumuweka mle pekee yake ni adhabu. Kwa hiyo, nenda kalinde haki zao,” alisema.

Rais Samia alibainisha changamoto nyingine zinazoikabili taasisi hiyo kuwa ni utawala bora, utawala wenye kusimamia haki, kufanya kazi ya kurekebisha tabia za wale wanaopelekewa.

“Si wale wote wanaoletwa kule ni wahalifu waliokubuhu, wengine wanafanya makosa kwa bahati mbaya, mwingine kosa limetokea yupo, ushahidi tunawajua majaji kazi zao wanavyofanya, saa nyingine unaambiwa ushahidi wa kimazingira unakutia makosani, pengine hakufanya,” alisema Rais Samia.

Wakati Rais Samia akieleza hayo, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka 2020/21 na Ripoti ya Uwajibikaji ya Mwaka 2020/21 zinabainisha dosari mbalimbali kwa jeshi la magereza.

Katika ripoti ya CAG, inabainisha upungufu wa watumishi 24,598 katika Idara ya huduma za magereza ikilinganishwa na idadi ya 12,765 waliopo kwa sasa hatua iliyochagiza uwepo wa madai ya watumishi yasiyolipwa Sh95bilioni kati ya 2019/21.