Rais Samia: Katiba si mali ya vyama vya siasa, ni ya Watanzania

Rais Samia Suluhu Hassan. Picha na Ikulu
Dar es Saalam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Katiba si mali ya vyama vya siasa bali ni mali ya Watanzania hivyo marekebisho yake yanahitaji tafakuri kubwa.
Ameeleza hayo leo Jumatatu Septemba 10, 2023 katika mkutano maalum wa baraza la vyama vya siasa na wadau wa demokrasia, akibainisha kuwa baada ya maoni ya pande zote wamekubaliana kuwa Katiba inahitaji marekebisho.
“Maoni yamekuja hapa kila upande, wale wa kikosi cha siasa, Zanzibar wote wamesema katiba na wote tukatoa kauli kwamba tunakubaliana marekebisho ya katiba yetu, lakini jambo hili ni mchakato na Katiba si mali ya vyama vya siasa, Katiba ni ya Watanzania, awe ana chama au hana. Katiba ni mali ya Watanzania kwahiyo marekebisho yake yanahitaji tafakuri kubwa sana."
“Hatuendi hivyo hii ni mali ya Watanzania, tunataka tukifanya marekebisho yatuchukue muda kitabu chetu kiende, lakini Katiba ni kitabu tunaweza tukatengeneza Katiba kitabu kizuri tukakipamba tukakiweka, wangapi wanakielewa hicho kitabu yaliyomo humo ndani wangapi wanaelewa, kitabu tulichonacho sasa wangapi wanakielewa unakwendaje kumuuliza Mtanzania nipe maoni yako kitu hakijui tunaanza na elimu ya Watanzania wajue ni kitu gani, kinasemaje kina nini," amesema.
Ameongeza, “Viongozi wa kisiasa tunadhani tuna haki ya kuburuza watu tunachokisema sisi watu wote wafuate waseme hivyo tunageuza watu makasuku."