Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia atoa maagizo Wizara ya Elimu, Necta kukomesha wizi wa mitihani

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ameshiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lililoanzishwa Novemba 21, 1973, huku akitoa maagizo juu ya kukomesha wizi na udanganyifu wa mitihani.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), kuhakikisha inakomesha vitendo vya wizi na udanganyifu katika mitihani kwa sababu bila kuwepo upimaji unaozingatia haki itakuwa vigumu kuzalisha ajira zenye tija.

 Kiongozi huyo amesema ili kufanikiwa kwa malengo ambayo Taifa imejiwekea, upimaji unaozingatia haki utasaidia kupata nguvukazi sahihi itakayoshiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa nchi.
Kauli hii imekuja wakati ambapo hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kwa wanafunzi na vituo vya mitihani vinavyobainika kufanya udanganyifu. Hivi  karibuni Necta ilitangaza kufuta matokeo kwa wanafunzi 31 wa darasa la saba kwa sababu ya udanganyifu.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Jumamosi, Desemba 16, 2023 katika maadhimisho ya miaka 50 ya Necta yaliyofanyika ofisi za baraza hilo, Bamanga jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo ametaka umakini uongezwe kwenye utungaji, usahihishaji na udhibiti wa mitihani na kuondoa mianya yote inayoweza kuruhusu wahitimu wasiokuwa na tija.

 Katika hilo alimuelekeza Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda kutofumbia macho vitendo vya udanganyifu kwa kuwa vinachangia kutengeneza nguvu kazi isiyo na uwezo wa kufanya kazi, akitolea mfano wa baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu kushindwa hata kufanya kazi za kawaida.

 “Tumetoka vyuoni, wote tunayajua yanayoendelea huko, sasa tukioa mianya ya watoto wetu kuijua mitihani kabla tunatoa wahitimu  wasiokuwa sawa vichwani, katika hili niombe sana uchujaji na udhibiti wa mitihani ufanyike kwa umakini mkubwa ili tutoe  nguvu kazi itakayokuja  kutumika vyema katika maeneo mbalimbali.

 “Changamoto ya udanganyifu lazima itafuatiwe mwarobaini, natumai wizara na baraza mtakuja na mikakati mizuri ya kushughulikia suala hili, kuweni wakali zaidi. Profesa Mkenda usiogope kulaumiwa lawama siku zote zipo kwanza ukiona unafanya jambo hausemwi basi ujue kuna shida mahali,” amesema Rais Samia.

 Akizungumzia hilo, Profesa Mkenda amesema katika kipindi cha miaka 50, Necta imekuwa chujio la kuwapata wanaostahili kwenda kwenye ngazi za juu na hata kulitumikia Taifa kupitia ajira zinazotolewa na Serikali.


“Hata kama chujio hili lina upungufu lakini Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo bado mitihani inaendeshwa vizuri barani Afrika. Kuna kipindi hapo nyuma kidogo nilipiga kelele kuhusu Necta na nikawa mkali kwa kuwa ulikuwepo  uvujishaji wa mitihani. Zilionekana dalili za mtihani kuvuja kutoka kwenye majengo haya hali ile ikadhibitiwa.

 “Kilichokuwa kinatokea na ndiyo tukalazimika kukikemea ni wizi wa kitaasisi, kinachofanyika ni shule moja inashirikiana na baadhi ya maofisa, mtihani unafunguliwa mkoa mwingine unapigwa picha halafu unafungwa tena na ile picha inatumwa mkoa mwingine,” amesema Profesa Mkenda.

 Waziri huyo amebainisha baada jitihada mbalimbali za udhibiti zilizofanywa na kamati za mitihani za mikoa na wilaya wizi huo umedhibitiwa, na majaribio ya aina hiyo hayafanikiwa.

  Katika hatua nyingine, Rais Samia ameielekeza Wizara ya Elimu kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), kuhahakikisha shule za pembezoni zinakuwa sehemu ya mradi unaowawezesha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi.

 Amesema kupitia mradi huo wanafunzi hata katika wanasoma maeneo ambayo hayanyasiyokuwa aa walimu wa sayansi watapata fursa ya kujifunza masomo hayo kwa njia ya mtandao.

 Pia, ameahidi katika bajeti zijazo kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo mitatu ya uchapaji mitihani, ambapo  kila mmoja utagharimu Sh6 bilioni.

 Kuhusu wanafunzi wanaopata daraja sifuri, Rais Samia amepongeza mpango wa baraza wa kufanya ufuatiliaji na tathmini mwanafunzi na kufanyiwa mipango ya kumuendeleza ili atumike  vyema katika ajira au kujiajiri, ili mradi awe na tija kwa Taifa.