Rais Samia ataka uwajibikaji COP28


Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza juu ya uwajibikaji hasa kwenye masuala ya utoaji fedha na kupunguza vichocheo vya mabadiliko ya tabianchi, huku akizitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao kwa sababu ni wazalishaji wakubwa wa hewa ukaa.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi zilizoendelea kuwajibika kwa kutoa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama walivyoahidi.

Ahadi ya kutoa fedha ya Dola za Marekani 100 bilioni (Sh250 trilioni) ilitolewa kwenye mkutano wa 15 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC – COP15) mwaka 2009.

“Copenhagen tuliahidi Dola 100 bilioni kila mwaka kukabiliana na athari za mabadilko ya tabianchi. Mpaka sasa imetoka kidogo kuliko ilivyopangwa,” amesema Rais Samia alipokuwa akihutubia COP28 kwenye mkutano wa Ngazi ya Juu wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaoendelea Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 70,000 kutoka nchi takribani 190.

Rais Samia pia amekumbusha kuwa licha ya dunia kukubaliana kuthibiti ongezeko la joto chini ya nyuzi joto 1.5 mpaka mwaka 2030 lakini hali ya sasa ya joto la dunia hairidhishi na inahitaji uwajibikaji.

Kutokana na madhara hayo Rais Samia amesema Tanzania inapoteza asilimia mbili hadi tatu ya pato la Taifa kila mwaka hivyo kusisitiza: “Ahadi ambayo haijatimizwa inaondoa mshikamano na uaminifu na kuwa na matokeo mabaya na ya gharama kubwa kwa nchi zinazoendelea. Muda umekwisha”.

Awali Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema ilikutimiza ahadi na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi ulimwengu, unahitaji uongozi - ushirikiano - na utashi wa kisiasa kwani mikutano hii ilikwishaonyesha njia za wazi za kufikia hatua hiyo muhimu.

"Ishara hatari zinaonekana duniani: uzalishaji mkubwa wa hewajoto, ukame na mwaka wa joto zaidi kuwahi kutokea tumeuona. Tupo mbali sana kufikia malengo ya Makubaliano ya kuthibiti joto. Lakini bado hatujachelewa,” amesema na kuongeza:

“Dunia inayo teknolojia ya kuzuia athari hizi kama inawajibika sasa. Nishati safi ipo na itaendelea kuwepo na ni jambo zuri kwa dunia, afya na uchumi,” amesema.

Akitoa maoni yake kuhusu kauli za viongozi zilizotolewa kwenye mkutano huo, Mhadhiri katika Kituo cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) Profesa Pius Nyada amesema kilichozungumzwa na viongozi wa nchi kinaakisi uhalisia wa wanayoendelea duniani na suala la uwajibikaji ni muhimu.

“Nchi za Afrika zinaathrika zaidi licha ya kuwa hazichangii kiasi kikubwa cha uchafuzi, hivyo nchi zinazoendelea zinatakiwa kuwajibika ili kama dunia tufikie malengo”.


Kuanzishwa kwa Mfuko maalumu

Ishara njema imeanza kuoneka baada ya mfuko maalumu wa fedha za maafa na majanga kuanza kufanya kazi na ahadi ya takribani Dola milioni 400 (Sh1 trilioni) ikitajwa na baadhi ya nchi.

Haya yanakuja kama utekelezaji wa makubaliano ya COP27, iliyofanyika Sharm El Sheikh, Misri na inalenga kusaidia nchi zinazoendelea ambazo ziko katika hatari kubwa ya athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi katika kukabiliana na hasara na uharibifu wa kiuchumi na usio wa kiuchumi unaohusishwa na athari mbaya.