Rais Samia amwandikia Putin barua Siku ya Ushindi Urusi

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemuandikia barua ya pongezi Rais wa Urusi, Vladimir Putin, akimpongeza kwa maadhimisho ya Siku ya Ushindi (Victory Day), siku inayokumbukwa kwa ushindi wa Urusi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia dhidi ya Ujerumani.
“Kwa niaba ya Watanzania, nakutumia salamu za pongezi za dhati kwa kuadhimisha siku hii muhimu ambayo inaakisi historia ya kujitoa kwa ajili ya uhuru na haki,” ameandika Rais Samia
Amesema kumbukumbu ya siku hiyo bado inaendelea kuzihamasisha nchi duniani kusimama kidete kulinda amani, haki na ushirikiano wa kimataifa.
“Tanzania inathamini kwa dhati uhusiano wake mzuri na Urusi, uhusiano uliojengwa juu ya kuheshimiana na mshikamano,” ameongeza Rais Samia huku akimtakia Putin na wananchi wake mafanikio na ustawi endelevu.
Siku ya Ushindi huadhimishwa Mei 9 kila mwaka nchini Urusi, ikiwa ni kumbukumbu ya ushindi wa mwaka 1945 katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambapo majeshi ya Umoja wa Kisovieti yalifanikiwa kuishinda Ujerumani ya Adolf Hitler.