Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Magufuli azindua mradi wa umeme wa megawati 132 Katavi

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Ijumaa Oktoba 11, 2019  amezindua mradi wa umeme wa Megawati 132 utakaohudumia Mkoa wa Katavi na mikoa jirani.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Ijumaa Oktoba 11, 2019  amezindua mradi wa umeme wa Megawati 132 mkoani Katavi.

Rais Magufuli amesema mradi huo utaokoa zaidi ya Sh5.5 bilioni zilizokuwa zikitumika kununua mafuta kwa ajili ya majenereta ya kufua umeme.

“Ni kweli Mkoa mpya wa Katavi umekuwa na tatizo la umeme na kwa dunia ya leo na kwa nchi ninayo plan (panga) ya viwanda huwezi ukawa na umeme wa jenereta.”

 “Matumizi ya mafuta kwa ajili ya kuwasha jenereta ili utengeneze umeme yamekuwa makubwa Sh6.5 bilioni kila mwaka inapotea na makusanyo ni Sh1 bilioni.

“Kwa hiyo mnatumia Sh5.5 bilioni sasa kwa maisha ya leo lazima kila kitu kibadilike,” amesema.

Amesema licha ya kwamba mahitaji ya umeme ya mkoa huo ni megawati 5, megawati 132 zinaweza kutumika kufungua viwanda.

Mbali na mradi huo amesema kuna miradi mingine ya umeme ukiwemo mradi wa umeme wa bwawa la Nyerere lililoko katika pori la akiba la Selous mkoani Pwani litakalozalisha megawati 2,115,

Mwingine ni mradi wa gridi ya Taifa utakaounganishwa kutoka Zambia utakaozalisha megawati 400 na kupita Katavi.

Awali, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema mradi huo ulianza Mei 2019 na unatarajiwa kukamilika Mei 2020.

Amesema mradi huo utagharimu Sh137 bilioni na ulianza kwa  kujenga kituo cha kusambaza umeme kitakachofungwa mashine mbili za megawati 50 kila moja.

“Kazi ya pili ni kujenga njia ya umeme ya Kilovolti 132 kutoka Kiloleni, kupita Inyonga na Ipole mpaka hapa. Mradi huu utajengwa kwa miezi 10 ni matumaini yetu mpaka Mei mwakani utakuwa umekamilika ili wananchi wa Katavi na maeneo yanayozunguka wataanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa na kuacha kutumia mafuta,” amesema.

Amesema awamu ya pili ya mradi huo itakuwa ni ujenzi na kilovoti 400 kutoka Iringa, kupita Mbeya, Sumbawanga, Tunduma, Katavi, Kigoma mpaka Nyakazi umbali wa kilometa 1,732.