Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jalada la 'Dk Manguruwe' latua FCU kukamilisha upelelezi

Mshtakiwa Simon Mkondya (aliyevaa kaunda suti) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Muktasari:

  • Mkondya na Rweyemamu wakabiliwa na mashitaka ya kuendesha upatu, kutakatisha fedha, matukio yanayodaiwa kuyatenda kati ya Januari Mosi 2020 na Desemba Mosi, 2023 Jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe, limepelekwa Kitengo cha Uhalifu wa Kifedha (Financial Crime Unit- FCU) kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama hiyo leo Jumatano Julai 9, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashitaka 28 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya pekee yake.

Hata hivyo, John ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu na pia hana mashitaka ya kutakatisha fedha.

Kasala ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu anayesikiliza shauri hilo.

"Jalada halisi la kesi hii limepelekwa FCU kwa ajili ya kukamilisha upelelezi wa kesi hii, hivyo kutokana na hali hii tunaomba Mahakama yako itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai wakili Kasala.

Hakimu Magutu baada ya kusikiliza taarifa hiyo, alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, 2025 kwa kutajwa.

Mshtakiwa Mkondya hakuletwa mahakamani hapo kwa sababu ni mgonjwa na badala yake kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video huku mshtakiwa huyo akiwa gerezani, lakini mshtakiwa wa pili ambaye yupo nje kwa dhamana alikuwepo mahakamani hapo.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2024.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, kati ya mashitaka hayo 28,  19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na tisa ni ya kutakatisha viwanja.

Inadaiwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa Mkaguzi wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.

Katika mashitakatisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Pia, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.