Prime
ACT Wazalendo inavyotumia changamoto za watawala kama fursa ya kuvuna wafuasi

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa chama hicho, wamekuwa wakijenga hoja dhidi ya changamoto hizo na kuonesha namna watakavyofanya kuzitatua, iwapo watapewa nafasi ya kushika dola Oktoba.
Ingawa kipyenga cha kampeni hakijapulizwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), lakini viongozi wa ACT Wazalendo wanatumia fursa ya ziara ya kuimarisha chama chao katika mikoa mbalimbali kueleza madhaifu ya chama tawala.
Viongozi hao, waliopo katika ziara ya siku 30 ya Operesheni 'Majimaji Linda Kura' wanaambatanisha hoja hizo na sababu ya chama hicho kushiriki uchaguzi huo, kikisema kinalenga kuhakikisha kinashika dola, kutatua kila changamoto iliyoshindikana na watawala.
Ni ziara ya kimkakati ambayo inafanyiwa utafiti na timu maalumu kabla ya kutia timu katika majimbo ya mikoa mbalimbali. Unaweza kusema ni ziara ya kujiweka mguu sawa kabla ya amsha amsha ya uchaguzi mkuu.
Hiki kinachofanyika na ACT Wazalendo hakina tofauti na ' road show' ambayo mara nyingi hutumiwa na viongozi wa kisiasa wa Kenya kuelekea kila unapokaribia uchaguzi mkuu wa taifa hilo jirani na Tanzania.
Katika ziara hiyo, ACT Wazalendo kumeibuka hoja na changamoto kadhaa ikiwamo migogoro ya ardhi na hali duni ya uchumi kwa wananchi, mambo ambayo kwa mujibu wa viongozi hao, hayatakuwa sehemu ya matatizo ya raia iwapo watakipa ridhaa chama hicho.
Liganga-Mchuchuma
Katika ziara hiyo, chama hicho kimeapa kuendelea kuuvalia njuga mradi wa Liganga na Mchuchuma unaolenga kukuza uchumi wa viwanda kwa kuanzisha sekta za msingi zitakazosaidia katika mnyororo wa thamani.
Akiwa mkoani Songea, kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe amesisitiza chama chake hakitachoka kuupigania mradi huo, uanze kwa sababu una faida na manufaa yatakayowanufaisha wananchi wa Ruvuma.
Mradi huo una thamani ya zaidi ya Dola 3 bilioni (takribani Sh7.8 trilioni) na unakadiriwa kuingiza zaidi ya Dola bilioni 1.2 (Sh1.3 trilioni) kwa mwaka kutokana na uzalishaji wa madini ya chuma, titani, vanadium na salfeti ya alumini.
Mapema mwaka huu, Waziri wa Viwanda, Dk Selemani Jafo alinukuliwa akisema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kimkataba za utekelezaji wa mradi huo.
Mradi huo unakadiriwa kuzalisha mapato ya Dola za Marekani 1.2 bilioni kila mwaka (zaidi ya Sh1.3 trilioni) kutokana na uzalishaji wa madini ya chuma, titani, vanadium na salfuti ya Alumini.
Hata hivyo, mradi huo una historia ndefu ya kuanzishwa kwake, tangu enzi za Serikali ya awamu ya nne na mikataba kadhaa ilikwama kwa kile kinachodaiwa kuwa haikuwa na maslahi kwa Watanzania.
Katika hotuba yake, Zitto anasema, "ACT Wazalendo tunataka mradi wa Liganga na Mchuchuma uanze mara moja na tutahakikisha unaanza kwa sababu faida yake ni kubwa mno.
"Tunataka kuona wananchi wa halmashauri mbalimbali wana miliki hisa katika uzalishaji na sikupewa zawadi za ujirani mwema au za kurudisha mchango kwa jamii," anasema Zitto ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini.
Anasema akiwa bungeni kila akisimama amekuwa akililia utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma lakini hadi sasa bado haujaanza kufanya kazi ili kuleta unafuu wa upatikanaji wa chuma nchini na kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo nje ya nchi.
"Tanzania imejaliwa chuma ambacho kinaweza kutumika kwa miaka zaidi ya 200 na bado kikabaki lakini wanaongoza wamekosa maarifa. Ajira za vijana hakuna, hakuna kwa sababu bidhaa za msingi za viwandani zinatokana na chuma ambacho bila makaa ya mawe huwezi kukiyeyusha," anaeleza.
Zitto amedai tangu aondoke bungeni mwaka 2020 uchangiaji wa wabunge unaolenga kuishinikiza serikali kutekeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma sambamba na makaa ya mawe yanayopatikana mkoani Ruvuma umekuwa wa kusuasua.
"Hivi wanajali namna ambavyo malori ya makaa ya mawe yanavyoharibu barabara? Au wanajali namna malori ya makaa ya mawe yanavyopinduka na kumwaga makaa ya mawe yanayoathiri afya za wananchi kutokana na vumbi? Hawajali," anasema Zitto.
Kutokana na hilo, Zitto anasema ndio maana ACT Wazalendo imeamua kushiriki uchaguzi ili kupambana hadi dakika za mwisho ili kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania wa maeneo mbalimbali.
"Hatua ya kwanza ni kuiondoa CCM ili kutekeleza sera mbadala, tukiendelea hivi maana kuwasikiliza watu wanaotaka tususie uchaguzi tutakuwa tumesalimu amri kwa watu ambao hawawezi kujiongeza hata kidogo," anasema Zitto.
Migogoro ardhi
Akiwa Mbarali mkoani Mbeya, Zitto alisisitiza mbinu ya kuondokana na migogoro wa ardhi inayohusisha hifadhi za taifa, mipaka na wawekezaji wilayani humo ni kuchagua upinzani hususan chama hicho. "Mgogoro wa ardhi haupo Mbarali pekee yake kila sehemu ya nchi kuna changamoto hii. Hii imesababishwa na sera mbovu za chama tawala," anasema Zitto.
Machi mwaka 2025, Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Stephen Wasira alitoa maelekezo kwa serikali iweke utaratibu mzuri wa kugawa sehemu ya ardhi kwa wananchi wa Mbarali ili itumike kwa shughuli za kilimo.
Maelekezo ya CCM yalitokana na malalamiko ya wananchi wa Mbarali waliosema wanashindwa kufanya shughuli za kilimo kwa sababu ya kuondolewa na serikali ili kupisha Hifadhi ya Mto Ruaha na kuwasababishia hali ngumu kiuchumi.
Katika maelezo yake, Zitto anawaambia wananchi wa Mbarali na Watanzania kuwa njia pekee ya kuondokana na migogoro ya ardhi ni kuiondoa CCM madakarani na kuweka upinzani.
Anasema iwapo chama hicho kitapewa nafasi ya kushika dola Oktoba mwaka huu, watahakikisha ardhi yote ‘iliyoporwa’ na kupewa wawekezaji inarejeshwa kwa wananchi.
"Tutapitia upya mipaka ya hifadhi na vijiji ikiwamo tatizo lenu la GN, kazi ya kumaliza mgogoro wa ardhi ndogo sana tupeni hii kazi sisi.Tutapitia upya mipaka yote kati ya mipaka na vijiji na tutaunda tume itakayopita vijiji vyote ili kuondoa migogoro," anasema Zitto.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) mwaka 2022, zaidi ya vijiji 920 vipo ndani ya mipaka ya hifadhi au mapori ya akiba.
Migogoro inayohusiana na mipaka imechangia zaidi ya asilimia 50 ya mashauri ya ardhi katika Mahakama Kuu ya Ardhi kwa mwaka 2023.
Mapambano ya haki
Akiwa mkoani Shinyanga katika ziara hiyo, kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu anasema ili kupatikane amani na utulivu nchini, serikali haina budi kuzingatia utendaji haki kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Kauli ya Dorothy, inajibu kilichoelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Kanisa la Arise and Shine, katika hotuba yake, aliposisitiza kuendelea kuwapo kwa amani na utulivu nchini.
Umaskini
Makamu mwenyekiti wa chama hicho bara, Issihaka Mchinjita anaeleza kushangazwa na hatua ya Mkoa wa Shinyanga kuwa wa nne kwa kuchangia katika Pato la Taifa, lakini ni miongoni mwa mikoa sita ambayo watu wake wanaishi chini ya mstari wa umasikini.
Mchango wa Shinyanga katika GDP ni Sh7.5 trilioni, ikiwa chini ya mikoa ya Mbeya, Mwanza na unaoongoza ni Dar es Salaam.
Mchinjita anasema hatua hiyo ni ithibati kuwa watawala wameshindwa kutimiza ahadi na malengo ya kuwainua wananchi kiuchumi na kujenga ustawi wa jamii. Anaeleza chama hicho kina dhamira ya dhati kuhakikisha kinaondoa umaskini kwa Watanzania kwa kuhakikisha kinatumia kila rasilimali iliyopo kwa ajili ya maendeleo.