Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Wabanhu kumrithi Mahalu SAUT

Muktasari:

  • Profesa Wabanhu anarithi nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Juvenalis Asantemungu ambaye alikuwa akiikaimu kufuatia changamoto za kiafya na baadaye kifo cha aliyekuwa Makamu Mkuu, Profesa Costa Mahalu.

Mwanza. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa amemteua Padri wa Jimbo Katoliki la Geita, Profesa Emmanuel Wabanhu kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT).

Pisa ambaye pia ni Kansela wa chuo hicho na Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi amesema uteuzi huo utaanza  Agosti Mosi, 2026.

Uteuzi huo umetangazwa jana Jumatano, Julai 15, 2026 kupitia taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha SAUT yenye makao makuu yake jijini Mwanza.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa  Profesa Wabanhu anarithi nafasi ya Profesa Juvenalis Asantemungu ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Makamu Mkuu wa chuo hicho kuanzia Juni 16, 2025 kufuatia changamoto za kiafya na baadaye kifo cha aliyekuwa Makamu Mkuu, Profesa Costa Mahalu.

Profesa Mahalu ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia alifariki dunia Machi 9, 2026 akiwa na umri wa miaka 77.

Msomi huyo mahiri wa sheria na mwanadiplomasia mkongwe alifariki dunia katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo umefanyika kwa kuzingatia masharti ya Hati ya Chuo Kikuu SAUT ya mwaka 2012 pamoja na marekebisho yake yaliyotolewa kupitia Tangazo la Serikali namba 580 la mwaka 2020 chini ya Sheria ya Vyuo Vikuu.

Profesa Wabanhu ni Padri wa Jimbo Katoliki  Geita na ni Profesa Mshiriki mwenye uzoefu  katika taaluma ya teolojia ya maadili akibobea katika maadili tetezi, msomi na mwalimu  anayejulikana kwa mchango wake katika taaluma hiyo.

Aliwahi kuwa  Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) Nairobi nchini  Kenya kwa zaidi ya miaka 13 na baadaye alihudumu kwa miaka miwili kwenye wadhifa wa  Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia utawala na fedha katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo cha Tabora (AMUCTA), Tanzania.

Katika mchango wake wa kitaaluma, Profesa Wabanhu ameandika vitabu vitano na kuchapisha zaidi ya makala 20 za kitaaluma katika majarida yanayotambuliwa kimataifa.

Ana Shahada ya kwanza ya teolojia kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana (Pontificia Università Urbaniana), Roma nchini Italia, Shahada ya Uzamili ya masomo ya dini, Shahada ya Uzamili ya teolojia, Shahada ya Uzamivu wa Teolojia Takatifu (STD) pamoja na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika maadili ya jamii (biashara) kutoka Chuo Kikuu cha Katholieke Universiteit Leuven, Ubelgiji.

Chuo cha SAUT kimempongeza kwa uteuzi huo na kueleza imani yake kuwa ataongoza vyema taasisi hiyo, huku kikitoa wito kwa wadau wote kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake mapya.