Profesa wa China atoa nondo Tanzania kunufaika fursa kidigitali

Mkurugenzi wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Peter Msofe wakati akizungumza katika mkutano wa pili wa kujadili kuhusu elimu ya sayansi kati ya Tanzania na China Jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Matumizi ya teknolojia ya kidigitali yametajwa katika sekta ya elimu yametajwa na wadau kuwa yaweza kuwa mwarobaini wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu ikiwemo uhaba wa walimu pamoja na vitabu.
Dar es Salaam. Imeelezwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasilino katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu mkazo yanataleta mapinduzi katika utoaji wa elimu nchini.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Julai 12, 2024 katika kongamano la kitaaluma lililowakutanisha wadau mbalimbali wa elimu pamoja na teknolojia kujadili matumizi ya teknolojia ya kidigitali katika elimu.
Akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Profesa Huang Xiao kutoka Chuo cha Zhejiang Normal kutoka China amesema matumizi ya teknolojia ya kidigitali itasaidia kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo pamoja na kuokoa muda na gharama.
Xiao amesema kupitia teknolojia ya kidigitali imefungua fursa mpya katika elimu, sasa mtu anaweza kujifunza chochote anachotaka kufahamu mtandaoni bila kujali mahala alipo.
"Pia kuna baadhi ya kozi zinazofundishwa mtandaoni hadi mtu anahitimu tofauti na awali ambazo ilimlazimu kuwepo katika chuo husika," amesema.
Amesema ufundishaji kwa njia ya mtandao umekuwa ni mbinu yenye manufaa hata katika kipindi ambacho kunatokea changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa ya kuambukiza pamoja na sababu za kijografia zinazoweza kuwa vikwazo vya mtu kupata elimu.
Ameongeza hata kwa wazazi sasa wanaweza kufuatilia maendeleo ya taaluma ya watoto wao kupitia mtandao.
"Kwa kiasi kikubwa matumizi ya teknolojia ya kidigitali katika elimu yatasaidia katika kuboresha utoaji wa elimu katika shule na vyuo mbalimbali," amesema.
Pamoja na kubainishwa kwa faida zinazotokana na teknolojia katika elimu wadau hao wadau wamebainisha vikwazo vinavyorudisha nyuma matumizi ya teknolojia katika elimu.
Baadhi ya vikwazo vilivyobainishwa ni pamoja uhaba wa vifaa vya kiteknolojia ya kidigitali, upatikanaji wa intaneti, wataalamu pamoja na baadhi ya watu kutokubali kubadilika kuendana na mabadiliko ya sasa.
Akizungungumza katika kongamano hilo, Dk Calvin Swai kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma amesema japokuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada katika kupeleka vifaa kama vile kompyuta, vishkwambi lakini bado havitoshelezi.
"Kunapokuwa na uhaba wa vifaa ni ngumu ufundishaji kwa njia ya digitali kufanyika kwa ufanisi," anasema.
Dk Swai pia amegusia suala la upatikanaji wa intanet haswa maeneo ya vijijini pamoja na uwepo wa walimu wachache wenye maarifa kuhusu masuala ya teknolojia.
"Tusiishie kunyoosha vidole na kulaumu tujiulize sisi wenyewe kama wasomi tunafanya nini katika kuhakikisha teknolojia inatumika katika elimu"amesema.
Vilevile aligusia suala la baadhi ya watu ikiwemo walimu kutokubali kubadilika kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Akitolea mfano baadhi ya walimu ambao wamepata vifaa ikiwemo vishkwambi hawavitumii katika kufanya kazi zao.
Kauli hiyo pia imeungwa mkono na Profesa Leonard Msele ambaye amesema kila mtu anatakiwa kujiona kuwa ana wajibu wa kufanya teknolojia itumike katika maisha yetu ya kila siku.
Awali, wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Profesa Peter Msofe ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema kongamano hilo limekuja katika kipindi muafaka ambapo serikali iko katika maboresho ya mitaala.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye amesema katika kipindi hiki matumizi ya sayansi na teknolojia hayakwepeki.
Ameongeza kutokana na umuhimu huo wa teknolojia chuo hicho kimekuwa kikitenga takribani bilioni tatu kila mwaka kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo masuala ya teknolojia.
"Kupitia tafiti itatupa mwanga wa hali halisi ilivyo na ni hatua gani zinatakiwa kuchukuliwa kufikia maendeleo makubwa katika upande wa teknolojia,” amesema.