Lugha ya Kiswahili kuuzwa nje ya nchi

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (Masikidu 2024) yaliyofanyika leo Julai 7 jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Leo ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani (Masikidu 2024), yaliyofanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam ambayo ni ya tatu tangu kuanzishwa kwake ambapo katika maadhimisho hayo Kiswahili kimetakiwa kufanywa bidhaa.
Dar es Salaam. Wakati lugha ya Kiswahili ikizidi kuchanja mbuga kwa kutambulika na kutumiwa na watu wengi ulimwenguni, lugha hiyo inafanywa bidhaa ili kuwanufaisha Watanzania.
Hatua hiyo inakuja ikiwa kuna watumiaji zaidi ya milioni 500 duniani kote wanaotumia lugha hiyo adhimu.
Hayo, yameelezwa leo Julai 7, 2024 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro, kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani (Masikidu 2024), yaliyofanyika kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam. Ambapo maadhimisho hayo yanafanyika kwa mara ya tatu.
Dk Ndumbaro amesema katika kutekeleza hilo lazima machapisho yote ya Kiswahili yafanyike hapa nchini hivyo ameagiza mabaraza ya Kiswahili likiwamo Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza) kutekeleza hilo sambamba na kuwawezesha watunzi wa vitabu na mashairi na wote wanaojihusisha na kazi zake.
"Pia tunapobidhaisha Kiswahili tunaangazia suala la utangazaji kwa kuwachukua watangazaji wetu kuwapeleka nje katika vituo mbalimbali vya redio na luninga za Kiswahili wakafanye kazi huko.”
"Aidha, tutumie sanaa kama muziki, filamu, mavazi tutambue Kiswahili kitakua bidhaa kubwa duniani lazima tuchangamkie fursa hii," amesema.
"Lazima tujipange ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI) , mitandao ya kijamii, kamusi mpya katika kukuza Kiswahili na ili kikue lazima tufungamanishe na teknolojia, vijana na mitandao ya kijamii kwa sababu lugha inakuzwa na vijana,' amebanisha.
Aidha amesema mabaraza ya Kiswahili ya Bakiza na Bakita yaendelee kukuza kanzidata ya wataalamu wa lugha hiyo. "Bakita na Bakiza shikamaneni mje na kamusi ya lugha fasaha ya Kiswahili ambayo tutaenda kuizindua nchini Uganda."amesema.
Dk Ndumbaro amesema, “tunataka Kiswahili iwe lugha rasmi ya saba ya Umoja wa Mataifa, kwa sasa kuna lugha sita na zote hamna hata moja ya kutoka Afrika hivyo tuingize ya Kiswahili inayokubalika.
Msigwa abainisha namna Kiswahili kitakavyouzwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amezifichua fursa zilizojificha katika ubidhaishwaji wa lugha ya Kiswahili kupitia mradi wa Wizara uitwao ‘Kubidhaishwa Kiswahili’, wenye lengo la kukieneza na kukiuza nje ya Tanzania.
"Watu watajifunza Kiswahili duniani hivyo tutapeleka walimu kwenye vituo 100 na vyuo mbalimbali kukifundisha huko mpango huo ukiwa tayari kuna walimu tutawapeleka huko.
"Tumepanga kuandaa machapisho mbalimbali tutakaoyasambaza huko duniani kwa sababu kwenye kujifunza lazima yawepo machapisho ikiwemo kamusi na vitabu mbalimbali.”
Msigwa ameongeza kwamba kuna nchi zilizoitikia zikiwemo Ufaransa, Kenya, Burundi, Afrika Kusini, Rwanda kwa sasa wanakamilisha taratibu kuchukua walimu kwenda kufundisha.
"Nitoe rai kwa vijana wasikibeze Kiswahili wale waliopo vyuoni, shule za msingi wajue ni lugha, utamaduni na biashara ajira yake itakua kubwa, na fursa ni nyingi hivyo wanapaswa kubobea huko kuna mahitaji makubwa," amesema.
Amesema kuna maofisa wa balozi wamemwambia watapeleka walimu 10 mwezi ujao nchini Marekani na walimu wengine nchini Switzerland.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Consolata Mushi amesema wameweka mikakati ya kukuza Kiswahili isiwe kama chombo cha mawasiliano pekee bali katika nyanja nyingine ikiwemo uchumi.
"Lengo letu ni kuwawezesha wadau wapate fursa ikiwemo kufundisha lugha hii na kufanya kazi katika vyombo mbalimbali duniani vyenye idhaa za Kiswahili kama ilivyo kauli mbiu yetu ya mwaka huu isemayo 'Kiswahili na Fursa za Maendeleo Duniani'.
Ameongeza kwamba maadhimisho ya leo ni sehemu ya kuitikia wito wa Kiswahili kutambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuadhimishwa mnamo Novemba 23, 2021 ambapo kwa mara ya kwanza yaliadhimishwa Julai 7, 2022, kisha 2023 na leo 2024.
Hata hivyo, Julai Mosi mwaka huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeipitisha lugha hiyo kuadhimishwa kila ifikapo Julai 7.
Naye, Waziri wa Habari, Vijana, Tamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Mwita amesema maadhimisho ya leo ni kuendelea kupeperusha bendera ya Kiswahili. Amesema maadhimisho ya mwaka 2025 yatafanyika visiwani Zanzibar.
"Tunazidi kuwahamasisha Watanzania lakini hata viongozi wetu wanapokwenda nje ya nchi kuendelea kuzungumza Kiswahili. Tunataka kuhakikisha Kiswahili kinakuwa bidhaa na kinatuletea kipato," amesema Mwita.
Naye, Mwakilishi mkazi wa Unesco hapa nchini, Michael Toto amesema Kiswahili ni chombo muhimu katika kufundishia, kuwasiliana na hata katika uchumi hivyo hakuna budi kuendelea kufanya kazi kwa pamoja.
Pia, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia video iliyorekodiwa mahususi kwa ajili ya maadhimisho hayo alisema Kiswahili kitumike katika kujenga amani na kufundishia maadili mema, kukuza bishara na kufikisha malengo ya maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.